Arumeru Mashariki waonyesha njia


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

HATIMAYE uchaguzi mdogo jimbo la Arumeru Mashariki na uchaguzi mdogo kata za Kirumba, Kiwira na Lizaboni umekamilika kwa wananchi kufanya uchaguzi sahihi bila kujali vitisho na kebehi za chama tawala.

Kushindwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulionekana mapema. Kampeni zilianza kwa rais mstaafu Benjamin Mkapa kudhalilisha familia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa kudai Vincent Nyerere siyo mwanafamilia ya Nyerere.

Vincent hakuwa mgombea wa jimbo la Arumeru na hakuwa sehemu ya sera ya CCM ambayo Mkapa alikwenda Arumeru kuinadi. Kwa hili, Mkapa alitumika kuonyesha kufilisika kwa CCM.

Kushindwa kulionekana pia katika vituko vya makada wa CCM katika maeneo mbalimbali ya jimbo.

Mwigulu Nchemba, katibu wa uchumi na fedha wa CCM, alidaiwa mapema, kutembea na fuko la fedha za kugawia watu anaowajua na asiowajua.

Alipojaribu kukana tuhuma hizo, ndipo zikaibuka kubwa zaidi; kwamba alifikia hatua ya kuwagawia fedha maaskofu na wachungaji.

Itachukua muda mrefu kwake kuondoa wingu hilo; lakini itachukua muda mrefu pia kwa baadhi ya watu kuamini kuwa CCM na serikali yake wana nia ya kweli ya kuondoa rushwa katika nchi.

Baadhi ya wananchi niliokutana nao katika harakati za kampeni waliniambia walikuwa wanahudhuria mikutano ya CCM na kupokea fedha; kisha wanaenda kuchanga fedha hizohizo kwenye mikutano ya CHADEMA.

Wakati wa kampeni, CHADEMA ilikuwa inaendesha michango ya wazi. Vijana wengi na watu wa kipato cha chini waliichangia CHADEMA kwa hiari yao.

Aidha, kushindwa kwa CCM kulionekana pia kwa makada wake, Stephen Wassira, Nchemba na Livingstone Lusinde kuendeleza mashambulizi kwa Vincent na kudai pia kuwa watu wa Arumeru hawahitaji taarifa za Nyerere ili kuondokana na shida zao za kila siku.

Maneno haya yangesemwa na wanasiasa kutoka vyama vingine nisingekuwa na hoja ya kuyazungumzia; lakini kwa kuwa yamesemwa na wana-CCM, nalazimika kupaza sauti.

Nadhani watu wa Arumeru wanahitaji fikra na taarifa za Baba wa Taifa ili angalau waone kama wanaweza kupata ufumbuzi wa matatizo yao.

Hii ni kwa kuwa CCM ya Nyerere iliondoka na hamasa ya wananchi kujiletea maendeleo yao wenyewe; nafasi yake ikachukuliwa na CCM inayodai kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuuza maliasili zao.

Wananchi wa Arumeru wamenyang’anywa ardhi yao, maji yao, na utu wao kwa kisingizio cha kuwapa wawekezaji ili wawaletee wananchi maendeleo.

Kwa hiyo, makada wa CCM wanapodai Nyerere hawezi kuwasaidia wananchi wa Arumeru, kimsingi wako sahihi, kwani kwa CCM hii ya sasa, Nyerere ni kikwazo na adui wake mkubwa.

Jitihada nyingi zimefanyika kuhakikisha fikra za Baba wa Taifa zinazimwa na watu wote wenye fikra za namna yake wanaonekana magaidi katika taifa.

Haishangazi basi, na huenda kauli na tabia za makada hao na viongozi wao, ndizo zimezaa fikra na  tuhuma, kwamba CCM na viongozi wake ndio walimuua Baba wa Taifa ili awapishe waweze kuiuza nchi hii aliyohangaika kuijenga.

