Ajali tunazitengeneza wenyewe, tubadilike

JUMANNE 22 Desemba 2009, nilisafiri kwenda Tanga na kurudi Dar es Salaam. Ilikuwa ni safari ya kawaida ya kifamilia.
Katika safari hiyo, akili ilitafakari juu ya safari salama. Ilitokana na gumzo la vifo vingi vinavyotokana na ajali barabarani, hasa kwa magari yaendayo na kutoka mikoani.
Gumzo mitaani huenda na dhana kwamba vifo vingi hutokea mwisho wa mwaka. Watu wengi husafiri kutoka sehemu wanakofanyia kazi kwenda makwao kuaga na kukaribisha mwaka.
Kulikuwa na ajali kadhaa za malori na mabasi, nilizokutana nazo. Ni kuanzia Kibaha, Mlandizi, Ruvu na barabara ya Segera. Hizi ziligeuza akili zangu. Niliamini usalama ni mdogo katika safari hizi.
Wakati nawaza hayo, kumbukumbu zinanijia kuhusu ajali kubwa zilizotokea hivi karibuni. Watu wasiopungua 30 wamepoteza maisha, wengine kujeruhiwa na upotevu wa mali.
Iliyoshitua ni ile iliyotokea wilayani Same, Kilimanjaro. Ilihusisha basi la kampuni ya Mohamed Trans na basi dogo aina ya Asia Combi. Watu zaidi ya 19 walifariki dunia.
Kwamba kabla ya ajali hiyo, basi la Mohammed Trans lilipasuka tairi la mbele na kuvamia basi hilo dogo, lililobeba watu wa familia kadhaa waliokuwa wakienda harusini Moshi.
Nyingine ilitokea mkoani Dodoma. Lori lililokuwa limebeba mizigo na abiria, likitokea mnadani lilipanda tuta na kupinduka. Takriban watu 10 walifariki dunia.
Pia niliona nusura za ajali kadhaa. Ni wakati wa kupishana. Mifano iko mingi. Wakati wa kupishana mambo huwa mshikemshike.
Binadamu muungwana lazima atashitushwa na wimbi la ajali za barabarani. Kinachoumiza ni vifo ambavyo vina uwezekano wa kuepukwa kama wahusika watafuata taratibu na sheria za barabarani.
Uendeshaji una sheria. Madereva wanaamini kwamba wanazijua lakini wanapuuza. Taratibu za ndani ya basi zinasababisha abiria nao wachangie uwingi wa vifo inapotokea ajali.
Hata kama tutafuata takwimu zitaonyesha kwamba tumekubali ajali kuwa sehemu ya maisha. Ni kwa madereva na makondakta kukiuka sheria.
Katika mabasi matatu tofauti niliyosafiri nayo, niligundua wadau wote katika safari, kuanzia madereva, trafiki, makondakta na abiria, ndio wanaofanya ajali kuwa sehemu ya maisha.
Madereva wana mwendokasi. Inapotokea ajali wakati gari liko kasi ni vigumu maafa kuepukika.
Trafiki wanajua. Kinachofanyika barabarani ni kuonyeshwa tu ratiba ya basi. Hawakagui ubora wa matairi, taa, usukani na hata moshi wa gari kuona kama kuna hitilafu.
Katika safari yangu nilishuhudia mabasi yakiwa yamejaza abiria. Mathalani, Simba Video Coach, nililokuwamo kutoka Chalinze hadi Muheza, lilijaza abiria kupita kiasi. Lilipita njia nzima bila kuguswa huku trafiki wakiona watu wamesimama.
Mbali ya waliosimama, ndani ya basi, majirani zangu wote, hawakufunga mikanda. Mikanda si urembo.
Utafiti unaonyesha kwamba dereva na abiria wakifunga mikanda wanakuwa katika usalama ajali inapotokea.
Tusipofunga mikanda lolote laweza kutokea, iwe kufa au kunusurika. Baadhi huenda kwa waganga kuagua wakiamini wamerogwa wakati huwakufuata taratibu za gari. Unatarajia nini wakati ajali imetokea ukiwa umesimama.
Tufike mwisho. Nchi yenye serikali ya viongozi adilifu hawasubiri kuwajibishwa. Watu wawajibike wenyewe.
Serikali imeshutumiwa. Kwamba imeshindwa mengi. Hili la ajali nalo linaingia katika ya orodha hiyo. Kila mtu anafanya atakavyo. Wananchi hawana budi kuzinduka. Waikatae hali hii.
Natoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza ndugu zao katika ajali za barabarani ndani ya mwaka huu na hata mingine.
Nawatakia afueni wanaouguza majeraha majumbani na hopsitalini. Nachukua fursa hii kuwafariji waliopata ulemavu. Hayo ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Mola azilaze mahali pema peponi roho za wote waliopoteza maisha katika ajali barabarani. Amen.