‘Tuwatie moyo wana - CCM, wataelewa’
KURA za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeibua makubwa. Kwa mara ya kwanza, wanachama wa chama hiki, angalau wameweza kung'amua janja ya wenzao wanaowatumia kama “shamba la bibi.”
Wamefanikiwa kuangusha mibuyu. Hii ni hatua ya kutia moyo na kuigwa.
Kila mara tukiwaambia kuwa wanatumiwa, hutuchukulia kama wapinzani na wasiolitakia mema taifa ingawa si kweli.
Bali ni lazima wakumbuke, katika kuteseka hakuna cha itikadi, uanachama, upenzi wala ushabiki. Kila mmoja ataguswa na hali itakayojitokeza.
Hii maana yake ni kwamba kama wana-CCM watajitambua, tunaweza kushirikiana nao kulikomboa taifa letu toka kwenye makucha ya mafisadi wanaozidi kutuzamisha kwa kutumia lugha tamu zenye matokeo machungu.
Nani alitegemea mibuyu na vigogo kama John Malecela, Joseph Mungai, Jackson Makweta na vingine vingefyekwa ikiwa ni tahadhari kuwa watu wetu wameanza kujitambua?
Sasa wamethubutu na kutoa tangazo rasmi kuwa hakuna dezo au mchekea tena. Bahati mbaya sana wameshindwa kung'oa vigogo wa ufisadi; wale waliosalia kwenye nafasi za juu za uongozi wa nchi.
Sijui ni bahati mbaya au kulikuwa na mipango. Hii ni kwa sababu, wengi walioangushwa si watu waliowahi kugubikwa na tuhuma nzito za matumizi mabaya ya madaraka, wizi na ufujaji wa rasilimali za taifa.
Bali, wengi walioshindwa wamekataliwa kutokana na umri wao. Kwamba wamekaa madarakani kwa muda mrefu na bila mabadiliko ya maana katika maisha ya wapigakura wao.
Wametudharau hadi kutupandikizia na watoto na marafiki zao. Ni dharau kiasi gani!
Tusiwabeze wala kuwadharau waliowezesha hili hata kama ni kidogo. Wana kila turufu ya ukombozi wa taifa hili; sawa na kila turufu ya kuweza kulikwaza kama ambavyo imekuwa miongo nenda rudi.
Lazima tushirikiane kuwatambua na kuwakabili na hatimaye kuwatokomeza adui zetu. Bila mashabiki wa maangamizi yao, CCM haina nguvu wala bao. Hii ni siri ya kuwajua na kuwashinda adui zetu – ufisadi na usanii.
Shida hazina rangi wala itikadi. Shida ni shida na ufisadi ni chanzo cha shida zetu. Shule ambazo watawala wanajigamba kwamba wamejenga na kusimamia, hazina walimu, hazina vifaa vya kutendea kazi na hazina maabara ya kufundishia.
Ni matundu matupu ya kupokelea ujinga na umaskini. Hili ni jambo la msingi na hatua moja katika kutatua tatizo letu sugu-ubabaishaji, ufisadi, usanii na mengine kama haya.
Wakati umefika wa kuachana hongo za -shirt, pesa kidogo, vijisimu uchwara na mengine. Watanzania hawawezi kuishi kwa kutegemea vitu hivi, bali uongozi bora wenye uchungu wa nchi na watu wake tena unaowajibika vilivyo kwa umma.
Wakati umefika wa wananchi hasa wapiga kura na wanachama kuacha kujirahisisha kwa matapeli wa kisiasa wanaotumia mshikamano feki kuharibu na kuangamiza taifa.
Kama walivyoweza kuangusha mibuyu, ni jukumu lenu sasa kututia shime tufagie takataka zote kuanzia juu kwenda chini. Tuwaulize hawa wanaojiita wanachama wenzetu. Wametufanyia nini kama taifa? Wametimiza ahadi ngapi?
Kisima cha maji safi au shule hata zahanati na barabara havina itikadi rangi wala ushabiki. Wajawazito wanaotaabika na kuabika pale Mwananyamala, Temeke, Kagunga, Ilala, Kimanzichana, Namanga na kwingineko wanapata yote haya bila kujali itikadi wala kabila na mkoa wa mtu.
Nani alitegemea kungekuwapo serikali ya mseto visiwani Zanzibar kama si subira na busara za wanachama wa upinzani? Kwanini upande mmoja uweze wa pili ushindwe wakati matatizo yao yanafanana na kusababishwa na kundi moja?
Kwanini watu tena wachache kwa idadi waweze, lakini walio wengi washindwe?
Watoto wanaokaa chini hawajui itikadi sawa na shida zao ambazo hazijui itikadi. Tuwaambie wenzetu ukweli – shida hazijui ushabiki. Kwenye uchaguzi ujao tuchague maendeleo badala ya mazoea.
Wale wenzetu ambao bado wako kizani kiasi cha kulala kitanda kimoja na mafisadi wajulikanao, tuwaelimishe kwa upole badala ya kubishana kiasi cha wao kutufungia milango ya maarifa.
Tuwaite, kwa sababu hawa ni Watanzania wenzetu. Tuwaeleze, tena kwa utuo, kuwa maisha magumu hayajui itikadi na kujinasua nayo ni kuwa na serikali inayowajibika kwetu.
Waelewe kuwa umaskini na mateso yao si wa kuumbwa na Mungu, bali watu, tena wanaowarubuni wakawapa kura kama kibali cha kuendelea kuwatesa na kuwanyonya.
Waeleze waziwazi kuwa misongamano barabarani ambayo rais alisema ni dalili za “maisha bora,” inaathiri watu wa itikadi zote.
Misongamano kwenye nyumba chafu na kulanguliwa viwanja hadi sehemu za wazi, rushwa na kupanda kwa bei za bidhaa, vinaathiri watu wa vyama vyote hata kama vimeundiwa CCM.
Uchafu mitaani, unyanyasaji wa polisi hata mgambo, mauaji ya vibaka, vikongwe na albino; ukosefu wa usalama na huduma muhimu na uonevu mwingine, vinaathiri wote, katika vyama vyote na itikadi zote, hata kama vimeshamiri wakati wa utawala wa CCM.
Waelimishwe kuwa ukosefu wa mbolea na pembejeo; ukosefu wa bei nzuri na masoko kwa mazao ya wakulima; aibu na adha zitokanazo na umaskini vyote vinaathiri wote katika jamii isipokuwa tabaka linalonufaika kutokana na ufukara wetu.
Waeleze waelewe kuwa hawa wanaowahonga wanatumia pesa ileile ya kashfa zinazonuka nchini kama vile EPA, Kagoda na nyingine.
Fedha zilizoibwa na zinazoendelea kuibwa, kama zingetumika vizuri, tungekuwa mbali mbele na si nyuma tulipo sasa.
Waelimishe wajue. Hawa wanaowahadaa na na kuwatumia hawawependi wala kuwawakilisha, bali wanawakilisha matumbo yao. Waelimishe kuwa hawa wanawadharau na kuwaona kama taahira.
Kwa hiyo, wana-CCM wakielewa na kukubali ukweli huu, kuwa wana nafasi katika kulikomboa taifa letu, basi tutashinda mapambano kwa faida yetu sote kama taifa.
Na wasitwambie kuwa hakuna chaguo. Lipo. Ni Dk. Willibrod Slaa ambaye wanajua utendaji wake na hasa pale alipofichua kashfa karibu zote zilizowaacha uchi mafisadi wakubwa na wadogo – waliopo hata waliopita.