‘Barrick imetunyanyasa sana...’
KAMPUNI ya African Barrick Gold, inayochimba dhahabu nchini, inatuhumiwa kutelekeza wafanyakazi wake waliopata maradhi hatari ya uti wa mgongo na mapafu wakiwa kazini.
Wanaotuhumu Barrick kwa kuwatekeleza, ni Sylvester Paul Chagato, Haji Luge, Emmanuel Mkama na Shaban Kanda.
Nyaraka zao zinaonyesha walikuwa wanafanya kazi za uchimbaji chini ya ardhi kwenye mgodi wa Bulyahulu, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Gazeti hili lilikutana na wagonjwa hao wiki mbili zilizopita, jijini Dar es Salaam ambako wanafuatilia matibabu katika hospitali za Muhimbili na Aga Khan.
Aidha, lilihojiana na Meneja Uhusiano wa Barrick, Teweli Teweli ambaye amekiri kuwa anafahamu “matatizo yanayowakabili wananchi hao. Lakini hili si tatizo la Barrick pekee...linaikumba migodi karibu yote nchini.”
Anasema, “Tunajitahidi kuwahudumia wale wanaoathirika. Hata hivyo, hatuna sera ya kutoa msaada wowote kwa familia zao kwa sasa, kutokana na ukweli kwamba wengi wao tayari tumewafuta kazi tokea mwaka 2007.”
Ripoti ya daktari mmoja kutoka hospitali ya Aga Khan imethibitisha Shaban Kanda, aliyeandikishwa hospitalini hapo kwa kadi Na. 33-25-07 na Haji Luge mwenye Na.19-64-49, waliambukizwa maradhi ya uti wa mgongo kutokana na kazi walizokuwa wakifanya mgodini.
Luge alifika hospitalini hapo tarehe 13 Mei 2011, wakati Kanda alifika Agosti 2007.
Katika ripoti yake ya 3 Machi 2011, daktari huyo anasema, “Shaban Juma Kanda, amepata maradhi ya uti wa mgongo kutokana na kuinua vitu vizito, kuinama kwa muda mrefu na kusimama kwa muda mrefu.”
Aliagiza kampuni ya Barrick kumpatia godoro maalum – Orthopedic bed – jambo ambalo Kanda anasema, pamoja na mengine, “halijatekelezwa mpaka sasa.”
Daktari huyo alikuwa akijibu barua ya Barrick ya 26 Mei 2011 iliyotaka kufahamu maradhi yanayomsumbua Luge kama yamesababishwa na kazi za mgodi.
Kuhusu Luge, taarifa ya daktari inasema, “...alifanyiwa upasuaji wa tumbo mara tatu na anategemewa kushauriwa tena, kutokana na kupata ajali akiwa chini ya mgodi.” Anasema, hospitali hiyo haiwezi kumfanyia upasuaji mwingine kutokana na mgonjwa kutokuwa na fedha.
Taarifa nyingine ya daktari mwingine, ambayo MwanaHALISI inayo, inathibitisha pia Mkama kupata maradhi ya uti wa mgongo; ikileleza kuwa yanasababishwa na “ubebaji wa vitu vizito katika maeneo ya migodi.”
Kabla ya kupelekwa kwenye hospitali ya Aga Khan, Mkama alipata matibabu katika hosiptali ya rufaa ya Bugando, jijini Mwanza.
Ripoti ya daktari inaonyesha Mkama aligundulika kuwa na maradhi hayo Agosti 2008, alipofanyiwa uchunguzi Bugando.
Chagato aliyegundulika kuwa na ugonjwa wa uti wa mgongo 21 Machi 2011, baada ya kufanyiwa uchunguzi na madkatari bingwa kutoka hospitali ya taifa ya Muhimbili anasema, “Hata nikipona madkatari wangu wanasema sitakuwa na uwezo tena wa kufanya kazi.”
Akiongea kwa uchungu, Chagato anasema, “Barrick hawana utu...wamenisimamisha kazi na wananilipa nusu mshahara, wakati matatizo haya nimeyapata kazini kwao.”
Anasema, “…nina uhaba mkubwa wa baadhi ya dawa. Nikiwaambia Barrick hilo, wanasema nitumie pesa zangu, wakati mimi wananilipa nusu mshahara na ninawadai zaidi ya Sh. 4 milioni nilizotumia kwa matibabu huko nyuma.”
“Tumeteseka sana…Angalau sisi tumediriki kufuatilia matibabu, lakini wako wengine kule kwetu wanasubiri kufa. Wengine tayari wamefariki dunia kwa maradhi hayahaya,” anasimulia Chagato.
Naye Kanda anasema, “Nimekata tamaa. Mpango wangu wa mwisho ni kujinyonga pale njia panda ya kuelekea ikulu. Viongozi wetu wanasherehekea kupanda ndege za Barrick, wakati sisi tunakufa.”
“Binafsi, sina uwezo tena wa kuitwa mwanaume. Mke wangu alikwishaondoka siku nyingi. Siwezi hata kuhudumia wanangu…kufanya kazi Barrick ni kosa la jinai? Hawa watu wanapata wapi jeuri hii?”
Akijibu madai hayo, Teweli anasema, “Hatuwezi kuwapa pesa watu hao kwa sababu ni kinyume na utaratibu wetu. Na hata familia zao hatuwezi kuwapa msaada wowote kwa sasa labda wasubiri tathmini ifanyike ili waweze kulipwa fidia.”
Hata hivyo, Teweli anasema, “...kuhusu kumnunulia Kanda godoro maalumu, kampuni inalifahamu na inalifanyia kazi.”
Mtaalamu wa magonjwa ya binadamu, na hasa ya migodini kutoka Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili, Dk. Yahya Kishusha, anasema tatizo kubwa la makampuni ya uchimbaji madini, ni kujali zaidi usalama wa migodi badala ya afya za wachimbaji.
Anasema migodini ni mazingira hatarishi sana kiafya, ambayo yanaua taratibu kutokana na kuvuta mfululizo hewa yenye vumbi ijulikanayo kwa kitaalamu kama silicosis.”
Kwa mujibu wa Dk. Kishusha, silikosisi ni maradhi yanayoathiri mapafu, yakisababishwa na uvutaji wa hewa ya sumu ambayo imetawala mno katika karibu migodi yote ya Barrick na hata migodi mingine nchini.
Ugonjwa wa silikosisi hushambulia mapafu na kusababisha upungufu wa pumzi, kuleta kukohoa na homa kali, huku rangi ya ngozi ya mwanadamu ikigeuka kuwa ya kibluu.
Kwa mujibu wa madaktari hao, wagonjwa wenye dalili hizo, mara nyingi hudhaniwa kimakosa kwamba wana uvimbe au maji ndani ya mapafu yao au wana magonjwa ya nyumonia au kifua kikuu.