Acha 'viguu na njia' watangetange
MTOTO anayependa kulala kila mahali; mara leo kwa shangazi, kesho kwa mjomba, keshokutwa kwa dada, mara nyingi huitwa na mzazi wake kuwa ni "kiguu na njia".
Ndivyo walivyo wanasiasa wanaohama vyama kila kukicha. Huwa wanadhihirisha sura zao halisi kisiasa. Hawa nao ni kiguu na njia wa kisiasa.
Lakini tabia ni kama ngozi ya mwili, haibadiliki isipokuwa mtu mwenyewe abadilike kifikra kama alivyosema Mrisho Mpoto, msanii maarufu nchini wa kughani mashairi.
Wanasiasa wameingia katika wakati wa kwenda huku na kule, lengo likiwa ni kutafuta madaraka ya haraka ili kutimiza haja zao. Mwaka 2010 unafanyika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani kwa upande wa Tanzania Bara.
Wa visiwani Zanzibar nao watachagua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wabunge. Pia watachagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani.
Sasa ni wakati wa wanasiasa na wanagenzi katika siasa, kutafuta vyeo, sifa na umaarufu kwa wanachama na wananchi watakaokuja kupiga kura.
Tutashuhudia watu wakiacha midomo wazi na kushangaa kwa kuona watu waliowashawishi kujiunga na vyama vyao wakiwasaliti na kubaki hawana la kufanya bali kushikilia vyama visivyo na mihimili tena.
Baadhi ya watendaji wa vyama watawatangaza na kuwanadi maadui zao wa jana kuwa ni mashujaa wao wapya na kuwaacha wanachama wao bila ya kuwathamini. Huku ni kutupa kinyemi baada ya kupata kipya. Ni mwaka wa mavuno kwa baadhi ya watu.
Lakini huu si msimu wa kushangaa kwa wanachama na viongozi wanaojua nini kinachoendelea, bali ni wakati wa kuendelea na mambo ya msingi yanayoweza kujenga chama.
Viongozi hao wanajua kuwa huu pia ni wakati wa kuvuna wanachama wanaotumwa kuvuruga baadhi ya vyama vinavyoonyesha ushindani ndani ya vyama vyenye nguvu. Wengine, baada ya kumaliza kazi ya kuvuruga vyama, sasa wanarudi kwenye vyama vyao vilivyowatuma kazi hiyo waliyoifanya kwa mafanikio.
Huu ndio wakati wa kunyanyasika kwa wagombea wenye kutumia malikauli. Watachafuliwa kwenye vyombo vya habari na wengine tutashuhudia wakimwaga jasho, damu na machozi kwa sababu ya kutaka kushindana na mabedui wasio na huruma.
Pia huu ndio wakati mtu akitaka ubaya aguse ulaji wa viguu na njia hao. Kwa wale wanaodhani ni mwisho wa kina David Kafulila, Augustine Mrema, Tambwe Hiza, Wilfred Rwakatare na Walid Kabourou, kuhama vyama wamenoa. Watu hao bado hawajafika bali wamepumzika tu kwa kuwa sasa wanatimiziwa mahitaji yao.
Wanaohama vyama wamelenga kuingia katika uchaguzi ndio maana baadhi yao walipohama tu wakatangazwa tayari ni wagombea majimbo fulani.
Wengine walipohama haikuchukua muda wakapewa vyeo vya juu na kutembea na watendaji wa vyama ili “kujenga imani” kwa wananchi.
Sasa ni wakati wa kumuuliza kila anayehama chama kilichompatia umaarufu alionao; chama alichopitia akajulikana aeleze nini kilichomhamisha hadi kuomba kura kwa chama kipya?
Ndio ninaposema Watanzania wawaache “viguu na njia” watangetange. Ukweli ni kwamba hawana jipya muda wote.