Ajali ya MV Faith Bandarini: Tunahitaji awepo wa kuchomoka


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version

UNAPATA picha gani usikiapo kuwa kwa karibu saa sita tangu meli ya Mv Fatih ilipofidikia na kuzama baharini – tena ikiwa sura (mlango) ya bandari – hapakuwa na huduma za uokoaji?

Unatarajia nini katika hali ambayo wakuu wengi wa serikali ambao kwa nafasi zao kikazi wangeweza kutoa maelekezo haya walikuwa wamelala fofo?

Kada mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa kiongozi mwandamizi serikalini, ambaye tumekubaliana nisimtaje, alipiga simu nyingi kuarifu baadhi yao. Wachache aliowapata walikuwa hawana taarifa.

Alimpigia ofisa mmoja wa kikachero na kumuuliza iwapo anazo taarifa za ajali, akajibiwa “sijui kwa sasa, ngoja nimpigie….” Ni msaidizi wake.

Nusu saa baadaye, simu ya kachero huyo ilijibu “simu unayopiga imezimwa.” Usishangae kitu; mzee hataki kusumbuliwa.

Na kweli, hakupatikana alipopigiwa tena na tena. Aliendelea kuchapa usingizi. Inawezekana si kulala bali “kula maraha” maana ilibainika alikuwa nje ya kituo chake cha kazi.

Meli ya Mv Fatih ilifidikia kiasi cha saa 4 usiku wa Ijumaa, 29 Mei, muda mfupi baada ya kufika na kutia nanga bandarini Malindi, mjini Zanzibar, na abiria wakiwa wanakaribia ngazi ili kushuka.

Watu wengi walifika mara tu baada ya ajali, lakini hadi saa 9 usiku hapakuwa na huduma yoyote ya kuokoa waliokuwa melini.

Watu hao waliokuwa mita chache kutoka ilipofidikia meli – bila ya shaka kwa kukosa uongozi – hawakuwa na la kufanya zaidi ya kutumbua macho tu.

Kama hapana kiongozi wa kutoa maelekezo wala taa za kuangaza ilipo meli; wafanyeje zaidi ya kuangalia tu. Wanaiona sehemu ya meli iliyobaki juu lakini wenye nyumba hawapo.

Uvumilivu ulipowaishia wakakubaliana kuwa wale wanaoweza kuzamia na kuokoa watu wajitose majini. Wapi? Haiwezekani maana giza limetanda.

Kijana wa familia ya kitajiri anajitolea gari. Inawashwa na taa kuelekezwa ilipo meli, ili kutoa mwanga, kwa mujibu wa waliokuwepo bandarini.

Inaelezwa kwamba meli hii ni mbovu. Ilipotea karibuni wakati ikitoka Pemba kwenda Unguja.

Hiyo ndiyo habari: Hadi saa 9 (usiku wa manane) hapana huduma ya uokoaji. Naibu waziri mmoja alifika saa 10 alfajiri. Ofisa wa juu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) aliyetarajiwa kuongoza shughuli za uokoaji, iliripotiwa kufika saa 12 asubuhi.

Viongozi wengine walifika baada ya kuwa wamekunywa chai makwao asubuhi ya Jumamosi; na wale vigogo, walifika adhuhuri.

Taarifa za kiserikali zinasema si Shirika la Bandari wala KMKM wenye wazamiaji stadi. Walipo wachache, hawana vifaa.

KMKM iliundwa kwa madhumuni ya kutoa ulinzi maeneo ya mwambao wa bahari ya Hindi, eneo la Zanzibar; na kusaidia shughuli za uokoaji. Hawa ni askari wanamaji au Navy kama wale wa Kigamboni, Dar es Salaam.

Ofisa mmoja ndani ya KMKM ameniambia uniti ya wazamiaji ni kama imekufa. Askari wachache waliokuwa na ujuzi baada ya kusomea hadi Uingereza, wamestaafu. Mmoja sasa ni mkuu wa kambi ya KMKM Ungujaukuu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Ndio maana wale vijana waliofika bandarini kutoka Kibweni yalipo makao makuu ya KMKM, walikwenda wao tu. Hawana vifaa. Kwa aibu na hofu ya kusakamwa na umma, walitoweka kimyakimya.

Meli inazama kwenye macho ya Bandari. Hakuna msaada unaopatikana kwa saa tisa. Hii ni katika nchi yenye serikali, rais, waziri kiongozi, mawaziri na watendaji tele.

Nchi ambayo mbali na KMKM, ina vikosi vitatu vingine vya ulinzi: Mafunzo (Magereza), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Valantia. Wote wana mafunzo ya uaskari.

Baada ya wakazi wa Dar es Salaam kushuhudia usanii na sinema bab-kubwa wakati mabomu yalipojilipukia tu yenyewe katika kambi ya JWTZ 511KJ Mbagala Kizuiani, na kukosekana kiongozi hata mmoja wa kuwajibika – maana waziri wa ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi, anasubiri ripoti ya tume aliyoiunda eti ikibaini palikuwa na uzembe ndio awajibike – wananchi wanatiliwa sinema nyingine mpya.

Nchi zetu zina tatizo kubwa la uzembe na uwajibikaji mbaya. Kiwango cha utawala bora kinazidi kushuka. Lakini hakuna anayejali. Hakuna kiongozi anayetambua maana ya dhamana. Ni kutegana tu!

Mwaka 1993 Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) liligharamia mkutano mkubwa wa Afrika Mashariki uliojadili namna nchi zetu zinavyoweza kukabiliana na majanga yanapotokea – waliita Strategies and Preparedness in Disaster Management Workshop.

Ulifanyikia hoteli ya Inn By The Sea ilioko Mbweni na mada mbalimbali zilitolewa. Maudhui ni umuhimu wa serikali na taasisi zake kupanga mbinu za kutoa huduma za dharua pakitokea janga. Labda mafuriko, tetemeko la ardhi, tufani na ajali majini, angani au barabarani.

Kazi hii inahitaji hospitali nzuri, vifaa kamili na dawa; inahitaji madaktari na wafanyakazi wajuzi wa kuhudumia kidharura; magari ya kubebea waathirika; mochwari nzuri.

Serikali ilianzisha mfuko wa maafa na kufadhiliwa kujenga uwezo na ujuzi wa watumishi ili kuhudumia watu pakitokea janga. Zilitoka fedha za kununua vifaa. Ukiuliza leo viko wapi vyote hivi, utakasirikiwa na kushutumiwa.

Baraza la Wawakilishi lilitunga sheria mwaka 2002/03 ya kuwezesha kuwepo mpango mkakati wa huduma za dharura panapotokea janga.

Kwamba pale janga linapotokea, sheria itumike kuhamasisha raslimali watu, zana na fedha ili kusaidia watu walioathirika.

Ukiuliza inatumikaje sheria hii katika kutatua shida zinapotokea, utashutumiwa na kupuuzwa.

Fedha za kujenga uwezo wa serikali kutoa huduma za dharura kwa watu, zinaishia kujenga vikosi vya kupiga na hata kuwaua.

Nani hajui mwenendo wa KMKM, JKU, Valantia na Mafunzo? Wazanzibari wanawajua. Asiyejua atembelee Zanzibar wakati wa uchaguzi. Hakika uwajibikaji wa SMZ upo tu katika kujitanua. Katika ajali hii, lazima tumpate wa kuwajibika.

0
No votes yet