Arumeru kuchagua baina ya rushwa na haki


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

TANGU mchakato wa kura za maoni za kutafuta wagombea ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki ulipoanza, tumeyasikia mengi. Yako mazuri na mengine machafu.

Mchakato huu umehusisha vyama viwili vikubwa vya siasa – Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachotaka kutetea kiti, na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinachotaka kudondosha CCM.

Aliyepitishwa na CCM ni Siyoi Sumari, mtoto wa marehemu Jeremiah Sumari, mbunge aliyefariki na kuacha wazi kit icha jimbo. CHADEMA imempitisha Joshua Nassari, aliyekuwa mgombea wa chama hicho uchaguzi wa 2010 aliposhindwa na Sumari (baba).

Katika uchaguzi huo, Sumari alishinda kwa kura 34,661 na Nasari kupata kura 19,123. Waliofuata ni John Pallangyo (CUF) 265, Linda Bana (Jahazi Asilia) 176, Fanuel Pallangyo (TLP) na Charles Msuya wa UPDP waliofungana kwa kura 88.

Kwa upande wa CHADEMA, ukiacha vitimbi vya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, aliyekwenda jimboni na kudai kuwa kuelezwa na Washiri (wazee wa kimila wa Wameru) kuwa hawataki kumuona Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema katika kampeni, mambo yalikuwa shwari.

Pia baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuwa mmoja wa wagombea, ambaye baadaye aliteuliwa, Joshua Nassari, aliitisha harambee mjini Arusha kuchangisha fedha na magari ya kampeni kabla ya uteuzi rasmi.

Malalamiko haya hayakupewa uzito wowote, labda kwa sababu ilikuwa wazi kuwa fedha hizo hazikuwa kwa ajili ya kushawishi kupigiwa kura za maoni, maana pangekuwa na rushwa lisingenyamaziwa na chama au Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambayo ilifuatilia upigaji kura.

Inajengwa imani hiyo kwa sababu hata washindani wa Nassari, baada ya kura za maoni, walikaririwa wakikubaliana na mchakato mzima wa kupatikana kwa mgombea. Nassari alipata kura 808 kati ya 888 zilizopigwa.

Waliomfuata ni Anna Mghwira aliyepata kura 23, Godlove Temba (18), Rebeca Magwisha (12), Samweli Shamy (10), Yohane Kimuto (6) na Anthony Musani ambaye alitoka CCM baada ya kushindwa kura za maoni aliambulia kura nane.

Kura za CCM kutafuta mgombea wake, zilifunikwa na wingu zito la rushwa na matumizi ya pesa yaliyopitiliza. Tatizo hili limeripotiwa hadi kwenye vikao vya juu vya chama, hasa Kamati Kuu (CC) ambako mjadala ulikuwa mkali.

Hata hivyo, pamoja na kuthibitika kuwa wagombea walitumia rushwa kushawishi kura na baadhi ya wajumbe wa vikao vya juu kutajwa kuhusika kupalilia rushwa kwa wagombea waliowataka, chama hicho kiliwarudisha wagombea wawili walioongoza wapigiwe kura tena kwa kuwa hakuna kati ya waliogombea, aliyefikia nusu ya kura zote.

Ilifahamika kuwa chama hicho kilipatiwa taarifa muhimu na TAKUKURU kuhusu mwenendo wa rushwa katika zoezi la kura ya maoni. Uamuzi wa CCM kudharau, unaonyesha kwa jinsi gani chama hicho kinavyoshikamana na walarushwa. Wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alisena kiongozi anayechukia vitendo vya rushwa, lazima aonyeshe hasa kwamba haipendi rushwa.

Mara ya kwanza, tuhuma hizo zilizowahusisha wagombea karibu wote, akiwamo Siyoi aliyeteuliwa, ziliwasilishwa.  Baadhi ya wajumbe walitaka ushindi ubatilishwe na kuchukuliwa mgombea ambaye hakuwa na uchafu huo, lakini CC ikazinyamazia na kuamuru uchaguzi urudiwe kwa kigezo kwamba “hawakutimiza akidi ya kura zilizotakiwa.”

Katika uchaguzi huo wa awali, Siyoi Sumari alikuwa amepata kura 361, William Sarakikya (259), Elirehema Kaaya (205) na Elishiria Kaaya (176). Anthony Musani alipata kura 22 na Rishiankira Urio kura 11.

Taarifa za ndani ya vikao, zilisema kwamba Siyoi ndiye aliongoza kwa utoaji milungula ili kuvutia kupigiwa kura. Wakati wenzake wanne ilidaiwa walitoa kati ya Sh. 30,000 na 80,000 kwa mjumbe kutegemea na “uzito” wa mpigakura, yeye ilidaiwa kuwa alitoa kati ya Sh. 100,000 na 200,000.

Hata wakati wa uchaguzi wa marejeo, mgombea huyo alidaiwa kutumia tena fedha na baadhi ya wapambe wake kutiwa mbaroni na TAKUKURU. Bado ni yeye aliyeteuliwa kuwa mgombea.

Hadi sasa, TAKUKURU inasema kuna watu inaendelea kuwahoji kwa tuhuma hizo, lakini hili halibadili kitu kwenye chama hicho. Mambo ni kanyaga twende.

Mpashaji habari wa MwanaHALISI anasema kwa ujumla tuhuma za rushwa zimefunika vikao vyote viwili vya CC vilivyohusika na uteuzi.

Amesema, “…kuruhusu uchaguzi kurudiwa ni kukiangamiza chama chetu. Hii maana yeke ni kwamba tumeona ile rushwa ya kwanza ni ndogo; na hivyo tunataka turuhusu wakahongane zaidi.”

Katika duru hilo la pili la uchaguzi Machi Mosi, Siyoi alipata kura 761 na kumtupa mbali mpinzani wake Sarakikya aliyepata kura 361.

Mara hii tena, uteuzi wa Siyoi uliipasua CC yenye mamlaka ya juu ya uamuzi ndani ya chama hicho. Baadhi ya wajumbe walitaka atoswe na apitishwe Sarakikya kutokana na tuhuma za matumizi makubwa ya fedha wakati wa kampeni.

Inaelezwa kwamba waliosimama kidete kutaka Siyoi atoswe ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira. Lakini mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete alikataa msimamo huo, akisema “hiyo haiwezi kuathiri uchaguzi.”

Ingawa Nape amekaririwa akikanusha habari hizo za ndani, vyanzo vya habari vimemkariri akisema kuwa tuhuma za matumizi makubwa ya fedha zilizotolewa na baadhi ya watu ili mgombea huyo achaguliwe, hazikupaswa kuvumiliwa.

Mjumbe mwingine, Wassira pia alitaka Siyoi atoswe kutokana na tuhuma hizo, Kikwete, ambaye aliungwa mkono na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu), William Lukuvi, hakuwasikiliza.

Hatua ya Mwenyekiti Kikwete kudharau tuhuma za rushwa na pendekezo la wajumbe wa CC kutaka Siyoi atoswe inafunza kitu muhimu kimoja: Kwamba kumbe hata pale rushwa inapodhihirika hata na TAKUKURU, utashi wa uongozi wa juu wa serikali na CCM hupewa nafasi kuamua hatima ya watuhumiwa wa rushwa.

Kwa sababu hiyo basi, Watanzania hawana sababu ya kutoamini kauli aliyopata kuitoa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, alipohojiwa na makachero wa mtandao wa kipelelezi wa WikiLeak.

Dk. Hoseah alinukuliwa na mtandao huo akisema kuwa pamoja na jitihada za taasisi anayoongoza kuzuia rushwa, nchini Tanzania, ni vigumu tatizo hilo kudhibitiwa kwa sababu uongozi wa juu unawazuia wasichukue hatua kukomesha rushwa kubwa.

Rais Kikwete aliwaeleza wajumbe kuwa Arusha ni mkoa wenye siasa za aina yake, hivyo ni muhimu kuwa makini kwani siku za nyuma kuliwahi kuibuka tuhuma za rushwa na wabunge wa CCM kukamatwa, lakini mahakama ikawaachia huru.

Inajulikana wazi kuwa hata kesi zilizokuwa na ushahidi mzuri wa kutia hatiani watuhumiwa, zilitupwa na mahakama kwa sababu ushahidi huo haukuwasilishwa ipasavyo.

Mvutano kuhusu rushwa haukuibuka tu kwenye CC, ulianzia Sekretarieti yake inayoongozwa na Katibu Mkuu, Wilson Mukama.

Vyombo vya habari vimemkariri Mukama akiwanyooshea vidole wajumbe waliokuwa wakitaka Siyoi atemwe, akitoa maelezo dhaifu kwa wajumbe wa sekretarieti hiyo kwamba miongoni mwao hakuna asiyekuwa na kambi yake.

“Kila mjumbe hapa ana kambi na zinajulikana,” alinukuliwa akiwaambia wajumbe na kuwataka kufanya uamuzi utakaokuwa na maslahi na chama chao na siyo ya kambi zao.

Hatua hiyo ilijenga picha kuwa si lazima kukubali kuchukua hatua inapobainika kuwa mchakato wa kuomba uteuzi uligubikwa na rushwa. Huko ni kufunika kombe ili mwanaharamu apite.

Tuhuma dhidi ya Siyoi na wapambe wake chini ya baba mkwe wake, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, zinakwenda mbali hadi katika matumizi ya viongozi wa kimila katika kampeni zake.

Katika hatua nyingine, ilidaiwa pia Siyoi amemtumia Mshiri Mkuu (kiongozi mkuu wa kimila wa Washiri), kumfanyia kampeni kwa kuwa yeye ni baba mdogo wake.

Hiyo ya kura za maoni inaweza kuwa ndiyo tisa, kumi ikawa ni uchaguzi wenyewe.

TAKUKURU imenyamazishwa ndani ya CCM, je, itaweza kufurukuta wakati chama kikishindana na vyama vingine, na hasa CHADEMA?

Kipenga kimepigwa ili mchezo uweze kuanza. Pale uteuzi rasmi wa wagombea utakapotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ndipo mchezo hasa utaanza.

Mchezo ambao kwa kawaida husisimua ni kampeni. Makubwa yanaweza kuonekana na ndiyo yatakayotoa taswira ya vipi wananchi wa Arumeru Mashariki watapiga kura zao siku ya uchaguzi.

Tunatarajia kuona makubwa zaidi, hasa katika matumizi ya fedha, kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Igunga, mkoani Tabora, Oktoba mwaka jana.

Katika uchaguzi huo, uliojaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya Rostam Aziz kujiuzulu, kulishuhudiwa uchafu mkubwa wa uchaguzi. Shahada za wapigakura zilinunuliwa, viongozi wa serikali kujiingiza katika kampeni na vyama kushambuliana na watu kutishiwa kwa risasi.

CHADEMA na CCM vinajivunia uadilifu wa makamanda wake wa kampeni. Wakati CCM ikimwachia jukumu hilo Katibu wa Uchumi na Mipango, Mwigulu Nchemba na kampeni kufunguliwa na Rais Msaafu, Benjamin Mkapa, CHADEMA kimeteua wabunge wawili kuwa mameneja wa kampeni yake, Mchungaji Israel Natse (Karatu) na Vincent Nyerere (Musoma Mjini).

Mkapa ambaye hajajibu waziwazi tuhuma za kukiuka maadili ya uongozi alipokuwa Ikulu, ndiye anayeonekana na CCM lulu katika wakati ambao wengi wa viongozi waandamizi wanajinasibisha na makundi ndani ya chama.

Sasa, katika mazingira hayo, wananchi wa Arumeru Mashariki watarajie kitu gani? Ushindani mkali; vikumbo, vituko na vitisho. Kitu kibaya kinachoweza kutokea ni msimamizi wa uchaguzi kutangaza mshindi mgombea aliyeteuliwa kwa nguvu ya pesa. Hilo likitokea, nini itakuwa hitimisho la kinyang’anyiro hicho ? Ni kudumisha utamaduni wa kuruhusu rushwa kuipiku haki.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)