…ni kupora, kujeruhi, kuua

JICHO la Baraka Nyamhanga “limekufa.” Mmoja wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wanaolinda mgodi wa North Mara alifyatua risasi, ikatua sikioni mwake na kutokezea jicho la kulia. Halioni tena.
Ni sehemu ya mtindo wa ulinzi wa askari wa migodi nchini – kupora, kujeruhi na kuua.
Hii ilikuwa tarehe 12 Desemba 2009. Baraka, mwenye umri wa miaka 15, alikuwa akichunga ng’ombe karibu na eneo kavu la tuta la kuzuia maji yenye sumu ya cyanide kutoka machimbo ya Nyabirama katika mgodi huo.
Kesho yake, Baraka alikuwa aende kuchukua fomu za kujiunga na Shule ya Sekondari Nyamongo. Hakwenda. Asingeweza kufanya hivyo. Alikuwa taabani akihangaikiwa kupata matibabu.
“Risasi iliniumiza vibaya. Baada ya kupigwa nilianguka chini. Nilibaki hapo nikilia kwa maumivu makali. Askari yule alikuja akaniamuru, ‘Amka! Nitakupiga risasi nyingine,’ ” anaeleza.
Baraka anasimulia kuwa kabla ya kupigwa risasi alikuwa ameketi na kupitiwa na usingizi mwembamba. Ghafla alistushwa na watu wanaokimbia, ndipo naye akakurupuka na kuanza kukimbia.
Ni moja ya risasi walizokuwa wakirushiwa wananchi iliyotua sikioni mwa Baraka na kutokezea jichoni.
Wakati Baraka akiwa bado na yule askari aliyemjeruhi, walifika wafanyakazi wa mgodini ambao walimpeleka mgodini na baadaye kumpeleka hospitali ya Tarime kwa ajili ya huduma ya kwanza.
Kesho yake alipelekwa hospitali ya mkoa wa Mara mjini Musoma ambako alichukuliwa picha (x-ray) ili kujua ukubwa wa tatizo.
Kutoka Musoma alipelekwa hospitali ya rufaa ya Bugando, Mwanza ambako alipata matibabu kwa gharama za mgodi. Alitoka hospitali tarehe 31Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa Baraka, Bugando walisema “jicho limekufa na hakuna uwezekano wa kulirejesha,” bali anasema walimshauri awaambie Barrick wamwekee jicho la bandia baada ya miezi sita tangu alipotoka hospitalini.
Tayari Baraka amefika mgodini na kutoa maombi mawili: Kupewa jicho la bandia na kusomeshwa shule. Hata hivyo uongozi wa mgodi umenukuliwa ukikubali kusaidia “ingawa si leo wala kesho.”
Matukio ya kupigwa, kujeruhiwa na kuuawa ni ya kawaida katika maeneo ya mgodi wa North Mara. Taarifa zinaonyesha kuwa tangu mgodi huo uchukuliwe na wageni mwaka 1995, watu 64 wameuawa na mamia wengine kujeruhiwa.
Aliyeuawa karibuni ni Mwita Ngoka, mkazi wa kijiji cha Kewanja. Alipigwa risasi na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) akidaiwa kuiba mawe yenye dhahabu.
Mratibu wa Sheria na Haki za Binadamu Tarime (Shehabita), Bonny Matto analalamikia uamuzi wa serikali kuruhusu askari kutumika kuua wananchi wake kwa kisingizio cha “kulinda mali ya mwekezaji.”
Anasema haelewi kwa nini serikali inaruhusu wenye migodi kuwa na “majeshi” yao wakati Ibara ya 147(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazuia kuwepo majeshi yoyote yale nchini isipokuwa ya serikali.
Naye Baraka amekumbwa na mkasa mwingine. Baada ya hospitali ya Bugando kumthibitishia, katikati ya Februari mwaka huu kuwa hali yake ilikuwa inatengemaa, alikwenda shuleni kuchukua na kujaza fomu ili aanze Kidato cha Kwanza.
Hapo ndipo alikatishwa tamaa. Aliambiwa alipe kwanza ada na michango mingine inayofikia Sh.160,000 ndipo aruhusiwe kuingia darasani. Baraka hana fedha wala mpango wa kuzipata.
Mikasa ya Baraka haikuanza jana. Mkasa wa kwanza ulikuwa kifo cha mama yake mzazi, Joyce Chacha. Alimwacha kichanga mikononi mwa baba yake, Nyamhanga Maita.
Kwa vile alikuwa anahitaji matunzo ya karibu, Maita alimwomba shemeji yake, Rahel Chacha amtunze mtoto huyo kwani hata kaka yake Maita Nyamhanga na dada yake Kurwa Nyamhanga (ameolewa sasa) walikuwa bado wadogo.
Kwa hiyo, Baraka akawa kwenye mikono salama ya mama yake mdogo. Lakini msiba ulimwandama tena. Tarehe 30 Novemba 2007, baba yake alifariki; akimwacha darasa la tano katika Shule ya Msingi Kenyange, kata ya Matongo.
Baraka alikumbwa na mkasa wa kupigwa risasi akiwa anaishi na mama yake mdogo lakini akichunga ng’ombe wa baba mkwe wa kaka yake, Maita.
Sasa Baraka hana wazazi. Ana ulemavu: Ni chongo. Amepoteza sura yake ya asili. Hawezi kwenda shule. Matarajio ya kupata elimu ya darasani yaweza kupotea kabisa.
Kwa Baraka, kama ilivyo kwa wananchi katika maeneo karibu na migodi, dhahabu imekuwa balaa.
Nyumba nyingi zilizo karibu na machimbo ya Nyabirama, ama zina nyufa au matundu – kutokana na risasi zinazorushwa ovyo kwa madai ya kufukuza wananchi.
Dirisha la nyumba ya Juma Marura, mwenyekiti wa kitongoji cha Mjini Kati lilipigwa na jiwe kutoka mgodini umbali wa mita 200 hivi na nondo ikapinda.
Aidha, karibu visima vya maji na mito, hasa mto Tighite, vimejaa maji ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu. Yamesheheni sumu itokanayo na kemikali zinazotumika kusafishia dhahabu mgodini.
Mwita Steven Waigama amelazimika kukarabati nyumba yake iliyobaki nyufa tupu. Nyufa zimetokana na mtikisiko unaofuatia milipuko ya baruti migodini.
Weirungu Matiku Marwa analalamikia wamiliki wa mgodi kwa kupora ekari 20 zilizoachwa na marehemu baba yake kwa ajili ya watoto 12.
“Eneo limechukuliwa na kampuni bila fidia. Sasa tunahangaika,” anaeleza Marwa.