Amani Kongo-DRC njiapanda


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 21 December 2011

Printer-friendly version

HALI ya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni mbaya. Siku nne tangu Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo (CENI) itangaze matokeo ya urais, Polisi imeanza kusaka wafuasi wa upinzani kwenye nyumba zao.

Tume hiyo ilitangaza Ijumaa wiki iliyopita kwamba Rais Joseph Kanambe Kabila ameshinda tena kiti hicho kwa kupata asilimia 49 wakati kiongozi mkuu wa upinzani, Etienne Tshisekedi alipata asilimia 32.

Kwa mujibu wa CENI, Kabila alipata kura 8,880,944 na Tshisekedi kura 5,864,775.

Nafasi hiyo iligombewa na wanasiasa wengine tisa, wengi wakimuunga mkono Tshisekedi anayeongoza Chama cha Union Democratie Populaire et Sociale (UDPS). Kabila anatoka chama People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD).

Mara baada ya matokeo hayo kutangazwa, Tshisekedi naye alijitangaza mshindi kwa kupata asilimia 54 ya kura kutokana na kile alichokieleza “matokeo ya kura zilizokusanywa vituoni na chama changu.”

Aliwaambia wafuasi wake mjini Kinshasa, “…kuanzia leo hii (Desemba 9), mimi ndiye rais wenu wananchi wa Kongo-DRC.”

Tangazo la Tshisekedi lilipokewa kwa ukali na msemaji wa serikali, Lambert Mende, aliyekaririwa na shirika la habari la Ufaransa (AFP) akiita kauli hiyo ni “uvunjaji matakwa ya katiba ya nchi. Na mtu aliyeitoa (Tshisekedi) anapaswa kukamatwa kwa kuchochea vurugu.”

Matokeo yaliyotangazwa na tume ambayo kiongozi wake, Daniel Ngoy Mulunda, ni mchungaji binafsi wa Kabila, yamekataliwa na jumuiya ya kimataifa kwa maelezo kuwa yametokana na ukiukaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi.

Taasisi za watazamaji uchaguzi zilizotuma wataalamu wake DRC, ikiwemo Carter Centre ya Marekani, zimesema matokeo ya CENI hayakuendana na maamuzi ya wananchi.

“Tatizo ni dhahiri kwamba hatua ya ujumlishaji wa kura ilijaa kasoro,” alisema David Pottie, kiongozi wa watazamaji wa Carter akiwa mjini Kinshasa.

Alizitaja baadhi ya kasoro kuwa ni matokeo ya vituo 2,000 vya uchaguzi katika jiji hilo kutopatikana huku vituo vingine ambavyo wapigakura wengi walijitokeza kupigakura, vikitangazwa kuwa watu wake walimuunga mkono Rais Kabila kwa asilimia 100.

Kituo cha Carter – kinachotokana na taasisi ya Jimmy Carter, rais mstaafu wa Marekani – kilisema kwa namna kazi ya ujumlishaji kura katika vituo vyote 169 nchi nzima ilivyofanywa, wametoa alama ya asilimia 40 tu ya mafanikio.

“Tunathubutu kusema kuwa ukiukaji wa taratibu za uchaguzi tuliogundua ni mkubwa mno kiasi cha kutibua matokeo ya mwisho ya uchaguzi,” alisema Pottie. Aliongeza, “Lakini, baada ya kusema hivyo, hatuna njia ya kufanya kuhusu kura milioni 1.5 na tunasita kutambua matokeo rasmi ya uchaguzi huu.”

Vyanzo vingine vya habari vimesema kasoro nyingi katika kuhesabu kura zilidhihirika jimbo la Katanga, kusini mwa nchi, anakotoka Mulemba-Nkulu. Wastani kwa nchi nzima wa kujitokeza kwa wapigakura ulikuwa chini ya asilimai 59, lakini kwa Mulemba-Nkulu, ulikuwa ni asilimia 99.46 huku kura zote 266,000 zilizopigwa zikimchagua Kabila.

Watazamaji wengine waliripoti kuwa wananchi walichoma moto magari mengi yaliyobeba masanduku yaliyosheheni kura bandia na baadhi ya waliokamatwa nayo waliuawa.

Baadhi ya kura hizo ziliingizwa kwenye masanduku dakika za mwisho baada ya upigaji kura kukamilika, tena bila ya kuthibitishwa kisheria huku yakifunguliwa katika vituo vya kuhesabia pasipo ushuhuda wa watazamaji. Masanduku mengine yalikatwa lakiri za vyama bila kushuhudiwa na wawakilishi wa vyama vya upinzani.

Matokeo ya awali yalionyesha Kabila alipata asilimia 46 ya kura dhidi ya 36 za Tshisekedi, lakini matokeo hayo tayari hayakuzingatiwa na tume. Ni matokeo hayo yalipokamilika, upinzani ulitangaza kuwa Tshisekedi ameshinda kwa asilimia 52.8.

Wagombea wengine walipata kura kama ifuatavyo: Andeka Djamba 0.6; Bombole Adam 0.8; Kabila Kabange 26.1; Kakese Malela 0.5; Kamerhe Vital 14.8; Kashala Oscar 0.4; Kengo Wa Dondo 2.5; Mbusa Nyamwisi 0.4; Mobutu Nzanga 0.8 na Mukendi Kamama 0.4.

Zipo taarifa zilizokariri kituo cha redio cha makao makuu ya Kanisa Katoliki Duniani mjini Vatican zilizoeleza kuwa Wakongomani wamemchagua Tshisekedi kuwa kiongozi wao. Kanisa hilo lilituma watazamaji 30 kuangalia uchaguzi nchini humo.

Siku moja kabla ya tume kutangaza matokeo, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Kongo-DRC (MONUSCO) kilihimiza wahusika katika kila eneo, waache vitendo vitakavyochochea fujo.

Kwa kuzingatia taarifa za watazamaji wa kimataifa, Mwakilishi Maalum wa kikosi hicho, Roger Meece, alisema kulikuwa na ukiukaji wa taratibu za uchaguzi tangu hatua za awali za uchaguzi na akasihi vyama vyote vilivyoshiriki kuwasilisha malalamiko yao kwa njia za amani kwa chombo kilichowekwa kisheria, ikiwemo mahakama.

Taarifa zinasema muda mfupi kabla ya matokeo kutangazwa na baada, polisi waliokuwa na bunduki za aina ya AK-47, walionekana wakivamia majumba ya raia katika jiji la Kinshasa, na kutoka na vijana walioaminika ni wafuasi wa Tshisekedi; waliwapakia kwenye magari yao na kuondoka nao.

Pia kuliripotiwa matukio machache ya uporaji madukani katika mitaa ya jiji hilo.

Wanaharakati wa haki za binadamu walisema siku chache kabla ya uchaguzi walishuhudia maiti za watu 18 waliouawa. Kumekuwa na madai kuwa wengi wao waliuawa na askari wa kikosi maalum cha ulinzi wa rais. Haijathibitishwa.

Wachambuzi wengi wanasema uchaguzi huo wa pili kufanyika tangu kuanguka kwa utawala wa dikteta Mobutu Sese Seko na kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyohusisha pia mataifa ya kigeni ya nchi jirani, haukukidhi matakwa halisi ya Wakongomani.

Raia wapatao milioni tano waliuawa katika vita vya ndani ya nchi kati ya miaka ya 1990 na 2000.

Ingawa wachambuzi wanasema si rahisi kuibuka kwa vita haraka kutokana na kuwepo kwa askari 19,000 wa Umoja wa Mataifa nchini humo, kuvurugwa kwa uchaguzi huo kunatengeneza mazingira ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Pia mazingira haya yatazidi kuzorotesha maendeleo ya nchi ambayo jirani zake, wanajitahidi kupiga hatua kwa kunufaika na utajiri na hata udhaifu wa Kongo-DRC.

Wafuasi wa Tshisekedi wa ndani na walioko nje barani Ulaya na Marekani wamepinga ushindi wa Kabila, mwanasiasa kijana anayedaiwa kutokuwa Mkongomani, bali Mnyarwanda.

Gazeti hili limepata kuchapisha taarifa hizo kwa kukariri gazeti la l’Oeil du Patriote (Jicho la Mzalendo) linalochapishwa nchini Ufaransa, taarifa nyingine za vyombo mbalimbali duniani, watu mashuhuri na raia wa DRC, zikisema baba mzazi wa Joseph Kabila anaitwa Adrien Christofer Kanambe na mama yake halisi anaitwa Macelina.

Kabila mwenyewe hajawahi kukanusha taarifa hizo za Wakongomani walioko zinazong’ang’ania kuwa wazazi wote wa Kabila ni Wanyarwanda.

Juhudi za upinzani kumzuia Kabila kugombea urais kutokana na utata huo wa uraia, hazikufua dafu.

0
No votes yet