Afrika na utawala usiothamini haki


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

SASA ni zaidi ya nusu karne tangu mwaka 1960 uitwe mwaka wa Afrika. Katika kipindi hiki chote Afrika imeshuhudia ustawi wa kujivunia lakini pia imelia na kusaga meno kutokana na udhalimu na maangamizi makubwa dhidi ya watu wake.

Afrika imepata bahati ya kuongozwa na viongozi wema na waadilifu kama Julius Nyerere, Kwame Nkrumah wa Ghana na Kenneth Kahunda wa Zambia.

Lakini pia Afrika imeshuhudia mateso kupitia mikono ya madikteta na mafisadi kama Mobutu Sese Seko wa iliyokuwa Zaire (DRC), Sani Abacha wa Nigeria, na sasa wapo kina Omar Al Bashir wa Sudan na wengine wengi.

Miaka zaidi ya hamsini baada ya uhuru kutoka ukoloni mkongwe, Afrika inashuhudia mambo yaliyowasukuma wanamapinduzi kudai uhuru ambayo ni ukoloni wa mfumo wa uliberali mamboleo, dhuluma, unyonyaji, udini, ukabila na ubaguzi wa rangi na kila aina ya uovu.

Baya zaidi ni kwamba hata serikali zilizochaguliwa kidemokrasia zina sura ya kidikteta; zinanuka rushwa na ufisadi; zinatumia mabavu na ukiukwaji sheria na pia zinadhibiti haki, zinaonea na kunyonya raia.

Mfano ni jambo la kawaida kukuta serikali inambana mjasiriamali mdogo alipe kodi zaidi ya “mwekezaji” anayemiliki hoteli ya kimataifa au mgodi wa dhahabu. Matokeo yake ni kuongezeka kwa umaskini, ujinga na magonjwa ingawa takwimu zinaonyesha uchumi kukua na kupongezwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Kwa Waafrika wengi tumaini la kuiona Afrika yenye neema ya asali na maziwa limetoweka. Njaa ni wimbo wa kila uchao. Hii ndiyo hali halisi ya Afrika ambayo viongozi waliochaguliwa kwa kura za wananchi ili wawatumikie wamegeuka kuwa watawala dhalimu, katili wasio na chembe ya utu ingawa wanapenda sana kusifiwa mithili ya Farao.

Sababu kubwa inayoifanya Afrika iendelee kutawaliwa na madhalimu ni dhana ya “Utawala bora” usiozingatia haki, usawa, utu na ustawi na umeaua uaminifu, uadilifu, uongozi bora, uwajibikaji na maendeleo ya watu.

Matokeo yake Afrika inaendelea kutawaliwa na watu wasio waadilifu wasiowajibika kwa umma na wanaoutumia dhana ya utawala bora kuiba mali za umma. Hii ni kinyume kabisa na ajenda kuu ya Afrika wakati wa harakati za ukombozi ambayo ilikuwa kuleta uhuru na kuunda serikali zinazongozwa kwa sheria zinazoheshimu haki, usawa; kuthamini utu na ustawi wa watu na uongozi bora.

Historia inaonyesha wazi kwamba serikali za Kiafrika zilifanikiwa sana katika kuunda mfumo unaoendeshwa kwa misingi ya utawala wa sheria. Lakini hazikuthubutu kwenda umbali wa kutunga sheria na kuunda mfumo wenye taasisi imara zinazosimamia kwa dhati haki, usawa, utu na ustawi.

Serikali nyingi za Kiafrika zilikuwa na mihimili mitatu ‘hewa’ ya dola iliyofanya kazi kwa mujibu wa sheria kandamizaji na kujigamba kuwa zinazingatia utawala wa sheria.

Baada ya kuingia kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi dhana ya utawala bora kutoka Benki ya Dunia ikawa chambo cha watawala kujisifia kwa wakubwa wa Magharibi kwamba wanatekeleza utawala bora  kisheria. Lakini Afrika inazidi kudorora chini ya utawala bora usiothamini haki za watu, usawa wao, utu wao na ustawi wao.

Tufahamu kwamba utawala bora hauna maana ya utawala wa sheria zinazolinda haki ya umma. Pili hauna maana kuwa ni uongozi bora unaoendesha serikali kiadilifu.

Pia tufahamu kuwa mtawala si kiongozi na kwamba mtawala hana sifa ya ubora. Mfano hatuwezi kusema uongozi wa wakoloni au makaburu. Kwa sifa ipi nzuri aliyonayo mkoloni mpaka tumuite kiongozi? Tunasema utawala wa wakoloni.

Serikali inaweza kuendeshwa na ama watawala au viongozi na utendaji wao ukawa tofauti kabisa ingawa wote wanatumia sheria.

Tofauti baina yao ni kwamba watawala hutumia mabavu, hufanya dhuluma na kuonea watu ilhali viongozi hutumia hekima, uaminifu na uadilifu wakijiona wao ni watumishi na si mabwana wakubwa “waogopwa na waheshimiwa.” Afrika imejaa mifano mingi ya nchi zinazoongozwa na dhana hii ya utawala bora lakini usio wa haki.

Mfano aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo kwa kutumia dhana hii ya utawala bora alisema yeye alikuwa rais kisheria baada ya uchaguzi mwaka 2010 lakini hakuwa rais wa haki.

Kisheria Katiba ya Ivory Coast ilimpa ushindi na kuhalalisha utawala wake. Alifanya dhuluma kupitia upenyo wa utawala bora wa sheria. Utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini nao pia ulikuwa utawala bora kisheria kwa mujibu wa sheria za Afrika Kusini zilizotungwa na bunge na kutekelezwa na mahakama.

Wabunge walipigiwa kura wapigakura walijiandikisha kisheria. Utawala huu ulitambuliwa kimataifa. Lakini utawala wa makaburu haukuwa wa haki ingawa serikali yake iliundwa kisheria.

Utawala bora wa kisheria usiozingatia haki umeigawa Afrika katika matabaka ya mabwana na watwana. Watawala wamekuwa mafisadi jeuri na fedhuli waliojaa matusi na kejeli kwa wananchi ambao ndio wanawapa nafasi hizo walizonazo.

Kote duniani haki, usawa na utu vikishatoweka basi tumaini hutoweka na watu hukata tamaa na kutafuta njia kuuondoa utawala bora wenye dhuluma.

Wengine hufanya mapinduzi na kuirejesha serikali kwa umma kama Mali. Wengine huandamana kama ilivyokuwa Tunisia na Misri. Wengine hutumia vyama vya siasa kuwaondoa watawala kama ilivyokuwa kwa Thabo Mbeki Afrika Kusini. Wengine hutumia nguvu ya hoja na kushinda kama Tanzania.

La kusikitisha sana watawala hawazisomi alama za nyakati na kujisahihisha na kuwa viongozi. Wanashikilia uzi ule ule. Kwa jeuri na ufidhuli huu nchi nyingi za Kiafrika zitaingia katika vita na umwagaji damu.

Watawala watakimbia nchi wakiacha watu wanachinjana. Kama wanajua kuwa hii ndiyo hatima basi kwa nini wanaendeleza utawala wa dhuluma, unyonyaji, mauaji, rushwa na ufisadi?

Afrika itaweza kustawi iwapo itajenga mifumo imara wa kisheria na kimaadili inayoheshimu haki, utu na usawa ambayo italeta tumaini, upendo, umoja, amani na ustawi kwa watu wake. Mifumo hii itawawazesha wananchi kuwawajibisha viongozi wanaojigeuza kuwa watawala maana wanakuwa wamevunja agano.

Na mwenye kuvunja ahadi ni mnafiki. Wale waliopewa dhamana ya uongozi na wananchi ya kuwawakilisha wanao wajibu mkubwa wa kuhuisha dhana ya uongozi bora ili kurejesha uadilifu na uaminifu katika uongozi ambao utasimamia kwa haki kukua kwa demokrasia, uchumi na maendeleo ya watu wa Afrika.

Viongozi hawa wasimamie na kutetea maslahi na haki ya wananchi kwani wamechaguliwa kuifanya kazi hii na si kugeuka kuwa watawala. Kubwa zaidi wananchi wawanyime kura watawala mafisadi.

Huu ndio ukombozi mpya kwa Afrika kutoka kwa watawala wake. Ole wao wanaoendelea kuukumbatia utawala uliojaa dhuluma, ufisadi na uonevu.

+447404486150
0
No votes yet