Akili ya Sofia haiwezi kuwaza zaidi ya ngono!

KUNA dhana iliyojengwa kwamba watu wenye fikra nyepesi hujadili watu; wenye fikra za kati hujadili matukio na wale wenye fikra pevu hujadili dhana au tuseme mawazo.
Ingawa ni ukweli kwamba nadharia hii hutoa changamoto katika jamii ili watu wajielekeze kujadili mambo ya maana na si kubobea katika umbeya, ni vigumu pia kufungwa katika misimamo hii hasa tunapotazama ofisi za umma na waliozikalia.
Hakuna ubishi kuhusu nafasi ya waziri katika serikali kwamba ni kubwa, nzito na nyeti katika kuendesha si nchi tu, bali pia katika kushughulikia matatizo ya wananchi.
Kwa kawaida mtu anayebebeshwa jukumu la uwaziri katika jamii kama yetu, anatarajiwa awe ni mtu ambaye ana upeo, anayetambua dhamana aliyopewa ina maana gani kwa taifa lake?
Ndiyo maana hata “wanaposaga” fedha za walipa kodi, inakuwa si shida sana kwa sababu wanatarajiwa kusaidia kutatua kero za jamii.
Nafasi za uwaziri katika nchi zote duniani ni chache lakini nyeti, ndiyo maana wenye wajibu wa kuteua watu wa kushika nafasi hizo hutakiwa kujaa hekima na busara ili uteuzi utakaofanywa kwa kweli uonekane ukijielekeza kuisadia jamii kukabiliana na changamoto za maisha.
Unapozungumzia uwaziri kwa taifa kama hili, kinadharia unazungumzia mtu aliyepewa dhamana ya ofisi ya umma akiwa na mlolongo wa changamoto.
Kwanza, kuwa mstari wa mbele katika kusaka mwarobaini wa umasikini wa watu wetu; kuwa mbunifu wa kutumia rasilimali za taifa ili kuleta mabadiliko ya maana katika maisha ya wananchi kwa ujumla wake.
Uwaziri kwa maneno mengine unatakiwa uelekezwe kwa mtu ambaye atatambua kwamba cheo alichopewa ni mzigo; ni kutumika, ni kutumwa na kukosa usingizi.
Kama hiyo ni sehemu ya sifa ya mtu anayestahili kukabidhiwa nafasi ya uwaziri; basi hapana shaka kwamba wengi wa mawaziri wetu hawastahili katu kukalia nafasi walizopewa.
Hawastahili kwa sababu wamekosa sifa hizo kutokana na matendo yao kila uchao; ni watu wasiosumbuliwa na umasikini wa watu wetu.
Lakini zaidi sana ni watu wasiokuwa na fahamu kama wao ni mawaziri na kwamba wanatarajiwa walau waonyeshe mfano wa nini kifanyike ili kutokomeza umasikini wetu.
Bahati mbaya wengi wamebakia kuwa watazamaji. Hawana mbinu wala mikakati.
Kwa kawaida uwaziri ni dhamana, na kwa maana hiyo ni vigumu kuutengenisha uwaziri na utu wake, vimeshikamana kwa kuwa ni kwa muunganisho wa utu na uwaziri (cheo) ndipo maana ya nafasi hiyo inaonekana kwa jamii.
Yupo Waziri wa Ofisi ya Rais Utawala Bora, Sofia Simba, huyu pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT-CCM), ni waziri ambaye amepewa dhamana nzito, ‘utawala bora’.
Katika malengo makuu ya Mpango wa serikali wa Kupunguza Umasikini nchini (Mkukuta) suala la utawala bora ni miongoni mwa malengo makuu matatu yaliyoanishwa.
Mengine ni kuwaongezea watu kipato na kuwapatia maisha bora. Kwa maana hiyo, suala la utawala bora ni jambo linalopewa umuhimu wa kipekee ili kung’oa umasikini nchini.
Kwa hiyo, Sofia si waziri mwepesi kwa maana ya majukumu ya utawala bora; ni waziri ambaye katika hali yoyote ile kuzungumzia habari ya mapambano dhidi ya rushwa nchini angepaswa aonekane akiwa mstari wa mbele kwa sababu hilo ni eneo lake la kujidai.
Ukizungumzia habari ya demokrasia; hapo kungekuwa ni nyumbani wake; lakini pia ukizungumzia habari ya kudhibiti watumishi wanaojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili na sheria za utumishi, hapo pia ungemwona. Lakini wapi!
Pamoja na majukumu yote haya, Sofia ni mweupe kama ubongo wa kichanga cha leo. Hana lolote katika fikra zake kinachokaribia kumfanyakutambua majukumu yake.
Ni waziri ambaye kwa utumishi wake wa miaka takribani mitano sasa kwanza kama Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na sasa Utawala Bora, ni vigumu kusema kwa yakini anafanya nini serikalini kama si kusubiri mshahara na marupurupu mengine ya uwaziri tu.
Hivi karibuni kwa kuthibitisha kiwango cha ufinyu wa fikra zake, aliwaambia wanawake wa CCM kwamba kama waume wao wanasaidia vyama vya upinzani, basi njia ya kuwakomesha ni kuwanyima tendo la ndoa.
Eti tendo la ndoa kwake ndicho kitu anachokiona cha maana na muhimu kutumika kama silaha! Sofia! Sofia!
Naogopa kumtaja Mama huyu kama ni mkware au vipi, yaani pamoja na nafasi zake zote alizoshikilia – waziri, mwenyekiti wa UWT, mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama chake, uwezo wake wa kifikiri hauvuki hisia na matamanio ya ngono!
Huyu ni kiongozi anayejinasibu kuwa anaweza kuwaunganisha wanawake na kuwaelekeza kwenye ukombozi wa kweli.
Ni mwanamke ambaye alitarajiwa kuwa nguzo ya wanawake wa CCM katika kuwaunganisha na kuwaelekeza kwenye njia inayofaa katika mapambano dhidi ya umaskini.
Ni mwanamke ambaye kwa macho ya wengi, angejua vilivyo njia bora zaidi za kupita ili wanawake wa taifa hili wajikomboe dhidi ya madhila ya umasikini wa kipato.
Alitakiwa kufahamu kwamba madhira haya yanachangiwa pamoja na mambo mengine, mfumo dume unaokataa kutambua nafasi za wanawake katika milki ya mali katika jamii.
Sofia kila anapomwaangalia wanawake wenzake anamwangalia kama mashine ya kumtuliza mwanaume; fikra zake kuhusu wanawake ni ngono.
Kwake, haoni nguvu nyingine yoyote ya wanawake ambayo inaweza kutumiwa kuleta mabadiliko katika jamii yetu; kwake mwanamke ni kiungo chake cha uzazi basi.
Katika dunia ya watu wanaowaza sawasawa siku Sofia alipotoa kauli ya kuwataka wanawake wawanyime waume zao unyumba, tungeona taharuki kubwa serikalini na hata bosi wake angemkemea kama si kumweka pembeni.
Lakini kwa kuwa nafasi za uwaziri zilikwisha kurahisishwa siku nyingi, bado ataendelea kutesa na kutesa, kwani ana shida gani wakati akili yake imeganda kwenye ngono na hicho ndicho kilichompa uwaziri?
- Login or register to post comments