Kwa upande mwingine, Mwalimu Nyerere kweli alifanya kosa la kiufundi, pale alipotamka hadharani kuwa hawezi kukaa kimya wakati anaona nchi inauzwa na misingi ya utaifa wetu inapuuzwa.

Kwa kufanya hivyo, wanadai wale ambao bado wameshikilia hekima na ujasiri wake, kwamba alijichongea na “kuharakisha” kifo chake mwenyewe.

CHADEMA, kwa upande wao, wamejitokeza katika kampeni za Arumeru kama watetezi wa fikra na tunu za Mwalimu.

Kule kushirikisha wananchi kuchangia chama chao kwa mwamvuli wa M4C (Movement for Change), ni ishara ya kupeleka chama kwa wanachama na wananchi kwa vitendo.

Baba wa Taifa aliijenga TANU kwa michango ya hiari ya wananchi wa Tanzania. Msimamo wa CHADEMA wa kupinga rushwa na ufisadi ni wa kuigwa.

Katika kampeni za CCM ilikuwa kana kwamba ni marufuku kutamka neno “rushwa” au “ufisadi.” Wapigadebe walionywa na kuonyeka, kuwa wasithubutu kutamka maneno hayo maana yangekirudi chama katika kampeni hizo.

Baba wa Taifa, mpaka anakufa, alikuwa jemedari wa kupinga na kukemea rushwa ya aina yoyote. Ilifika mahali ikaonekana Mwalimu, hata alipotoka usingizini, alikuwa akikemea rushwa.

Hivi sasa chama alichokiasisi, kinaona nongwa kuzungumzia rushwa katika kampeni zake. Hata makada, kama Christopher ole Sendeka, waliojijengea sifa ya kukemea rushwa, mara hii wameonywa wakaonyeka wasitamke neno rushwa katika kampeni za Arumeru.

Wale wasioonyeka kama Samwel Sitta na Nape Nnauye walilazimika kubaki nje ya ulingo ili wasivunje mwiko jukwaani wakatamka neno “rushwa.”

Kwa upande wake, CHADEMA imeendelea kupinga rushwa, ufisadi na uuzwaji wa raslimali za taifa.  Baba wa Taifa alikuwa na msimamo wa wazi juu ya mambo haya.

CHADEMA imeanzisha harakati za kuhamasisha watu kujali tunu za taifa. Alifahamika kwa msimamo wake wa kujali taifa kuliko chama, rafiki na hata familia yake.

Sasa wanasiasa wa CCM wanahangaikia familia zao ili ziingie katika siasa na kuunda mtandao wa kifamilia katika uongozi wa nchi.

Lakini mpaka anaondoka madarakani, Baba wa Taifa hakumpigania ndugu yake yeyote kuingia katika siasa.

Hata wale aliowateua kushika madaraka katika chama na serikali, wawe wanatoka Butiama au karibu na Butiama, hawakumpora uwezo wa kuwashughulikia pale walipofanya madudu.

Badala ya Mwalimu kuogopa kuwajibisha wateule wake wa ngazi mbalimbali; wateule ndio walimwogopa kupita kiasi.

Wananchi wakazi wa Arumeru Mashariki wametumia vema nafasi yao. Wamechagua haki badala ya dhulma. Wamechagua sera badala ya matusi.

Arumeru wamelinda kura badala ya kuiba kura. Wamechangia chama badala ya kuhongwa. Wamemjibu Mkapa kuwa wao si wavivu wa kufikiri.

Wana wa Arumeru wametuma ujumbe kwa watawala kuwa hawaridhiki na jinsi mambo yanavyokwenda.

Walipigania ardhi yao mpaka Umoja wa Mataifa; lakini ardhi hiyo imeuzwa na CCM. Wameahidiwa maendeleo na CCM kwa miaka mingi, lakini hawakuyapata.

Sasa wenye haki ya kuahidi ni CHADEMA. CCM wana haki moja tu: Kueleza wamefanya nini miaka yote, siyo kuahidi, kuahidi na kuahidi.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet