Amos Wako alivyoshupalia kuishitaki Marekani

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali ya Kenya, Amos Wako ameingia katika mvutano mkali na serikali ya Marekani. Chimbuko la mvutano huo ni hatua ya Marekani kumnyima viza ya kuingilia Marekani.
Marekani inamtuhumu Wako, anayeshikilia wadhifa huo kwa miaka 18 sasa tangu wakati Kenya ikiongozwa na Chama cha KANU chini ya rais Daniel arap Moi, kwamba anahusika na mipango ya kukwamisha mageuzi ya kisiasa na kiuchumi baada ya kuundwa kwa serikali ya umoja.
Uamuzi wa Wako kukataliwa kuingia Marekani umemkasirisha mwanasheria huyo na kutishia kuifungulia mashitaka Marekani akiupinga.
Marekani inamuona Wako kama kiongozi mwandamizi katika serikali aliyeshindwa kuwajibika ipasavyo na majukumu yake likiwemo la kushindwa kuchukua hatua madhubuti kudhibiti ufisadi.
Katika kukomesha utamaduni wa wakosaji kuvumiliwa na serikali katika nchi ambayo ufisadi ni kama jambo la kawaida, jumuiya ya kimataifa inachukulia hatua kama ya kuzuilia usafiri wa Ulaya na Marekani kwa viongozi waandamizi, ni uamuzi muhimu ili kuepusha kujirudia kwa matukio ya ghasia baada ya uchaguzi ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,300 mwaka jana.
Kenya ambayo itafanya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge mwaka 2012, ilikumbwa na machafuko baada ya uchaguzi wa Desemba 2007 ambapo kundi lililoongozwa na Raila Odinga anayetumikia uwaziri mkuu katika serikali ya umoja, lilipinga matokeo ya ushindi wa Mwai Kibaki.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Johnnie Carson ndiye aliyetangaza uamuzi wa kumzuia Wako kuingia Marekani na akasema hatua kama hiyo itachukuliwa kwa viongozi wengine watatu waandamizi wa serikali. Hakuwataja.
Lakini Balozi wa Marekani nchini Kenya, Michael Ranneberger alitoboa siri hiyo kwa kumtaja Wako kama mmoja wa viongozi hao waandamizi wanaokabiliwa na marufuku ya kuingia Marekani kwa kukwamisha mageuzi ya kiutawala.
Wako analaumiwa kwa kuchelea kushitaki wahusika wa mauaji ya ghasia za uchaguzi na kwamba anaonea muhali viongozi waandamizi serikalini wanaotuhumiwa kutajirika kwa kula rushwa katika miradi inayogharimu nchi mabilioni ya fedha.
Wako ambaye alizaliwa 31 Julai mwaka 1945, amekuwa mwanasheria mkuu wa Kenya tangu Mei 1991. Alihitimu Shahada ya Sayansi katika uchumi kwenye Chuo Kikuu cha London, Uingereza.
Pia ana Shahada ya Sheria aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania na Shahada ya Pili ya Sheria kwenye Chuo Kikuu cha London.
Wako amefanya kazi katika mashirika mbalimbali ya kitaaluma ikiwemo wadhifa wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Afrika (ABA) kutoka mwaka 1978 hadi 1980. Aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Wanasheria wa Afrika na ni mwanachama wa Bodi ya Wanasheria ya Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya.
Wako aliteuliwa tena Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Kenya baada ya kuondoka utawala wa Moi na kuingia kwa Kibaki. Amekuwa akishughulikia ufisadi uliohusisha fedha nyingi katika historia ya nchi hiyo ulioitwa kama “Kashfa ya Goldenberg.”
Suala hilo limechukua muda mwingi wa utumishi wa Wako kama mwanasheria mkuu wa serikali. Hata hivyo, hatua dhidi ya wahusika hazijachukuliwa sawasawa.
Uamuzi wa Marekani kumtaja kama viongozi wanaokwamisha mageuzi nchini Kenya, umemleta Wako hadharani na kushuhudiwa akitoa matamshi makali dhidi ya Marekani.
Mashitaka anayokusudia kuifungulia serikali ya Marekani yanahusu madai yake kwamba amedhalilishwa kutokana na uamuzi wa kuzuiwa kuingia Marekani chini ya tuhuma za kuhusika kukwamisha mageuzi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari wiki iliyopita, Wako alitoa maelezo ya kutetea hadhi yake na nafasi yake kama mwanasheria mkuu wa Kenya.
"Mwanasheria Mkuu hajahusika kwa namna yoyote ile na ukwamishaji wa mageuzi," amesema mbele ya waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.
Akaongeza, "Nachukulia uamuzi wa Marekani wa kumlenga mwanasheria mkuu peke yake kama ni ajenda ya Marekani au ya Magharibi.”
Shirika moja la habari la kimagharibi limemtaja Wako kama “Mtu mwenye mambo mengi amabye amepata kudumu kwenye nafasi yake licha ya shutuma mbalimbali pamoja na kushinikizwa kujiuzulu na mashirika yasiyo ya kiserikali.”
Wako anaonekana kuwa mzito katika kushughulikia wanasiasa na watendaji wa taasisi za umma waliohusika na kupora fedha za serikali.
Akionyesha kutamba kwa kukataa shinikozo za kutakiwa ajiuzulu, Wako alieleza waandishi wa habari kuwa hana kusudio la kwenda Marekani na kwa hivyo uamuzi wa kumzuia hauna maana yoyote.
Awali, maofisa waandamizi wa Marekani walitangaza kuwapiga marufuku viongozi waandamizi wa Kenya kwenda Marekani lakini hawakutaja jina la Wako.
Walisema tu kwamba mmoja wa wahusika hao “anakwamisha mageuzi, ameshindwa kukomesha utamaduni wa kuvumilia maovu na hajadhibiti ufisadi.”
Serikali ya Marekani pia imetuma barua kwa maofisa wengine kadhaa wa Kenya na kuwaonya kuwa wataipata iwapo matendo yao yatathibitika kuzorotesha mageuzi.
Wako anaungana na Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Jakoyo Midiwo, Waziri wa Sheria Mutula Kilonzo na Johnstone Muthama ambaye ni mbunge ambao viza zao za kuingilia Marekani zimefutwa.
Mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakilalamika kwa kutochukuliwa hatua watu waliohusika na mauaji baada ya uchaguzi. Hata wafuatiliaji wa upatanishi wameitaka serikali kushitaki wahusika lakini serikali imegoma licha ya ahadi nyingi.
Julai mwaka huu, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan alitoa orodha ya watuhumiwa wa kuchochea mauaji hayo na kukabidhi kwa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC).
Orodha hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Uchunguzi ikishirikisha majaji, haijatolewa hadharani tangu ilipokabidhiwa kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC, Luis Moreno-Ocampo.
Lakini mahakama hiyo imeahidi kushitaki wahusika wote na kuomba serikali itoe ushirikiano.