Afa ya rais ni uchumi, isifanyiwe mzaha


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Tafakuri

NIMEJARIBU kujizuia kujadili tukio la kuanguka kwa Rais Jakaya Kikwete viwanja vya Jangwani Jumamosi iliyopita, nimeshindwa.

Si kwa sababu ninashabikia hali iliyomtokea Rais, ila ninaumwa ndani ya nafsi yangu kwamba tukio hili linafanyiwa mzaha mkubwa!

Nina uchungu wa kweli moyoni. Ninasumbuliwa na kitu kimoja tu, usiri wa kijinga kabisa katika mambo mazito na ya kitaifa.

Afya ya rais wa taifa lolote, kubwa au dogo, inaweza kuleta athari kubwa sana za kiuchumi. Kuna wawekezaji wanawekeza katika nchi kwa sababu ya imani yao kwa kiongozi mkuu wa dola, wanatambua kwamba sera zake zitawasababishia wanawiri kiuchumi.

Nieleweni vema. Hapa sizungumzii kushamiri kwa njia za magendo, la hasha. Katika njia za wazi na zinazokubalika.

Kwa mafano, 15 Machi 2010, Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) liliripoti kuwa soko la hisa la Misri lilianguka kutokana na “sintafahamu” ya afya ya rais Hosni Mubarak ambaye alikuwa amefanyiwa upasuaji nchini Ujerumani kwa takribani wiki moja.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81 alikuwa hajaonekana hadharani kwa zaidi ya wiki moja na hivyo wawekezaji wakaanza kuingiwa hofu wakijiuliza itakuaje hatima ya fedha zao.

Taarifa zilisema, “mawasiliano mabaya” kuhusu afya ya rais yalisababisha hofu miongoni mwa jamii.

Inawezekana wapo watu ambao hawatanielewa kwa sababu wanaamini mno katika usiri na kufunika kila kitu hata kama kwa kufanya hivyo, si rais wala taifa linapata faida.

Katika dunia tunayoishi, kila mtawala hata kama anatokana na chama hichohicho, au hata kama ni mtoto anaingia madarakani badala ya baba yake, kamwe hawezi kuwa sawa juu ya njia na mikakati ya kufikia maendeleo tarajiwa.

Ndiyo maana ukitazama staili ya rais mstaafu Benjamin Mkapa hata kama anatokana na chama hichohicho cha Rais Kikwete, haraka utagundua kwamba hawa ni watu wawili tofauti katika kuendesha nchi.

Ni kweli wanatokana na chama kimoja. Walitumia utaratibu mmoja wa kuingia madarakani, lakini wanatofautiana sana juu ya mbinu za kufikia malengo tarajiwa.

Ndiyo maana wawekezaji pamoja na sera nzuri, na ahadi nzuri za kuwataka wawekeze kwenye nchi fulani, imani yao inajengwa zaidi kwa kuangalia ni kiongozi gani aliye juu kabisa kama mlinzi wa sera hizo?

Je, anasimamia kile anachoamini? Je, kuwepo kwa kiongozi huyo kutawahakikishia kurejesha faida kutokana na fedha walizowekeza?

Ndiyo maana kwa mfano, baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967 nchini Tanzania na utekelezaji wake kama kutaifisha majumba mwanzoni mwa miaka ya sabini, iliichukua nchi yetu takribani miaka 35 kwa wawekezaji wa maana kuamua kuwekeza katika sekta ya umma.

Hata Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, aliposema sasa kila kitu ruksa, bado wapo waliosita kutia fedha zao kwenye sekta ya ujenzi. Wengi walikuwa na hofu.

Imani ilikuja kujengeka kwa kina zaidi wakati wa serikali ya awamu ya tatu, baada ya kuamini kweli Mwalimu Julius Nyerere hana tena nafasi ya kubuni sera za kiuchumi za Tanzania.

Kwa hali hii, inapotokea Rais anapata matatizo ya kiafya, tena yanayotokea hadharani kama ya kuanguka mara tatu, inakuwa vigumu mno umma kusadiki maelezo mepesi kama haya ya “kufunga ramadhani, kuishiwa sukari, uchovu.”

Wasaidizi wa rais ni lazima wajue wazi kwamba urais si mtu, ni taasisi, tena iliyojengwa juu ya mkataba wa wananchi – Katiba.

Kitendo chochote cha kujaribu kufanya afya ya rais kuwa ni siri, ni sawa na kutaka kuufanya urais kuwa ni jambo la siri. Haiwezekani, haikubaliki na hakika haitakubalika.

Lazima wasaidizi wa rais wafahamu kuwa Dk. Jakaya Kikwete ni rais wa Tanzania, amechaguliwa tena kwa kura nyingi mwaka 2005.

Ni kiongozi wetu sote Watanzania, wenye vyama na wasiokuwa na vyama – anaheshimiwa hivyo, ndiyo maana hata pale anapofanya maamuzi mengine mepesi kama kuwapa nyadhifa watu wepesi, bado watu wanaheshimu na kuvumilia kwa sababu yeye ni kiongozi wa taifa.

Binafsi nilipata kuingia katika mgogoro na Wakenya wakati fulani waliokuwa wanahoji safari za mara kwa mara za rais wetu. Haraka niliwajibu kwamba rais Mwai Kibaki hana nguvu za mwili za kusafiri kama rais wetu.

Lakini zaidi niliwaambia, Kikwete hana hofu ya kumfanya asitoke nje ya nchi kwa sababu urais wake hauna mgogoro na yeyote. Mjadala ukaisha!

Kwamba Kikwete ni rais wa Watanzania wote hakuna ubishi. Wenye vyama na wasiokuwa navyo, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo, waumini wa dini na wapagani, kila anayeishi na kukaa katika ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata Zanzibar pamoja na kiburi chao cha kuchomeka kinachoitwa “nchi kamili ndani ya Muungano” katika mabadiliko yao ya 10 ya Katiba, Kikwete ni rais wao pia.

Sasa kwa kuwa huo ndio ukweli, tungependa sasa kuona wasaidizi wa Rais Kikwete wakifanya kazi waliyoajiriwa kuifanya. Washauri vizuri, kwamba haiingii akilini kiongozi wetu kuanguka mara tatu hadharani na umma upewe maelezo mepesi kama wanayoyatoa.

Wasaidizi hawa kama hawawezi kumweka kitako rais na kumwambia kwamba sasa zinatakiwa hatua kubwa, chungu na nzito kukabili shida inayomsumbua, basi waache kazi wanayofanya.

Ninasema tena, afya ya Rais ni uchumi wa nchi, tuache mzaha. Umma unataka hatua na maelezo ya kisayansi yaliyojengwa juu ya msingi unaoitwa ukweli, si kusokota habari.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: