Ahadi za Rais Kikwete hazijatekelezwa


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 04 January 2012

Printer-friendly versionSend to friend
Ndani ya Jamii

NI vema wananchi wamemaliza mwaka 2011 na kuanza mwaka mpya wa 2012. Hata hivyo, ukweli utabaki palepale; wengi wao hawatasahau kauli tata na ahadi mithili ya Abunuwasi zilizotolewa na Rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete.

Miongoni mwa kauli hizo, ni pamoja na ile ya “nitaboresha maslahi ya walimu, sifahamu kwa nini taifa langu ni masikini, siwajui Dowans, uchumi unapaa na watoto wa shule mnapata mimba kwa sababu ya viherehere vyenu.

Akiwa nchini Marekani, Rais Kikwete alinukuliwa akisema kuwa hafahamu kwanini nchi yake ni maskini wakati ina utajiri wa kutupwa. Alikuwa akizungumza na baadhi ya Watanzania wanaoishi Marekani.

Akihutubia taifa Aprili 2011, Rais alisema serikali yake imetenga kiasi cha Sh. 60 bilioni za kujengea nyumba za walimu kila mwaka ili kuondoa tatizo hilo nchini.

Aliahidi kulipa malimbikizo yote ya walimu kabla ya Julai; kila shule itapata walimu watano na maabara. Ahadi hiyo haijatekelezwa.

Badala yake serikali imetoa waraka wa kupunguza ajira kwa asilimia 50, kupunguza upandishaji vyeo watumishi wake kwa kiwango hichohicho. Waraka huo ulitoka Novemba 2011.

Rais Kikwete alisema pia mazungumzo na Benki ya Dunia (WB) tayari yamefanyika kwa ajili ya serikali kupata mkopo wa vitabu na ujenzi wa maabara hizo.

Lakini karibu shule zote nchini hazina vitabu. Hazina madawati. Hazina walimu. Hata wale walimu wachache waliopo, wako njiani kugoma kutokana na kunyimwa stahiki zao.

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kinasema baada ya kufanyika uhakiki kati yake na serikali, deni la walimu lililothibitika la mishahara na marupurupu hadi 31 Desemba 2011, lilikuwa Sh. 53 bilioni.

Kuhusu ujenzi wa barabara, Rais Kikwete akiwa wilayani Kilwa alisema barabara ya Mingoyo hadi Nangurukuru imekamilika; kipande cha Somanga hadi Ndundu kiko mbioni kuwekwa lami. Lakini hadi 31 Desemba 2011, ujenzi wa barabara hiyo ulikuwa haujakamilika.

Hakuishia hapo. Rais aliendelea kuhubiri mradi wake huo wa ujenzi wa barabara za juu jijini Dar es Salaam.

Lakini alipotembelea Wizara ya Ujenzi, 21 Machi 2011, Rais Kikwete alizuia mpango wa upanuzi wa barabara ya Morogoro ambayo awali alisema ni miongoni mwa zile zitakazotumika katika kutekeleza mradi wa barabara za juu.

Katika mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete aliendelea kuhubiri kile alichoita, “Maisha bora kwa kila Mtanzania.” Aliendelea kusema maisha hayo yatapatikana kwa “Ari mpya zaidi, nguvu mpya zaidi na kasi mpya zaidi.”

Hata hivyo, kila siku zilivyozidi kuyoyoma, ndivyo maisha bora yalivyogeuka “maisha magumu kwa kila Mtanzania.”

Leo hii, umeme umepanda bei, lakini haupo. Mafuta ya taa ambayo ndiyo kimbilio la wanyonge katika matumizi ya nishati, hayakamatiki tena. Serikali baada ya kupambana na walanguzi na wachakachuaji wa mafuta, imeamua kupandisha bei ya nishati hiyo.

Kwenye zahanati na hospitali za serikali, hakuna dawa na kuna msongamano mkubwa wa wagonjwa. Kitanda cha kulala mgonjwa mmoja kinatumika kwa wagonjwa watatu. Ajabu hata kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wagonjwa wamesongamana. Kila mwenye mgonjwa anakimbilia Muhimbili maana hospitali za wilaya na mikoa hazina dawa, vifaa vya kisasa na madaktari wenye motisha.

Akihutubia kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa CCM, tarehe 5 Februari 2011, mjini Dodoma, Rais Kikwete alikana kufahamu wamiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Dowans Holdings (DHSA) na Dowans Tanzania Limited (DTL).

“Siwajui wala sijakutana na wamiliki wa makampuni ya Dowans Tanzania Ltd na Dowans Holdings SA,” alisema akijaribu kujitoa mikononi mwao.

Lakini Edward Lowassa, aliyeshinikizwa kujiuzulu na bunge lilipojadili ripoti ya uchunguzi wa sakata la mkataba wa Richmond waliourithi Dowans, alipotoka hadharani na kusema Rais Kikwete anawafahamu wahusika waliongiza nchi kwenye mkataba tata wa Richmond/Dowans; hakuweza tena kujitosa kukana madai hayo. Hii ina maana amekubaliana na kilichosemwa na kilichoelezwa vikaoni mwa chama chake.

Akihutubia mkutano wa NEC mjini Dodoma, 26 Novemba 2011, Lowassa alisema, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo wewe Rais Kikwete hukulifahamu au hukunituma” kuhusu Richmond/Dowans.

Alisema, “…Mwenyekiti, natukanwa kwa ufisadi wa Richmond wakati wewe unafahamu kilichosababisha kashfa ya Richmond ni makosa ya watendaji walio chini yangu? Sasa kosa langu ni lipi? Ni kule kukubali kuwajibika kwa ajili ya serikali yangu na chama chetu? Kwa nini nihukumiwe kwa kosa hilo?”

Huku akimtolea macho Kikwete alisema, “Unakumbuka vema jinsi nilivyotaka kuvunja mkataba ule. Nilikupigia simu ukiwa nje ya nchi, lakini ukasema umepata ushauri wa kamati ya makatibu wakuu, ushauri ambao ulisababisha mkataba usivunjwe?”

Lowassa alisema Rais Kikwete anafahamu kila kitu kwani ni yeye aliyeridhia Rostam Aziz kutafuta mbia baada ya Richmond kushindwa kuleta umeme.

“Uliponitaka ushauri wa mtu wa kutusaidia ili kuondokana na aibu ya Richmond kushindwa kutimiza mkataba wake, nilipokutajia jina la Rostam, haraka ulikubali na kusema, naona hilo ni sawa,” alieleza Lowassa kwa njia ya kumsuta Rais Kikwete.

Kuhusu uchumi, Rais Kikwete alisikika akisema, “uchumi unapaa.” Alisema kuna mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika kipindi cha miaka sita ya utawala wake. Alijigamba kuwa hivi sasa maisha ya Watanzania ni mazuri, ukilinganisha na huko nyuma.

Lakini Rais Kikwete anajua kuwa uchumi haupai bali unatua na umeshindwa hata kuanza kusafiri. Bei za bidhaa nchini, hasa vyakula mbvalimbali, hazikamatiki. Usafiri haushikiki, ilhali sarafu ya taifa – shilingi – inapungua thamani kila uchao.

Mwaka 2011, Rais Kikwete amenukuliwa mara kadhaa akisema, “Hakuna mwanafunzi wa chuo kikuu atakayefukuzwa chuo kwa kukosa ada.” Leo, maelfu ya wanafunzi wako nyumbani kwa kukosa ada.

Wengine wameshitakiwa mahakamani kwa madai kuwa wanachochea migomo vyuoni baada ya serikali kushindwa kuwapa fedha za mikopo wanazostahili kama vile alivyoahidi kiongozi wao.

Amefunga mwaka 2011 kwa shamrashamra za kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa taifa mfu la Tanganyika. Amekuja na ahadi kedekede, ikiwamo kaulimbiu ya "Tumethubutu, Tumeweza na Tunazidi kusonga mbele."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: