Ajenda ya tija mahali pa kazi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 July 2010

Printer-friendly version
Makala ya Mtangazaji

WIZARA ya Kazi na Maendeleo ya Vijana, inawasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha 2010/2011 kesho, bungeni mjini Dodoma, huku jitihada kubwa zikilenga kumaliza mivutano na wafanyakazi.

Ni takribani miaka 10 sasa, wafanyakazi wamekuwa wakilalamika kupunjwa stahiki zao; wamekuwa wakitaka kulipwa mshahara unaokidhi mahitaji yao; kuboresha mafao yao ya uzeeni hasa yale yanayotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii – hususani mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Mashirika ya Umma (PPF).

Aidha, wafanyakazi wamekuwa wakishinikiza serikali ipunguzwe kodi ya mapato anayolipa mfanyakazi.

Madai haya ni nyeti. Kama hayatazingatiwa vilivyo, yanaweza kuathiri hata amani na utulivu uliopo nchini. Ni kwa sababu, hakuna asiyejua jinsi gharama za maisha zilivyopanda.

Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, anatarajiwa kuliambia Bunge la taifa, pamoja na mambo mengine, jinsi serikali ilivyojipanga katika kumaliza matatizo ya wafanyakazi.

Kwanza, serikali tayari imepitisha sheria mbili muhimu: Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (Social Security Regulatory Authority Act) Na. 8 ya mwaka 2008 na sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Act) Na. 20 ya mwaka 2008.

Sheri hizi zinasaidia kutoa matumaini katika kurekebisha hali ya mafao ya uzeeni na mafao ya fidia kwa wanaoumia au kuugua kazini. Taratibu za kuwalea walioathirika na maradhi au ajali kazini hadi wanakufa. Haya ni mambo ambayo serikali inasema yanatia matumaini.

Kabla ya kupitishwa kwa sheria hii, waliokuwa wanaugua au kuumia kazini, walikuwa wanalipwa kwa mkupuo na kutelekezwa; malipo ambayo yalilipwa kwa kutumia viwango vya mwaka 1966.

Hali ni hiyohiyo katika mafao ya uzeeni. Ni dhahiri kuwa kuna kupishana sana kwa mafao baina ya mifuko ya hifadhi inayowatumikia Watanzania walewale. Profesa wa Chuo Kikuu anapoondoka na Sh. 10 milioni na akiwa hana pensheni ya kila mwisho wa mwezi inatia huruma na machungu.

Tunaambiwa hali hiyo ni afadhali ukilinganisha na siku za nyuma ambazo Profesa kama huyo alikuwa anaondoka na shilingi laki nne au tano. Je, tungewatembelea leo huko waliko, tungekutaje hali zao za maisha?

Bila shaka kwa watu kama hawa ambao wametumia muda wao wote, akili zao zote kutumikia taifa, bila kufanya shughuli nyingine za kipato, hali zao ni mbaya.

Hali hiyo, ndiyo inayowakatisha tamaa wahadhiri waliopo leo katika vyuo vya umma. Huu ndiyo msingi wa vijana wengi kutokimbilia kazi hii sasa.

Haya ni mapungufu makubwa. Lakini inatarajiwa kuwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii ambayo inatarajiwa kuanza kazi hivi karibuni, italipa kipaumbele suala hili.

Mengine ambayo mfuko huu unatakiwa kuangalia kwa jicho la haraka, ni ushindani katika kupata wanachama na uhamasishaji wa mafao pale mfanyakazi anapolazimika kujiunga na mfuko mwingine. Kama haya yatapatiwa ufumbuzi kwa wakati mwafaka, yatawapatia wafanyakazi wa Tanzania matumaini mapya.

Ni muhimu pia mfuko wa fidia kwa wafanyakazi ukaundwa haraka.

Jingine ambalo tunapenda kuligusia hapa, ni lile linalohusu kima cha chini cha mshahara. Suala hili, pamoja na lile la kiwango cha kodi ya mapato vinaendelea kuibua hisia kali miongoni mwa wafanyakazi.

Kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana serikali hii ya Awamu ya Nne, imekuwa ikiongeza mishahara ya kima cha chini kila mwezi kutoka Sh. 64,000 hadi Sh. 80,000 na hatimaye sasa zimefikia Sh. 104,000.

Katika bajeti hii, tumesikia kiwango hiki kimeongezeka. Hii inatoa matumaini mapya; hata kiwango cha kodi nacho kimepungua kutokana na majadiliano ya pamoja kati ya wafanyakazi na serikali.

Vilevile, kumetokea mabadiliko makubwa katika viwango vya kima cha chini vya mishahara katika sekta mbalimbali binafsi. Tangu Novemba 2007, sekta hii ilikuwa imegubikwa na utata na vurugu. Yote haya yamewezekana kupitia ushirikiano kati ya wafanyakazi kupitia bodi zao za kisekta na serikali.

Tungependa kuvipongeza sana vyama vya wafanyakazi hususani viongozi wao, kwa kusimama imara katika kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi.

Kwa kupitia taratibu za kitaifa na kimataifa kama zilivyoainishwa na Shirika la Kazi duniani (ILO) zinazohimiza majadiliano ya pamoja, wameweza kufanikiwa kupata ufumbuzi wa mambo mengi mazito ambayo yalikuwa hayajatatuliwa kwa miaka mingi.

Kwa kuzingatia utaratibu huu, kutokana na ujasiri wa vyama vya wafanyakazi, imegundulika kwamba hakuna lisilowezekana. Ni vema utamaduni huu ambao unazingatia kuheshimiana kwa kambi zote mbili ukadumishwa. Hatutarajii kambi moja itatumia vitisho dhidi ya kambi nyingine.

Kuhusu suala la tija mahali pa kazi: Suala la nyongeza ya mishahara ni suala tamu kulisikia na kulipata, lakini ni vema wafanyakazi wakatambua kuwa wakati waajiri wanaendelea kuboresha mishahara, mafao na maslahi yao, yote haya na mengine yatawezekana iwapo suala la tija mahali pa kazi litazingatiwa.

Taifa hili, linakabiliwa na tatizo kubwa mahali pa kazi. Sote tunashuhudia huduma zinavyotolewa chini ya viwango katika shule, hospitali, maofisini na katika maeneo mengine mengi. Wakati mwingine huduma hizi hafifu huambatana na mambo ya rushwa.

Hata uzalishaji viwandani umepungua na kile kinachozalishwa kiko chini ya kiwango. Hali hii, haikubaliki na imepunguza kwa kiwango kikubwa uwezo wa waajiri kuboresha maslahi yao.

Tunatoa ushauri kwamba ajenda hii ya tija mahali pa kazi, iwe ni ya kudumu kwa vyama vya wafanyakazi nchini na pale inapobidi washirikiane na waajiri wao kuisimamia.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)