Alivyoondolewa Kifukwe hatua kwa hatua


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Francis Kifukwe na Yussuf Manji

MTU yeyote aliyefuatilia siasa za uchaguzi wa viongozi katika klabu ya Yanga atagundua kuwa Francis Kifukwe hakuwa na nafasi katika safu mpya—alishaondolewa na Jumapili ilikuwa siku ya kuhitimisha.

Waliomwondoa ni viongozi wa Kamati ya Uchaguzi na Mdhamini mkuu, Yussuf Manji.

Kauli ya mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera ilikuwa ya kumalizia mchezo uliofanyika awali.

Kamati ya uchaguzi, chini ya mwenyekiti Jaji John Mkwawa ilikata jina la Kifukwe kwa madai alishindwa kutokea kwenye usaili.

Sababu hiyo haikuwa na nguvu kwa sababu Kifukwe aliomba ruhusa kwamba angekuwa safarini wakati wa usaili. Ndiyo maana Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipoketi kupitia rufani yake iliona kamati ya uchaguzi ya Yanga ‘imechemka’.

Lakini takriban wagombea wote walikuwa wanasubiri upepo wa mdhamini mkuu, Yussuf Manji utavuma kuelekea wapi.

Ilidaiwa mapema kwamba, Manji alikuwa akimfikiria zaidi mwanasheria Lloyd Nchunga ambaye ni kipenzi pia cha makamu mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Ridhiwani Kikwete.

Ridhiwani alipoachiwa nafasi ya uenyekiti, na kwa hiyo ndiye aliyekabidhiwa rungu la kusimamia uchaguzi huo uliofanyika kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, mazingira ya kuelekezwa kibra yakawa wazi.

Jaji Mkwawa alikuwa safarini kikazi, hivyo Ridhiwani alitumia rungu lake kumtwanga Kifukwe usoni.

Aliposema “…msichague watu wanaotoka Baa ya Bakulutu (Kinondoni). Yanga inahitaji maendeleo na daima mbele nyuma mwiko, msisikilize kelele za kuiletea maendeleo Yanga leo wakati huko nyuma walishindwa, maana tunaweza kukaa miaka minne tukawa tunalia huku makosa tumefanya sisi wenyewe,” Ridhiwani alimlenga Kifukwe.

Iko hivi. Wakati Rais wa Yanga ni Tarimba Abbas, klabu hiyo ilikuwa na maseneta 12 wakiwemo Mbaraka Igangula na Kifukwe. Igangula alikuja kuchaguliwa makamu wa rais na aliongoza miezi kadhaa baada ya Tarimba kujiuzulu.

Ulipofanyika uchaguzi mkuu, Kifukwe alishinda nafasi ya rais huku katibu mkuu akiwa Jamal Malinzi. Ndiyo maana, Kifukwe alipodaiwa aliuza gari la klabu hiyo na pesa kutia ndani, Malinzi aliwasilisha utetezi kwenye kamati hiyo, lakini ulitupwa.

Kwa hiyo, Ridhiwani alipokuwa anasema wasichaguliwe watu waliowahi kuongoza, kilikuwa kijembe dhidi ya Kifukwe. Lakini pia kijiwe cha Kifukwe anapopata kinywaji chake ni Baa ya Bakulutu.

Manji naye anaingia. Katika namna ya kushangaza kabisa, baada ya Kifukwe kushushiwa rungu na kukosa utulivu, Manji alimfuata nje na kumshauri ajitoe.

Lakini ni Manji aliyewaita tena wagombea wote wa nafasi ya uenyekiti, Nchunga, Igangula na Ahmed Falcon na kuwaambia yeyote kati yao akishinda ahakikishe anamteua Kifukwe kuwa mjumbe wa Baraza la Wadhamini.

Huu ni ushahidi mwingine kwamba safu ilishapangwa na ili Kifukwe asijisikie vibaya ashirikishwe kwenye nafasi nyingine.

Sawa. Kwa nini Manji anamwombea nafasi ya uongozi wakati uchaguzi ulikuwa haujafanyika? Maana hata kuitwa kujieleza ilikuwa bado.

Kwa nini Manji hakumshauri Kifukwe kupambana kufa kupona badala yake akataka ajitoe? Kama mfumo wa uchaguzi haumtaki, atakubaliwa vipi kuingizwa kwenye jopo la ‘wateule’ hao?

Kifukwe na Igangula walipaswa kusoma mazingira yaliyosababisha aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Masauni Yussuf Masauni kujiuzulu.

Wangejiuzulu nani walikuwa wahusika wakuu, ilikuwaje na waliweka mkakati gani, wangegundua watu wale wale ndio wamejipa uwezo wa kuweka watu madarakani na kuwaondoa.

Kwa hiyo, Bendera alipoibuka na kutoa rai Kifukwe asijitoe na hata kulazimisha wanachama kumpigia kura alikuwa anajaribu kuondoa kiwingu tu ukweli hakuwa na nafasi.

Hivi angeshinda katika mazingira hayo, wanachama 1437 waliomchagua Nchunga wangeridhika kwamba haki imetendeka? Kanuni za uchaguzi wa klabu hiyo zingeruhusu? Kila la kheri uongozi mpya.

0
No votes yet