Ajali hizi zingezuilika


editor's picture

Na editor - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

APRILI 29 na Mei 29 mwaka huu ni siku ambazo hazitasahaulika katika maisha ya Watanzania. Ni siku za maafa makubwa.

Sasa wananchi wanaweza kuanza kuogopa tarehe 29 za kila mwezi. Kwani ni Aprili 29 wakati mabomu yalipolipuka jijini Dar es Salaam na 29 Mei meli ya mv Fatih ilipozama bandarini Zanzibar.

Kwa upande wa kambi 511KJ ya jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala Kuu Dar es Salaam, mfyatuko wa mabomu aliua watu 26, kujeruhi mamia na kuharibu nyumba na makazi ya wananchi.

Bandarini Zanzibar, tayari maiti 10 zilikuwa zimeopolewa juzi Jumatatu kutoka meli iliyozama. Bado kazi ya uokoaji na utafutaji maiti inaendelea.

Matukio haya mawili yanalazimisha kila mwenye nia njema na nchi na wananchi wake, kutaka kuwepo na uchunguzi wa kutosha ili majanga ya aina hii yasitokee tena.

Katika kitongoji cha Mbagala, hakuna mpaka wa maana kati ya kambi ya jeshi na raia. Toleo hili lina makala juu ya suala hili.

Kinachoonekana ni kwamba ghala la silaha limo uwani mwa makazi ya wananchi na karibu wananchi wanaishi katika kambi ya jeshi. Hii siyo hali nzuri kwa usalama wa jeshi na raia.

Pale bandarini Zanzibar, meli imezama wakati inatia nanga. Kuna maelezo kuwa meli ilipata hitilafu kwa muda mrefu huku nahodha akiwasiliana na kituo cha kuongozea meli kwa muda mrefu bila msaada wowote.

Ukiangalia matukio yote haya mawili utaona kuwa yangeweza kuepukwa. Jeshi lingezuia wananchi kujenga karibu na kambi; lingeweka silaha zake mbali na makazi ya wananchi; au lisingeweka kambi mahali hapo.

Bandarini Zanzibar, nahodha wa meli iliyozama angepewa msaada mapema, hata wa meli ndogo za kusindikiza mv Fatih kwa hatua yoyote ya dharura, ama ajali isingetokea au ingekuwa ya maafa kidogo.

Na mara nyingi meli hazipati uharibifu wa dharura. Hili linatokea kuwa tatizo la muda mrefu ambalo ama halikuonekana au kuna walioliona na kulipuuzia.

Katika hili inaonekana mamlaka za ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini zinalegalega au huduma zake hazipo kabisa; hasa kwa mv Fatih ambayo si siku nyingi ilikuwa imepotea baharini wakati ikitoka Pemba kwenda Unguja.

Ajali hizi zinaonyesha kuwepo chembechembe za uzembe. Kuna kila sababu kwa wahusika kujali na kuthamini kazi zao na wanaowatumikia ndipo taifa liseme “ajali za kizembe sasa basi!”

0
No votes yet