Ahadi, porojo katika suala la umeme


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 13 July 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

HISTORIA ya kero ya umeme nchini inaonyesha mgawo wa kwanza mkubwa ulitokea mwaka 1992. Mvua hazikutosha kwa hivyo nchi ikawa na ukame kwa kuwa kina cha maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme kilipungua.

Ukafanyika mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu mazingira jijini Rio de Janeiro, Brazil. Tanzania iliwakilishwa na ujumbe wa watu 40. Hapo Reo, yalijadiliwa kile kiitwacho “mabadiliko ya tabia.”

Kadhia hii ya ukame kuathiri kiwango cha maji kwenye mabwawa, ikatumiwa na viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kubuni “miradi hewa” ya umeme.

Kwa kuwa dhamira ya kubuni miradi ilikuwa kunyonya uchumi kwa maslahi binafsi, ikaja miradi ya kifisadi kwa kisingizio cha kupata nishati ya kutumia kuleta maendeleo ya uchumi.

Serikali ikaanzisha mradi wa umeme wa muda mfupi eneo la Ubungo na mwaka 1994 ikaingia mkataba na kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) unaoisumbua hadi leo.

Mwaka 2000 na 2001 miradi ya Songas na Kihansi ilikamilika. Mwaka 1980 Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC) liligundua gesi Kilwa Kisiwani, mkoani Lindi.

Uchimbaji wake ulipoanza pamoja na usafirishaji ndio uliwezesha kujengwa mitambo ya kuzalisha umeme wa gesi jijini Dar es Salaam mwaka 2001. Uendeshaji unafanywa na kampuni ya SonGas ya Canada kupitia kampuni ya Pan African Energy Tanzania. Lakini hakuna mabadiliko.

Mradi mwingine wa muda mrefu ni  ujenzi wa bwawa la Kihansi mwaka 1995 ambalo lilikamilika kujengwa mwaka 2000. Bwawa la Kihansi linazalisha megawati 180.

Badala ya kutafuta miradi ya uhakika kwa kulisaidia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kupata fedha za kutosha kutoka kwa wadaiwa wake sugu, serikali ikaamua kukodi menejimenti ya kuendesha shirika hili. Ndipo mwaka 2002 wakaingia Net Group Solution, kampuni kutoka Afrika Kusini.

Umma haukupenda hatua hii baada ya menejimenti ya TANESCO pamoja na wafanyakazi kutoridhika na mkataba wa miaka minne na wageni. Serikali ya Benjamin Mkapa ikashikilia mpini.

Ikaaamuru polisi waliovaa silaha za kila aina, yakiwemo mabomu ya machozi na risasi za moto, kusindikiza maofisa wa Net Group hadi ndani ya makao makuu ya TANESCO.

Wakurugenzi wa kampuni hiyo walikuwa wanalipwa mishahara mikubwa ya hadi Sh. 25 milioni (mkurugenzi mkuu), Sh. 23 milioni (mkurugenzi wa fedha) na Sh. 22 milioni (mkurugenzi wa utumishi).

Kweli, miaka minne baadaye, Desemba 2006, Net Group walipofunga virango wakaiacha TANESCO hoi. Haina mapato ya maana, hakuna uwekezaji uliofanywa, wala hakuna vitendea kazi vilivyonunuliwa. Kilivhopatikana ni mavuno kwa wageni. Basi!

Serikali haikujifunza. Ikaleta mradi wa kutengeneza mvua kutoka nchini Thailand. Wananchi walikataa miujiza hiyo. Wakaingiza kampuni hewa ya Richmond Development (LLC) ambayo haikuwa na fedha wala ujuzi wa kufanya kazi iliyoomba.

Ili kuzima kelele za wananchi, vyombo vya habari na baadhi ya wabunge wa upinzani, haraka mkataba ukarithishwa kwa Dowans Costa Rica SA, kampuni nyingine ya mashaka.

Halafu serikali ikalazimisha TANESCO kuingia mkataba na kampuni ya Aggrekko ya Scotland wa kuzalisha umeme megawati 40. Kampuni hiyo ilifungasha virago baada ya kukorofishana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu masuala ya kodi.

Shida haina adabu. Tayari Aggrekko wamerejeshwa nchini ili iweze kuzalisha megawati 100 za umeme. Nayo Dowans iliyokuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu, serikali ikaridhia kununua umeme wake kupitia kinachoitwa, “kampuni ya Symbion Power ya Marekani.” Lakini Symbioni yenye uwezo wa kuzalisha megawati 120, inaweza kuzalisha megawati 60 tu.

Hivyo, tangu mwaka 1992, serikali haijapata ufumbuzi wa tatizo la uhaba wa umeme zaidi ya kutumbukia katika kashfa za ufisadi. Mwaka 2003 ilianzisha wimbo wa kutengeneza miradi ya Mchuchuma na Kiwira, lakini zimebaki porojo tupu.

Porojo hizo zimeanza kupamba moto tangu Rais Jakaya Kikwete alipomteua mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kuwa waziri wa nishati na madini mwaka 2008. Akizungumza bungeni, Julai 2008, Ngeleja alisema, “Tatizo la umeme litakuwa historia.”

Kauli yake iliungwa mkono na Aloyce Massanja, kaimu mkurugenzi wa miradi ya Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Mto Rufiji (Rubada), 29 Desemba 2009 pale aliposema, “Tatizo la umeme nchini litasahaulika ifikapo 2012.”

Aliahidi kukamilika mradi wa Stiegler’s Gorge wa Rufiji wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,100 za umeme. Kiasi cha juu cha uzalishaji ni megawati 2,750.

Tarehe 24 Desemba 2010 Ngeleja akasema mgawo wa umeme utakuwa historia ifikapo 2013. Alikuwa akikagua mradi wa kuzalisha gesi wa Songosongo, Kilwa Kisiwani. Alijitapa katika miaka mitatu ijayo, kutakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 900 katika vyanzo mbalimbali.

Tarehe 15 Februari 2011, Ngeleja akisoma taarifa ya serikali kuhusu mwisho wa tatizo la umeme nchini, alionyesha ufumbuzi uko mbali mno. Alisema serikali inahitaji Sh. 300 bilioni kukamilisha miradi ya muda mfupi na mrefu kufikia mwaka 2033.

Aidha, alibainisha uwezo halisi wa mitambo yote ya kuzalisha umeme katika gridi ya taifa kuwa ni megawati 1,006 ambapo mitambo ya maji ina uwezo wa megawati 561 na mitambo ya gesi asili na mafuta mazito ina uwezo wa kutoa megawati 445.

Tarehe 26 Machi 2011 akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kabita wilayani Magu mkoa wa Mwanza, Makamu wa rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal akaongeza kibwagizo kwa kusema kero ya umeme inamalizika mwaka 2015.

Tarehe 25 Mei 2011, Ngeleja anampiga vijembe Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba. Alisema watu wanapita mitaani kudai yeye ni mzigo. Ngeleja alikuwa akimjibu Makamba aliyedai waziri huyo ni mzigo.

Makamba alifikia hatua hiyo baada ya kumuona Ngeleja amedanganya pale aliposema serikali imedhamiria kukodi mitambo ya kufua umeme wa megawati 260 kabla ya Julai 2011. Akasema serikali imedhamiria kununua mtambo wake mpya mwaka huu wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150. Mpaka sasa mtambo huo haujanunuliwa.

Hadithi ni ndefu. 27 Juni 2011 Ngeleja akaibuka na kusema, “umeme ni janga la taifa.” Ametaka wananchi wavumilie. Alikuwa akizungumza katika semina ya wabunge mjini Dodoma.

Baadaye 3 Julai 2011 Ngeleja taarifa zikavuja; maofisa katika wizara yake wamehonga baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya nishati na madini ili kupitisha bajeti ya wizara yake.

Je, tatizo ni nini? Serikali haijawekeza katika eneo hili. Mabwawa ya maji yana uwezo wa kuzalisha megawati 773, lakini sasa yanazalisha umeme usiozidi megawati 400. Mitambo inayotumia gesi ina uwezo wa kuzalisha megawati 225.

Kutokana na uchakavu wa mitambo ya kusafirisha na kuzalisha gesi kutoka Songosongo, mitambo ya umeme ya Songas yenye uwezo wa kuzalisha megawati 180, sasa inazalisha nusu ya megawati. Ni  kati ya megawati 80-100.

Tegeta wenye uwezo wa kuzalisha megawati 45, sasa unazalisha megawati 25, Symbion wenye uwezo wa kuazalisha megawati 100, sasa unazalisha megawati 60.

Mitambo ya IPTL ina uwezo wa kuzalisha 100, lakini inazalisha chini ya megawati 50. Nani alaumiwe?

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet