‘Shutuma zimeua vita ya ufisadi’


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 January 2012

Printer-friendly versionSend to friend

LAZARO Nyalandu, Mbunge wa Singida Kaskazini alipoteuliwa Desemba 2010 kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara alifurahi na aliapa kutumia uwezo wake wote kuwatumikia wananchi.

Alianza kwa kasi, akaeleza malengo yake alipokutana na hakika alizungumza kwa upana alivyokusudia viwanda visaidie kukuza pato la taifa.

Weledi wake huonekana hata anapopata fursa ya kujibu maswali bungeni. Anajiamini. Lakini mwaka mmoja wa kutekeleza majukumu yake na kutatua changamoto mbalimbali, Nyalandu anasema; “Nchi imejaa lawama”.

Nyalandu anasema katika kipindi cha mwaka mmoja ameshuhudia makundi mbalimbali ya watu wakilaumu; wananchi wanalaumu serikali, wapambanaji wanalaumu mafisadi, serikali inalaumu wanaobeza, mafisadi nao wanashutumu wanaoeneza shutuma.

“Nchi imejaa lawama, serikali inalaumu hawa, wanasiasa wanatuhumu wale, ndani ya CCM kuna kushutumiana. Hali hii inaangamiza wananchi,” anasema Nyalandu.

Katika mahojiano na MwanaHALISI yaliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam, Nyalandu alisema kutokana na kukithiri kwa shutuma hizo, hata mapambano dhidi ya ufisadi yamepoteza mwelekeo.

Kwa mujibu wa Nyalandu, shutuma zinazotolewa na viongozi wa dini, vyombo vya habari, viongozi wa serikali, wanasiasa, wanachi zimeacha makundi yote yakinyoshena kidole bila kupata ufumbuzi wowote katika vita dhidi ya mafisadi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndicho kilianzisha kampeni dhidi ya mafisadi mwaka 2007 na kilitaja majina 11 ambao ni viongozi wa serikali ya CCM.

Baadaye CCM ilidaka na ikaanzisha falsafa ya kujivua gamba ikilenga wanasiasa nguli watatu. Mbunge wa zamani wa Igunga, Rostam Aziz (kwa ushiriki wake katika suala la Richmond/ Dowans) sawa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge (kwa vijisenti).

Rostam alipojiuzulu Julai 2011, CCM walichekelea na kuona wanafanikiwa, lakini wakashindwa kushinikiza Lowassa na Chenge kujiuzulu. Kibao kikageuka, nao wakapata nguvu ya kujibu mapigo kwamba hawajui tuhuma dhidi yao.

“Hata akili ya kuondokana na ufisadi sasa imefutika,” anasema Nyalandu na kuongeza ufisadi mwingine ni matumizi mabaya ya muda wa kazi.

“Mtu anaingia ofisini saa 2.00 asubuhi, anafanya kazi kidogo kisha anakwenda kufungua kinywa. Anakunywa chai anatumia saa nzima. Kisha mchana anakwenda lunch (chakula cha mchana) anatumia zaidi saa mbili, huo nao ni ufisadi.”

“Inafahamika kwamba kuna baadhi ya watumishi wa serikali hawawajibiki ipasavyo, hawatimizi wajibu wao. Huu nao ni ufisadi,” anasema.

“Hebu tazama, hadi mwaka jana taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha kuwa walipa kodi Tanzania hawazidi milioni. Katika nchi yenye wananchi wanaofikia 50 milioni hapo lazima kuwe na ufisadi. Kuna watu wengi hawalipi kodi huo nao ni ufisadi,” anasema.

Naibu waziri huyo anasema kinachoendelea sasa watu wameacha kufanya kazi badala yake wanazungumzia urais 2015 kwa siasa za kuwindana ndani na nje ya chama.

“Kuwindana kumekuwa sera, ni sehemu ya maisha ya kisiasa kwa baadhi ya wana CCM na hata upinzani, wamesahau makujumu yao,” anaeleza.

Athari zake zimeanza kuonekana kwani “sasa imefika hatua ya watu kukodoleana macho. Wanaangalia mtu mmoja mmoja, ukionekana wewe unasaidia kundi moja basi ni adui.”

Akijipima uzito kisiasa na akitahmini hali ilivyo sasa, Nyalandu anasema hana mpango wa kuwania urais mwaka 2015 na anawashauri wanaofikiria ikulu kuwa huu si wakati mwafaka kuonyeshea nia mapema.

“Kwa anayetaka urais kwanza angoje. Maana tuna rais ambaye amebakiza miaka minne ya kipindi chake,” anasema naibu waziri huo anayetajwa kujificha kwenye makwapa ya baadhi ya makada wa CCM wanaowania urais.

“Pili, ukifika muda afikirie kutuondoa katika tope la ufisadi maana dhana ya ufisadi naiona pana. Hatuna budi kuufukuza ufisadi nyumba kwa nyumba, mtaa hadi mtaa,” anabainisha.

“Tatu anayeota nafasi hiyo, ajipambanue katika dhana ya ukweli namna atakavyowaaminisha wananchi kama kweli anachukia ufisadi na awe na rekodi nzuri ya utendaji.”

Kwa upande wake alisema hana kundi ingawa anatajwa kuwa nyuma ya baadhi ya makada wa CCM wanaotajwa kuwania urais. Miongoni mwa wanaotajwa sasa ni Lowassa; Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe.

“Nina marafiki wengi. Lowassa ni mzee wangu. Ninamheshimu na ninamtembelea kwake na kunywa hata chai, lakini hakuwahi kuniambia wala sijamsikia akitangaza kutaka urais.

“Membe ni rafiki yangu, nakwenda hadi jimboni kwake maana sisi tupo kwenye ubunge tangu mwaka 2000, hajaniambia na sijamsikia akitangaza kuwania urais labda aseme ‘ooh nisaidie…kadhalika mzee wangu Sitta,” anasema.

Kuhusu utata wa uraia wake, Nyalandu amesema “nina uraia wa Tanzania tu” hata watoto wake wawili japokuwa walizaliwa Marekani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: