Anthony Mtaka na ajenda ya kuimarisha UV-CCM


Iddy Mkwama's picture

Na Iddy Mkwama - Imechapwa 12 August 2008

Printer-friendly versionSend to friend

ANTHONY John Mtaka ni miongoni mwa vijana 34 waliojitosa kuomba uteuzi wa kuwania uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.

Mtaka amekulia ndani ya chama na kuanza kukitumikia tangu utotoni akiwa chipukizi.

Anasema, "Umoja wa vijana una raslimali nyingi na unakopesheka. Hakuna sababu ya vijana kulalamikia suala la kukosa ajira wakati uwezo wa kujiajiri upo mikononi mwetu. Cha msingi ni kuwapatia fursa."

"Umoja huu haupaswi kuyumba kiuchumi kwa kuwa unaweza kujiendesha kwa kutumia raslimali zake. Tuna mashamba kwenye baadhi ya mikoa na kwingine kuna vyumba vya maduka kwa ajili ya kukodisha," anasema Mtaka ambaye ni Mwenyekiti wa CCM tawi la Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro.

Anaamini kuwa mafanikio ya umoja huu yatafikiwa iwapo raslimali zilizopo zitatumiwa vizuri; ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa benki ya vijana wa CCM au chama cha kuweka na kukopa (SACCOS).

"Tukishaanzisha taasisi ya fedha ni rahisi kujikwamua kiuchumi. Vijana watakopa na kuanzisha miradi ya maendeleo. Watendaji wengine ndani ya chama watapata mikopo kwa riba ndogo kuliko wanapokopa kwenye taasisi nyingine za fedha," anasema.

?Kama tutakuwa na fursa nyingi ndani ya chama vijana watajitokeza kuomba uanachama kwa wingi wakifuata fursa zilizopo," anasema Mtaka katika mahojiano na gazeti hili.

Anasema kwa sasa umoja huo unatakiwa kutumika kama silaha ya kuwakwamua vijana kiuchumi huku wakiendelea "kupikwa? kuwa viongozi bora na wenye maadili.

?Ukiachilia mbali umoja huu kuwa tanuri la kupika viongozi bora, utumike kama sehemu ya kuwakwamua vijana kiuchumi. Umoja wa vijana usiwe jukwaa la siasa peke yake na wala usitumike kama daraja la kupatia wanasiasa wengine sifa, kuonekana au kupata ubunge; bali uwe sehemu ya kuongeza fursa kwa vijana,? anasema Mtaka anaamini katika umuhimu wa umoja kujengea vijana fursa za kujitegemea kama njia pekee ya kuwaondolea mawazo ya kuitegemea serikali kama mwajiri mkuu.

Hata suala la kuanzishwa kwa idara ya mambo ya nje ya umoja huo linaweza kufanikiwa iwapo kutakuwa na uchumi imara.

'Tuboreshe uchumi wetu kwanza' tukifanikiwa ndio itakuwa rahisi kuongeza idara ya mambo ya nje. Tukiianzisha kwa wakati huu tukiwa hatuna uchumi imara, itakuwa mzigo kwetu."

Anasema hakuna sababu ya kuwa na idara, halafu ikatokea safari ya kwenda kushiriki kongamano Uganda au Kenya na mwakilishi akakosa hata nauli ya kumpeleka huko.

Anasisitizia kwamba UV-CCM haupaswi kubweteka hasa ikizingatiwa mwelekeo wa kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa (BAVITA).

Anasema pasipokuwa na mipango thabiti, umoja huu unaweza kupoteza umaarufu na hata kufa.

"Chukulia mfano kulipoanzishwa TAMWA na taasisi nyingine za wanawake. Ni ukweli usiofichika kwamba taasisi hizi zinawasaidia sana wanawake na kasi yao kwa kiasi kikubwa imechangia kuiyumbisha UWT," anasema Mtaka.

Katika hili anasema sharti watumie muda huu kujiimarisha kabla ya kuanzishwa kwa baraza hili.

"BAVITA ikianza na ikiwa na nguvu inaweza kuiyumbisha UV-CCM na hata kuiua kabisa," anasema.

Kuyumba kwa umoja huo, anasema, kutasababisha hata CCM nayo kuyumba kwani chama hicho kinategemea sana nguvu za jumuiya zake ukiwemo Umoja wa Vijana.

Anasema akichaguliwa atahakikisha anashirikiana na wenzake kuleta mabadiliko ndani ya UV-CCM na kuifanya iwe imara.

Anakusudia kuongeza idadi ya wanachama wa UV-CCM kwa kuhakikisha kuwa nusu ya wanachama wanaojiunga na CCM katika mkoa, wawe ni vijana.

Anasema amebaini asilimia kubwa ya vijana nchini si wanachama wa chama chochote cha siasa,`hivyo kama kutakuwa na fursa ndani ya CCM, vijana wote hao wanaweza kujiunga na chama hicho. Mtaka alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa UV-CM tawi la Mzumbe mwaka 2007 alikuta wanachama 400. Leo kuna wanachama wapatao 8,000.

Pia alijenga ushawishi kwa wanachama wa chuo hicho kugombea nafasi mbalimbali katika ndani ya mkoa na taifa kwa kuwajengea moyo wa kujiamini na kuthubutu.

Mtaka ansema hana wasiwasi katika kuingia kwenye uchaguzi kwa kuwa ana mtaji wa kutosha kutokana na shughuli alizozifanya tangu akiwa shule ya msingi hadi sasa.

?Historia yangu inanipa matumaini ya kushinda; sina wasiwasi kutokana na shughuli nilizozifanya ndani ya chama tangu mwaka 1996 nikiwa chipukizi wa chama,? anaeleza Mtaka.

Anasema yuko karibu na vijana katika mikoa mingi nchini kutokana na kushiriki katika kukimbiza mwenge.

"Najua vijana wanataka nini; najua matatizo yao na najua nifanye nini kuwasaidia. Nilifahamiana nao wakati nikiwa kiongozi wa mbio za mwenge," anasema.

Mtaka alianza kujihusisha na siasa baada ya kuvutiwa na umahiri wa viongozi wenye utumishi unaoheshimika ndani ya chama na jumuiya.

"Siasa kwangu ni zaidi ya dini. Naipenda mno. Tangu nikiwa mdogo, nilikuwa narekodi na kuigiza hotuba za viongozi mbalimbali, nilishiriki kuwavalisha skafu na hata kubeba mabango ya viongozi wakati wa kampeni kule nyumbani," anasema.

Katika kuamua kuwania uongozi wa juu katika UV-CCM, Mtaka alitaka kutimiza ndoto za siku nyingi.

"Sijakurupuka kugombea nafasi hii. Nilijipanga mahususi kwa muda mrefu. Niliamini ipo siku na sasa ndio imefika," anasema.

Mtaka alisoma sekondari kati ya mwaka 1997 na 2000 shule ya Miembeni ya wilayani Musoma. Kidato cha tano na sita alisomea sekondari ya Suji iliyopo Same, mkoani Kilimanjaro na kuhitimu mwaka 2002 alipojiunga na Chuo cha Ualimu cha Marangu kwa mafunzo ya ualimu ngazi ya stashahada.

Hata hivyo, pamoja na kuhitimu na kupata cheti hakufundisha, badala yake alikwenda kuongeza ujuzi Chuo Kikuu cha Mzumbe anakoendelea kusomea uongozi na utawala ngazi ya shahada.

Ndani ya CCM, Mtaka ni Mjumbe wa Baraza la UV-CCM Mkoa wa Mwanza, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Mvomero na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kutoka wilaya ya Musoma.

0
No votes yet