ABDALLAH KIGODA: Mfumuko wa bei utaangamiza taifa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Dk. Abdallah Kigoda ameitaka serikali kupambana na mfumuko wa bei nchini kwa maelezo kuwa usipodhibitiwa kwa haraka, unaweza kuangamiza taifa.

Katika mahojiano na MwanaHALISI wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam, Dk. Kigoda alisema ni wajibu wa serikali kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi ipasavyo ili kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili wananchi.

“Hapa kwetu, mfumuko wa bei ni mkubwa kuliko ilivyo katika nchi ambako tunanunua bidhaa. Jambo hili lisipodhibitiwa kwa haraka, uchumi wa taifa utazidi kudorora,” ameeleza.

Dk. Kigoda ambaye kwa sasa, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge (Fedha, Uchumi na Mipango), amesema pato la taifa (GDP) limefikia wastani wa asilimia 67 kwa sababu ya kuporomoka kwa shilingi.

Amesema ili kuondokana na adha ya kuporomoka kwa uchumi, sharti serikali itimize kwa dhati nia yake ya kuboresha usafiri wa reli na barabara ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, hasa chakula kutoka kwenye maeneo ambayo yanazalisha kwa wingi kila mwaka.

Anasema kuporomoka kwa uchumi kumesababishwa na matatizo mengi, lakini kubwa likiwa ukosefu wa umeme wa uhakika, kuporomoka kwa uchumi duniani na kuchelewa kwa wahisani kuchangia bajeti kuu ya taifa katika miradi ya maendeleo.

Amesema, “Ndani ya kamati yetu, tumeiagiza serikali kuacha mara moja kukopa fedha kutoka mabenki binafsi kwa ajili ya uwekezaji. Tunataka serikali itumie fedha za kigeni kuwekeza kwenye maeneo yenye tija, hasa kilimo, nishati na miundombinu.”

Anasema ukopaji wa fedha unaofanywa na serikali kwenye mabenki binafsi, “hudhoofisha mwenendo wa fedha katika sekta za kiuchumi kutokana na wazalishaji wengi kukosa fedha za kuendeshea mitaji yao.”

Alipoulizwa iwapo kuna uwiano wowote kwenye mfumuko wa bei, kati Tanzania na nchi inazofanyanazo biashara, Dk. Kigoda alisema mfumuko wa bei uliopo nchini ni mkubwa ukilinganisha na nchi jirani za Kenya, Uganda na hata Brazil ambayo inaingiza kwa wingi bidhaa nchini.

“Hapa utaona tunaingiza mfumuko wa bei, badala ya kuupunguza. Katika eneo hili, ni muhimu hatua za kisera zikachukuliwa haraka hasa katika maeneo ya uzalishaji na utunzaji wa fedha za kigeni ndani ya BoT,” amesisitiza.

Hata hivyo, Dk. Kigoda anasema serikali tayari imeanza kuchukua hatua ya kukabiliana na tatizo hilo; tayari imeanza kuwekeza fedha kwenye miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa reli, barabara na miradi mikubwa ya umeme.

Anasema kwa bahati mbaya, uwezo wa taifa kuzalisha bidhaa zake ni mdogo kuliko uingizaji wa bidhaa kutoka nje.

Alipoulizwa ni hatua gani zichukuliwe kuondokana na uzalishaji mdogo, Dk. Kigoda alikuwa na mawili:

Kwanza, kuhakikisha ziada ya chakula iliyopo kwenye maeneo yenye chakula kingi, inapelekwa kwenye maeneo yenye upungufu.

Pili, anasema taarifa zilizopo zinaonyesha serikali inakusanya fedha nyingi zaidi kuliko wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa.

Lakini anasema wingi wa fedha hizo hauonekani kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na baadhi ya matumizi ya hovyo serikalini.

Anasema mara kadhaa kamati yake imekuwa ikiishauri serikali kuachana na matumizi ya anasa ikiwamo ununuzi wa magari ya kifahari. Imekuwa ikishauri pia upunguzaji ukubwa wa serikali na kudhibiti mapato yake.

Kuhusu kukosekana kwa umeme wa uhakika, Dk. Kigoda anasema ni vema serikali ikaharakisha mkakati wa kuingiza nchini majenereta ya kuzalisha umeme wa dharula ili kukabiliana na tatizo hilo.

Dk. Kigoda ambaye ni mbunge wa Handeni (CCM), mkoani Tanga anasema, “Hakuna nchi ambayo inaweza kufanikiwa kwenye uchumi, bila kuwa na umeme wa uhakika. Kama nasi tunataka kuondoka na utegemezi, sharti kwanza tuwekeze kwenye umeme.”

Alipoulizwa ni jambo gani ambalo limemfurahisha katika kukabiliana na upungufu mkubwa wa nishati, Dk. Kigoda alisema kilichomfurahisha ni uamuzi wa Benki Kuu ya taifa (BoT) kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei kwa kupandisha riba ili kupunguza mikopo holela kwenye mabenki binafsi.

Anasema, “BoT imeweka utaratibu kwa benki nyingine kuchangia kwenye akiba za fedha za kigeni. Hili litasaidia kuongezeka kwa reserve (akiba) ya fedha za kigeni nchini.”

Anasema, “Katika hili la mfumuko wa bei, wapo wengine wanaoweka fedha za kigeni ili kutafuta faida. Nashauri watumie fedha za ndani kwa matumizi yetu ya ndani.”

Akizungumzia matatizo yaliyopo katika jimbo lake la Handeni, Dk. Kigoda anasema moja ya matatizo makubwa yanayowakabili wananchi wake, ni kukosekana kwa maji safi na salama kwa matumizi yao na mifugo.

Anasema wilaya ya Handeni inayochukua asilimia 30 ya mkoa wa Tanga, ina mradi mmoja mkubwa wa maji uliojengwa mwaka miaka 20 iliyopita. Anasema gharama za kuukarabati sasa zimefikia Sh. 120 bilioni.

“Wakati mradi huu ulipokuwa unafanyiwa uhakiki, ulikuwa uhudumie watu 100,000; leo hii mradi huu unahudumia watu 200, 000, huku mashine, pampu, mabomba – vyote vikiwa vimechakaa,” anasimulia Dk. Kigoda kwa sauti ya uchungu.

Anasema, “Sasa tunatafuta fedha ili kuuboresha. Lakini wakati hilo likiwa linasubiri fedha kutoka serikalini na pengine kwa wahisani, tumeamua kuwekeza katika uchimbaji wa mabawa, visima virefu na vifupi.”

Anasema tayari wameanza mradi wa kuchimba visima virefu kupitia kwa kutumia msaada uliotolewa na mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Mustaph Sabodo; ambapo visima 25 vitachimbwa katika awamu ya awali ya mradi.

Lengo la Dk. Kigoda ni kuchimba angalau kila kisima kimoja kwa kila kata ya jimbo lake.

Anasema mbali na miradi hiyo miwili, halmashauri ya wilaya ya Handeni, imepanga kutumia vyanzo vya maji vilivyopo eneo la Kilumbi, pembeni mwa barabara ya Chalinze-Segera.

Anasema iwapo watafanikiwa kuyavuna maji hayo na kuyapeleka kwenye vijiji vya Mkata, Mmanya, Komkonga na Kabuku, anaamini kwa kiasi kikubwa tatizo hilo linaweza kupungua sana au kuisha kabisa.

Anasema kila diwani katika halmashauri yake amepewa jukumu la kusimamia uchimbaji angalau wa kisima kimoja ili kukabiliana na uhaba wa maji.

Kwa upande wa elimu, anasema jimbo lake lina sekondari zaidi ya 30; mbili zikiwa za Kidato cha V na VI – Handeni High School na Chogoa High School. Aidha, kuna vyuo viwili vya useremala vya Chanika na Handeni. Anasema mipango iko mbioni kuanzisha chuo kingine huko Nkata.

Kuhusu zahanati, Dk. Kigoda anasema anamshukuru Mungu, kwamba vijiji vingi vina zahanati; sasa mipango iko mbioni kuanzisha kituo cha afya Kabuku kwa Mgwe.

0
No votes yet