Aloyce Kimaro aapa: Sitanyamazia ufisadi

MBUNGE wa Vunjo (CCM) Aloyce Kimaro, bado anang’ang’ania watuhumiwa wa ufisadi na kusema, “Katika hili, katu sitarudi nyuma.”
Kimaro, mmoja wa wabunge waliojitokeza kuwa na kauli kali na komavu, ndani na nje ya bunge, amesema katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, “Sitarudi nyuma.”
Ni Kimaro aliyetaka uchunguzi ufanywe kuhusu jinsi mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya, ulivyobinafsishwa na kudai kuwa rais mstaafu Benjamin Mkapa anatajwa katika umiliki huo.
Akiongea kwa uchungu, Kimaro alitaka serikali kurudisha mikononi mwa wananchi mgodi huo na bila mjadala.
Alimtuhumu Mkapa akisema alishirikiana na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona kujimilikisha mgodi huo kinyume cha sheria na bila kufuata taratibu.
Sasa ni takriban miezi mitatu tangu Kimaro alipotaka serikali kuchukua hatua. Je, ameridhika na mwenendo wa serikali?
“Angalau serikali imesikia wananchi wanataka nini. Sisi kama wabunge ni vipaza sauti vya wananchi. Ni wajibu wetu kusema kile ambacho wananchi wanataka na serikali ina wajibu wa kusikia na kutekeleza,” alisema.
Anasema katika “sakata la Kiwira,” alichotaka yeye ni kuonyesha watawala kuwa wana wajibu wa kutenda kwa kufuata haki na taratibu.
“Nilitaka kukomesha utaratibu huu wa kiongozi kutumia vibaya madaraka yake. Ule utaratibu uliozoeleka wa kutumia madaraka kujinufaisha. Huu si utaratibu mzuri. Huo ndio niliotaka kuukomesha,” anasema Kimaro.
Anasema mambo ya aina hiyo yasiposemwa hadharani, “Watu hawatajirekebisha. Nilichotaka ni kufuta utaratibu wa mazoea ya viongozi.”
Alipoulizwa alitaka Kiwira ifanywe nini hasa, Kimaro alijibu haraka, “Nataka irudishwe mikononi mwa wananchi. Huo ndio msimamo wangu na kamwe siwezi kurudi nyuma.”
Alipoulizwa iwapo haitarudishwa atafanya nini, Kimaro alisema, “Nitaendelea kusisitiza irudishwe mikononi mwa wananchi.”
Mwanasiasa na mfanyabishara, Kimaro amekuwa mwiba kwa baadhi ya wabunge na wanasiasa hasa wale wanaoonekana kupalilia ufisadi. Anasema, “Taifa tayari lilifikia mahali pabaya kutokana na kujengwa mtindo wa kulindana.”
Anasema dhamira yake ya kupambana na ufisadi haiwezi kuporwa na mtu yeyote yule na kwamba vita hivyo si vyake peke yake.
“Tuko wapiganaji wengi na tumetapakaa kila pembe ya nchi,” anasema Kimaro kwa kujiamini.
“Hivi ni vita ambavyo havina mipaka na siyo vya mtu mmoja. Ni vita vikubwa kati ya wapenda haki ambao ni wengi, na mabeberu na wafuasi wao ambao ni wachache,” anafafanua.
Anasema, “Mimi na wenzangu ni wawakilishi wa wanananchi ambao ndio wanapigana vita hivi vya ukombozi mpya,”
Taifa, anasema Kimaro, lilikuwa limeanza kujenga matabaka ya watu; hasa viongozi kutoulizwa hata pale inapobainika wazi wamepora uchumi wa taifa na kutumia vibaya madaraka waliyopewa.
“Tulikuwa tunakwenda kubaya. Sasa tunataka kuhakikisha kwamba kila kiongozi anawajibika kulinda maslahi ya wananchi na kuheshimu dhamana aliyopewa,” anaeleza.
Kimaro ambaye kitaaluma ni mwalimu wa masomo ya hisabati na fizikia aliyefundisha shule mbalimbali ikiwamo Minaki na Azania, zote za Dar es Salaam, anasema serikali ikikubali kunyamazia ufisadi itakuwa imekubali kutawaliwa na mafisadi.
Alipoulizwa iwapo watawala hawatamsikiliza atachukua hatua gani, Kimaro alisema, “Sitarudi nyuma mpaka kilio cha wananchi kisikilizwe.”
Alipobanwa ni akina nani wengine alionao, Kimaro hakuwa tayari kuwataja badala yake alisema, “Nimekwambia tunafanya kazi ya wananchi.”
Awali, Kimaro alikuwa mwanachama wa vyama vya upinzani vya NCCR-Mageuzi na Tanzania Labour Party (TLP).
Alipoulizwa kama haoni hatari ya watuhumiwa wa ufisadi kuungana na kupanga njama za kutompitisha kugombea tena ubunge katika uchaguzi ujao, alisema haraka kuwa haoni kama kuna hatari kama hiyo.
“Sioni. Hakuna kitu kama hicho. Hakika, nakwambia mafisadi watashindwa, kwa sababu wako wachache na sisi tuko wengi. Si hivyo tu, wananchi tayari wamewaelewa na kuwafahamu,” alisema kwa kujiamini.
Alipoulizwa iwapo mafisadi ndani ya CCM watafanikiwa kumbana na kumning’iniza ataunda chama chake au atajiunga na vyama vingine vilivyopo, Kimaro alisema hafikirii kutoka CCM.
Anasema, “Sina mpango wa kutoka CCM. Hiki ni chama kizuri sana. Ni chama kinachojisafisha kwa kila tuhuma. Hiki ni chama kikubwa chenye wanachama nchi mzima. Sasa humo ndani ndiyo utakuta wanachama wengine si waaminifu.”
Anasema, “Ndani ya chama hiki, kutokana na ukubwa wake, wamo watu ambao si waaminifu. Sasa ni jukumu letu kupambana na wanaochafua chama chetu ili kiwe safi mbele ya jamii.”
Alipotakiwa kutoa maoni kuhusiana na hatua ya serikali ya kulegeza kamba kuhusu mafisadi, Kimaro alisema ni lazima serikali itachukua hatua.
Alisema, “Kwa sasa siwezi kusema kwamba serikali imelegeza kamba dhidi ya mafisadi. Serikali imeomba muda ili ishughulikie tatizo hili.”
Akiongea kwa njia ya kusisitiza, Kimaro alisema, “Tungoje. Kama hatua hazijachukuliwa tunaweza kusema kwamba serikali inaogopa mafisadi.” Lakini siyo sasa.
Anasema kabla ya muda huo kwisha ni vigumu kusema kwamba serikali imeogopa mafisadi.
“Hii ni serikali ya wananchi. Serikali ya wananchi inatenda yale ambayo wananchi wanataka. Na katika hili, wananchi wanataka serikali ishunghulikie mafasadi, tena bila kuwatazama usoni,” alisema.
Kuhusu maendele ya jimbo lake la Vunjo, Kimaro alisema amefanya mengi. Kubwa analojivunia ni kuanzisha taasisi ya fedha inayojulikana kama VIKOBA.
Taasisi hiyo tayari ina wanachama 3000; inatoa mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kimaro ameoa. Ana watoto watatu; wawili wa kiume na mmoja wa kike.