Anna Richard Lupembe: Mbunge mpole anayelilia maendeleo Rukwa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

UKIKUTANA na mbunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Viti Maalum, mkoa wa Rukwa, Anna Richard Lupembe (43), utakiri kuwa hana majivuno; anajiheshimu na anaheshimu wenzake.

Hii ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni, lakini anaufahamu mkubwa, anapolinganishwa na baadhi ya wabunge, hasa wa rika lake.

Kabla ya kuingia katika kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 2005, Lupembe alikuwa mfanyakazi wa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, mjini Dar es Salaam, Lupembe anasema kilichomsukuma kujitosa katika kinyang’anyiro hicho, ni dhamira yake ya kutaka kuona “Maisha bora kwa kila Mtanzania’” yanapatikana.

Macho yake ya kwanza anayaelekeza kwao, Rukwa, na anasikitika kwamba licha ya mkoa huo kuwa pembezoni mwa nchi na kupakana na nchi jirani, umekuwa nyuma kimaendeleo.

Anasema, “Mkoa wa Rukwa hauna miuondombinu ya kutosha. Barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga, haijajengwa kwa kiwango cha lami,” pamoja na kwamba barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla. 

Umuhimu wa barabara ya Tunduma Sumbawaga ni mkubwa kiuchumi na kisiasa pia. Ni barabara hii inayounganisha nchi jirani za Zambia na Kongo. Si hivyo tu, bali ni barabara hii inayounganisha mikoa ya Mbeya, Tabora na Kigoma.

Anasema, “Kwa kweli kushindwa kujengwa kwa lami kwa barabara hili, kunachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wa mkoa wa Rukwa na ile inayopakana nayo.”

Lupembe anasema hata barabara Sumbawaga–Muze, ni muhimu ikatazamwa kwa kujengwa kwa kiwango cha lami.

Anasema barabara hii inayotoka Sumbawanga hadi Muze huko Ziwa Tanganyika na ile ya Tunduma hadi Sumbawanga, ni uti wa mgogo kwa uchumi wa wananchi wa Rukwa, lakini bado hazijaangaliwa vya kutosha.

Jingine linalosumbua kichwa cha Lupembe ni tatizo la maji na umeme hasa katika wilaya ya Nkasi. 

“Nkasi hakuna umeme, hakuna maji. Ni muhimu serikali ikafika mahali ikaliangalia suala hili kwa mapana yake,” anasisitiza.

Mkoa wa Rukwa una majimbo tisa ya uchaguzi. Kati ya majimbo hayo, majimbo manane yanawakilishwa na wabunge kutoka CCM na moja linawakilishwa na mbunge wa upinzani, Said Amour Arfi (Mpanda Kati) wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hata hivyo, Lupembe anasema pamoja na kwamba jimbo hilo limeshikiliwa na mbunge wa Chadema, wabunge wote mkoani wanapeana ushirikiano wa kutosha linapofika suala la kujadili maendeleo ya mkoa wao.

Anasema ikifika hapo, wabunge wote wa mkoa wa Rukwa, akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huweka kando itikadi za vyama vyao.

Anasema, “Katika kutafuta maendeleo, sisi sote tunaweka kando itikadi za vyama vyetu na kutanguliza mbele maslahi ya wananchi. Mheshimiwa Arfi anatoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na watendaji serikalini.”

Anasema, “Anahudhuria vikao vya Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda na anapitisha bajeti ya maendeleo. Haijawahi kutokea hata mara moja, Arfi akakwamisha bajeti ya maendeleo kwa maslahi yake binafsi.”  

Hata hivyo, Lupembe anasema pamoja na ushirikiano huo unaotolewa na Arfi, dhamira ya chama chake ni kuhakikisha kwamba jimbo la Mpanda Kati linachukuliwa na CCM katika uchaguzi ujao.

“Kwa kweli hili limetutia doa kubwa sana. Haijawahi kutokea tangu mfumo wa vyama vingi uanze, kwamba jimbo la mkoa wa Rukwa lishikiliwe na mbunge wa upinzani. Kwa kweli inatuuma tena sana. Lakini tunajipanga kulirudisha,” anasema.

Akizungumzia miradi ya maendeleo, hasa shule za msingi na sekondari, Lupembe anasema mkoa wa Rukwa umepiga hatua kubwa katika ujenzi wa shule, ingawa bado nguvu inahitajika katika kuzifanya shule hizo kuwa za kisasa.

Anasema kila kata ya mkoa wa Sumbawanga ina shule ya Sekondari, lakini tatizo kubwa lililopo ni vifaa vya kufundishia pamoja na madawati na mabweni.  

Anasema kutokana na hali hiyo, kila mwananchi wa mkoa wa Rukwa ana wajibu wa kuchangia alichonacho ili kuhakikisha shule hizo zinatimiza mahitaji yake kwa wanafunzi.

Tayari yeye Lupembe kwa msaada aliopewa na Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF) ametoa vitanda 50 kwa shule za sekondari za Milanzi na Msanzi.

Si hivyo tu, bali pia kwa msaada wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ametoa mabati 100 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya wasichana katika shule ya Sekondari Ntendo iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga.

Lupembe ni mbunge wa Viti Maalum wa mkoa na hivyo anajibika katika mkoa wote, tofauti na wabunge wenzake wa majimbo. Je, anafanyaje kazi zake zake?

Anasema, “Nafanya kazi katika mazingira magumu. Mkoa wa Rukwa ni mkubwa sana. Nami nikiwa mbunge wa viti maalum nalazimika kupitia kila wilaya kukutana na wananchi, hasa wanawake wenzangu,” anasema.

Anna Richard Lupembe alizaliwa 26 Aprili 1966 mkoani Iringa, akiwa mtoto wa mwisho kati ya 11 wa Richard Lupembe na Talika Mkusa.

Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya msingi Chemichemi kati ya mwaka 1973 hadi 1979. Mwaka 1980 alijiunga na shule ya Sekondari Namfua alihitimu masomo yake hayo mwaka 1983.

Mwaka 1990 alijiunga na Chuo cha Benki cha Amon Nsekela, Iringa kwa masomo ya kozi za benki. Alimaliza masomo yake hayo mwaka 1991.
Baada ya kumaliza masomo yake hayo, Lupembe aliajiriwa na Benk ya Taifa ya Biashara (NBC) kama katibu muhtasi. Alifanya kazi katika idara hiyo kutoka mwaka 1987 hadi 1997. 

Mwaka 1997 alipandishwa na kuwa karani wa fedha wa iliyokuja kuitwa NBC Bank 1997. Alidumu hapo hadi mwaka 2001.  Ameshika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya na nje ya chama chake.

Lupembea katika kuhimiza maendeleo hasa kwa wanawake, hatafuni maneno. Anasema ni vema wanawake wakajielekeza katika kilimo hasa mpunga na mahindi ambayo hustawi katika mkoa wa Rukwa.

Katika hili la maendeleo, Lupembe tayari amefungua chama cha kuweka na kukopa (SACOS) katika wilaya tatu za mkoa huo, lengo likiwa kufungua Saccos moja kila wilaya.

Kwa sasa, Saccos hizo zimefunguliwa katika wilaya ya Mpanda ambayo inaitwa, Leti Saccos, Sumbawanga-Umchia Sacos na Saccosi ya wanawake ya Sumbawanga.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: