Amani tunayo, soka mbovu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version

SOMALIA haijaonja amani tangu mwaka 1991 baada ya Rais Siad Barre kupinduliwa. Kila siku wananchi wa Somalia wanasikia milio ya bunduki kati ya wababe wa vita.

Pamoja na kukosekana utulivu, uchumi kuvurugika na mambo mengi kuparaganyika, bado kila mwaka timu ya taifa ya Somalia na klabu bingwa hushiriki mashindano ya kimataifa ikiwemo ya Cecafa.

Mara kwa mara ligi yao huvurugwa na mapambano ya silaha na viongozi hukosa fursa ya kuteua wachezaji na kusimamia mazoezi. Wasamaria wema ndio hugharimia mazoezi ya timu yao ya taifa, wachezaji hukusanywa Kenya. Timu hiyo ya kuungaunga mwaka juzi, iliichapa Kilimanjaro Stars bao 1-0 katika michezo ya Kombe la Chalenji.

Angola, ambayo ilipata utulivu baada ya kuuawa Jonas Savimbi mwaka 2002 imepiga hatua kisoka na ingawa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo haina utulivu kwa miaka mingi, Tanzania haifui dafu katika soka.

Liberia iliyokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na nchi kama Rwanda na Burundi huzichachafya timu za Tanzania mara nyingi.

Tanzania inakosea wapi katika soka hadi inatolewa na wadogo zetu kisiasa Msumbiji? Msumbiji inaweza vipi kuandaa Michezo ya Mataifa ya Afrika? Kwa nini amani na utulivu wa Tanzania haujasaidia kupata mafanikio ya kiuchumi na kimichezo?

Wadau wa michezo wanaosoma safu hii wamekuwa wakitoa maoni yao juu ya kinachosababisha Tanzania kuwa kibonde. Je, unakubaliana nao? Wanasema:

Nimefurahishwa na staili yako ya kukusanya mawazo shirikishi. Mimi ningekuwa kocha ningetafuta vipaji kwa kusaka wachezaji warefu wenye misuli timu nzima. Amini usiamini, tatizo liko kwenye ufupi wa wachezaji na maumbile madogo. Hili ni tatizo katika nchi za Afrika Mashariki. 0713233201.

Nimesoma maoni ya wadau mbalimbali lakini ukweli hakuna njia ya mkato kwenye mpira. Watanzania mara nyingi tumekuwa tunataka mafanikio ya haraka wakati hatujafanya juhudi zozote.

Klabu hazitimizi wajibu wao na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hawajafanya wajibu wao, hawasimamii yale waliyoagiza. Mfano walitaka kila klabu ya Ligi Kuu iwe na timu za vijana, je, klabu zimeanzisha timu za vijana? Je, hao waliopo wanaendelezwa?

Huu nimwaka wa tano yanafanyika mashindano ya Copa Coca Cola, kama wale watoto wangeendelezwa wengi wao wangekuja kucheza kwa umahiri Ligi Kuu ya Bara. Lakini kwa bahati mbaya wengi wao hawajulikani walipo. 0777436701.

Tatizo kubwa linaloathiri maendeleo ya michezo nchini ni miundombinu. Inachangia ugumu wa uendelezaji na ukuzaji wa vipaji vya michezo kwa ujumla nchini. Naandaa makala ndefu kuelezea kwa kina tatizo hili. 0716540363.

TFF waache kujali Dar es Salaam tu. Michuano kama hii ifanyike hata mikoani kama Mara (Musoma), Lindi ili kuhamasisha wachezaji. Pia wajali wachezaji wakiumia wakiwa kwenye timu ya taifa kama ilivyo kwa Victor Costa. 0756949971.

Pale TFF hakuna sera madhubuti ya kuendeleza soka Tanzania. Vijana hawaendelezwi, mpira kwao hauna maslahi, lakini uliza TFF ya jana na leo ina vitegauchumi vingapi? Ndiyo maana wanagombea nafasi za uongozi wa kisiasa huku wanaocheza mpira wakiwa na maisha magumu.

Kwa kweli ni vigumu soka letu kuendelea. Labda Leodegar Tenga atuachie TFF yetu na soka letu, amekaa miaka mingi inatosha. 0714696814.

Tatizo linaanzia TFF, hawazijali klabu ndogo za mitaani. Wanashindwa hata kwenda viwanja vya mchangani na mitaani kuangalia vipaji na kama utafuatilia vizuri utaona hata mashindano ya Copa Coca Cola yanapoteza mvuto mwaka hadi mwaka kwa sababu fedha nyingi zinawekwa kwenye posho na mambo mengine ya utawala badala ya kuzijali klabu zinazotoa wachezaji. 0786458545.

Tuwe kama wenzetu, tuwe na timu za vijana kimaeneo tuondokane na u–Simba na u-Yanga na timu hizo ziwe na shule za soka ndipo tutafika mbali. Watanzania tushauriane tufanye maamuzi magumu, tuzifute au tuzivunje klabu za Simba na Yanga kwa manufaa ya soka la Tanzania. 0787101066.

Hivi mwandishi kweli kabisa unaamini TFF hii ambayo imeshindwa hata kuweka namba kwenye viti kwenye Uwanja wa Taifa itatufikisha mbali? Matokeo yake ni uharibifu wa uwanja, mapato kutoeleweka kwa usahihi na kupotea ladha ya utazamaji. 0717114777.

Tujifunze kwa wenzetu Mexixo ambako inafanya vizuri sasa. Nchi hiyo ina wachezaji wenye umri mdogo kwa sababu nchi imeamua kuwekeza katika soka kwa vitendo. 0718085308.

Michezo Tanzania imetawaliwa na siasa. Timu ikishinda huitwa bungeni kupongezwa, isiposhinda lawama kibao kwa timu. Kwa mtindo huu hatuwezi kufika mbali, tuache siasa kama tunataka kufanya vizuri. 0713535493.

Jimmy David Ngonya, kiongozi wa muda mrefu katika klabu ya Simba ya Dar es Salaam, anasema matatizo yako katika mfumo wa uongozi wa soka.

Kwanza anasema haoni sababu ya kuwepo vyama vya soka vya mikoa na wilaya, badala yake zianzishwe kamati za kusimamia ligi. “Umewahi kusikia vyama vya soka vya mikoa Ulaya?” anahoji.

Pili anasema haoni kwa nini uwekwe msisitizo kwa wasomi tu kuongoza soka. Katiba ya TFF inataka klabu wanachama wake ziongozwe na watu wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne, lakini Ngonya anasema kuwa uongozi ni kipaji si vyeti.

Tatu anashangaa kuona wagombea uongozi katika TFF wanalazimika kulipia fomu kiasi cha Sh. 300,000 lakini katibu mkuu ambaye kimsingi ni mwajiriwa halipi hata senti. Tujadili.

0789 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: