Anayejua kinachoendelea serikalini atuambie


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

TAFADHALI. Kuna mtu anayefahamu kinachoendelea sasa serikalini? Kama yupo naomba atuambie.

Nimeanza makala haya kwa swali kwa sababu inaelekea wakubwa wanaotutawala hata wao wenyewe hawajui kinachoendelea katika ofisi zao. Mkubwa hajui mdogo anafanya nini na mdogo hajui bosi wake anafanya nini!

Fuatilia picha ifuatayo. Awali tulitangaziwa na Spika wa Bunge letu tukufu, Anne Makinda kwamba posho za wabunge zimeongezwa mara tatu kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 kwa sababu ya kupanda gharama za maisha huko Dodoma.

Baadaye, Katibu wa Bunge ambaye ndiye mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dk. Thomas Kashilila akasema bila kusita kuwa posho za wabunge hazijapanda na haziwezi kupanda bila kibali cha maandishi cha Rais wa Jamhuri.

Wambea wakamfuata Spika: “Enhe mama vipi mbona yule dogo anasema posho haziwezi kutolewa mpaka bwana mkubwa atoe kibali cha maandishi?” Hapo ndipo yakatolewa maelezo kuwa posho zenyewe ziliishaanza kulipwa kitambo!

Sasa hapo nani anasema ukweli na nani anadanganya? Wote Spika Makinda na Dk. Kashilila ni wakubwa wanaowajibika kila mmoja kwa nafasi yake. Lakini kila mmoja anatoa kauli tofauti kuhusu suala moja nyeti linalopaswa kuwa na jibu moja tu.

Wakati Watanzania wakitafakari vioja vya Bunge kugundua kuwa maisha yamepanda sana Dodoma kuliko Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Mtwara na hivyo kujipandishia na kuanza kujilipa posho mara tatu ya hapo awali yaani kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 likazuka hili la posho za madaktari.

Tukatangaziwa kuwa madaktari wanafunzi ambao hawapati mishahara bali wao hupata posho hawajalipwa posho kwa miezi miwili mizima na kwamba sasa huu ni mwezi wa tatu bila posho. Bila mishahara maana hawastahili mishahara na bila makazi kwa sababu wao hawapewi nyumba za kukaa!

Madaktatari wanatembea kwa mguu kwenda Muhimbili, wanawakopa baba na mama wenye nyumba wao kwa miezi miwili mizima na sasa ni mwezi wa tatu wanaendelea kukopa hata kwa mama nitilie wanakokula! Ama kweli ukistaajabu ya Musa utakumbana na ya Firauni!

Kugoma kwao kukawa nongwa. Serikali ikawahamishia wizarani na vitisho juu. Jambo hili likatafsiriwa kuwa ni adhabu kwa watu ambao wanadai haki yao ambayo bila hiyo haki ya posho (soma mshahara) madaktari hawawezi kuishi.

Ndipo hapo sasa madaktari wengine wakaingia kwenye mgomo maana ikaonekana wadogo wao, wataalamu wenzao na wafanyakazi wenzao wananyanyaswa kwa kudai haki na hapo hapo wakaibua mgogoro baina ya serikali na wana taaluma ya afya kwa ujumla, mgogoro ambao ulikuwa umefifia kwa miaka kadhaa.

Badala ya kuwafuata madaktari na kuwasihi warejee kazini kutibu wagonjwa, viongozi wetu wakaanza kushindana kwa safari. Rais Jakaya Kikwete akapaa hadi Davos, Uswisi kwenye mkutano wa nchi zilizoendelea na zenye viwanda vingi duniani na kutoka huko ‘puruuuu’ hadi Addis Ababa kwenye kikao cha Umoja wa Afrika.

Waziri Mkuu yeye akapaa puruuu hadi Arusha na aliporejea akawa na kikao na wahariri wa vyombo vya habari nchini, ambako bila wasiwasi mtoto wa mkulima akatamka madaktari wamfuate siyo yeye aende Hoteli ya Starlight kukutana nao.

Hilo si la msingi kwani Rais au yeyote wa familia yake akiugua hupelekwa Ulaya; waziri au yeyeote wa familia yake akiugua hupelekwa India. Wana matatizo gani mpaka wapapatike kuwaona madaktari wanaogoma?

Watawala wakazidi kulikoroga. Waziri mkuu Pinda akatoa hotuba ndefu iliyojaa vitisho na ubabe wa ajabu halafu akaamrisha madaktari warejee kazini mara moja na akapiga marufuku kufanya vikao visivyokuwa na mwisho. Watu wazima wenye akili zao leo wanatishiwa nyau?

Haya sasa madaktari hawakwenda kazini na mikutanoni kwenye vikao vyao hawakwenda pia. Vitisho na ubabe havikusaidia kwani mtu mzima hatishiwi nyau!

Mbaya zaidi Pinda akajaribu kupotosha watu. Eti akaanza kuhoji, huyu kiongozi wa mgomo ni nani? Eti kumbukumbu zinaonyesha kuwa aliwahi kuongoza mgomo na akapigwa marufuku kushiriki migomo na kwamba ana mashaka kama alipata cheti kamili cha udaktari!

Serikali haikulipa posho za madaktari, haikuwathamini madaktari, walipodai haki yao wakaadhibiwa kwa kuhamishwa vituo vya kufanyia mazoezi leo wanagoma anakuja na hoja mufilisi eti kiongozi wao aliwahi kuongoza mgomo!

Haya ya Pinda yakatukumbusha Watanzania hotuba moja ya Rais Kikwete alipohutubia kuhusu vitisho vya mgomo wa wafanyakazi akamtaja kiongozi wa wafanyakazi  Nicholaus Mgaya mara saba katika hotuba yake kana kwamba tatizo lilikuwa Mgaya na siyo madai yao ya mishahara.

Hilo tuliache na turejee kwenye posho za wabunge. Akazuka Pinda sasa katika kubadilisha mada maana ya madaktari imekifu, akadai safari hii eti Rais kabariki posho za wabunge zipande mara tatu maana maisha yamepanda sana Dodoma. Kesho yake ikulu ikamruka kimanga ikisema si kweli, Rais hajabariki posho hizo!

Sasa Yarabi nani anamshauri Rais wetu na ushauri gani anampa? Sawa Rais wetu hajabariki posho za wabunge, lakini anasemaje kuhusu posho hizo? Haiwezekani kuwe na malumbano baina ya Spika wake na Katibu wa Bunge lake, wote kutoka chma chake, kuhusu posho yeye mwenyekiti  amekaa kimya.

Haiwezekani kuzuke malumbano baina ya Waziri Mkuu wake na Ikulu yake kuhusu posho hizo hizo za wabunge na yeye akabaki kimya. Madaktari hawawataki waziri wake, katibu mkuu wake na mganga mkuu wake na bado rais akapata muda wa kusafiri nje na akirejea hana la kusema! Nani anamshauri Rais wetu?

Ukisoma kwenye Tovuti ya Bunge, wasifu wa Waziri wa Afya Dk. Haji Mponda unaonyesha si dakitari wa kutibu wagonjwa bali ni daktari wa Afya ya Umma inayohusika na utawala, uchumi na mazingira, hivyo hana historia ya hospitalini na kuuguza wanaoharisha na wanaotapika na hajui adha ya kuosha vidonda.

Waziri mkuu naye anatishia madaktari badala ya kuomba suluhu. Kumbukumbu zinaonyesha posho zake katika kikao cha Katibu mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo alilipwa pale pale mkutano ulipoisha lakini posho za wenzake miezi miwili hadi mitatu halipi halafu anakuwa mkali, “haraka rudini kazini na marufuku kukutana Starlight au popote!”

Nani anamshauri Waziri mkuu au hana mshauri? Nani anamshauri Rais wetu au naye hana mshauri? Lakini zaidi ni kitu gani kinaendelea serikalini maana inaelekea ofisi ya Rais ikulu, ofisi ya Bunge la Jamhuri na ofisi ya Waziri mkuu kila mtu na lwake. Nauliza, anayejua kinachoendelea kwenye ofisi hizi tatu, tafadhali atuambie !

0785788727/0718582755, kicheere@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)