ASANTE kocha wa Simba Patric Phiri. Asante kocha wa Yanga Kostadin Papic kwa kutufundishia timu zetu zikaweza kucheza mpira nzuri wa kuvutia.
Asante pia viongozi wa Simba na Yanga kwa kuweka mazingira mazuri kwa makocha hao kufanya kazi zao bila mizengwe.
Hakuna ubishi kwamba ubora wa timu ya Tanzania, Taifa Stars unatokana na ubora wa timu hizi mbili kubwa, Simba na Yanga. Timu hizi zikiwa bora na timu ya taifa itakuwa bora. Zikidorora, Stars nayo itadorora.
Ushahidi umeonekana wiki iliyopita wakati Taifa Stars ilipocheza mchezo wa kirafiki na miamba ya soka kutoka Afrika Magharibi, Ivory Coast.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Stars ilionekana bora. Ilicheza vizuri kuliko ilivyokuwa inacheza katika michezo yake iliyotangulia. Wachezaji wetu, hasa wale wanaocheza kwenye ligi yetu ya Bongo wengi wao walicheza vizuri.
Kwa mtazamo wangu, uwezo ulioonyeshwa na wachezaji wa Stars kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na ubora wa makocha wa klabu zao, hasa Simba na Yanga.
Si kwamba nabeza uwezo wa kocha wa Stars, Marcio Maximo – hapana. Nataka wapenzi wa soka waelewe kwamba, timu ya taifa haiwezi kuwa bora kama klabu zinazotoa wachezaji hazitakuwa bora.
Na katika nchi yetu, klabu zinazotoa wachezaji wengi katika timu ya taifa ni Simba na Yanga. Klabu nyingine zinachangia asilimia ndogo mno ya wachezaji.
Mfano katika mchezo dhidi ya Ivory Coast, Simba na Yanga zilitoa wachezaji kumi waliocheza uwanjani, huku timu nyingine sita zikitoa wachezaji sita tu.
Wachezaji hao kumi ni Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub, Nurdin Bakari, Abdi Kassim, Mrisho Ngassa, Jerryson Tegete na Kigi Makasi waliotoka Yanga, huku Simba ikiwatoa Juma Jabu, Kelvin Yondani na Mussa Hassan Mgosi.
Timu nyingine zilizochangia wachezaji sita ni pamoja na Azam FC iliyomtoa John Boko, Moro United ilichangia Stephano Mwasikana Mtibwa Sugar iliyomtoa Abdulhamid Humud, ambaye kama ningeambiwa nichague mchezaji bora wa mechi ile nisingekuwa na kigugumizi kumchagua.
Wachezaji wengine watatu wanacheza nje ya nchi, ambao ni kipa Mwarami Mohammed anayecheza Ferroviaro de Nampula (Reli ya Nampula) Msumbiji, viungo Henry Joseph anayecheza Kongsvinger ya Norway na Nizar Khalfan anayecheza Vancouver Whitecaps ya Canada.
Kwa aliyekuwa uwanjani aliona jinsi wachezaji wetu wanaocheza mpira wa kulipwa nje ya nchi walivyochemsha. Henry Joseph na Nizar Khalfan hawakuonyesha utofauti kati yao na wachezaji wanaocheza ligi ya ndani.
Ukizifuatilia Simba na Yanga uwanjani hivi sasa utaona zinavyocheza mpira wa kufundishwa. Wachezaji wanamiliki mpira. Wanatoa pasi zinazofika kwa mlengwa. Goli linatafutwa kwa mipango. Yote hii ni kazi ya Phiri na Papic. Hongera.
Miezi mitatu tu tangu aishike Yanga, Papic ameibadilisha sana timu hiyo. Aliyeiona Yanga ikicheza chini ya kocha aliyemaliza mkataba wake, Dusan Kondic atakubaliana nami akiiona leo inavyocheza.
Hakukuwa na soka lolote la kufundishwa lilikokuwa likichezwa na Yanga chini ya Kondic. Kila mchezaji alikuwa anacheza kutokana na kipaji chake. Lakini Yanga ya leo inacheza kandanda safi kama ilivyo kwa Simba.
Matunda ya Papic na Phiri yameonekana kwenye Stars ya Maximo. Ingawa Stars ilifungwa na mastaa hao wa Ivory waliotapakaa kila kona ya dunia, lakini wapenzi wa soka waliofika uwanjani walitoka wakiwa wamepata burudani ya kutosha na “roho zao zilikuwa kwatu.”
Naamini kama Papic na Phiri watabaki kwenye klabu zao kwa muda wa miaka miwili ijayo, basi sitashangaa kuiona Tanzania ikishiriki michuano ya Afrika kama hii iliyoanza mwishoni mwa wiki huko Angola.
Na kama wataendelea kuwepo mpaka msimu ujao tu wa ligi na watapewa ushirikiano na viongozi wa klabu zao kama wanavyopewa sasa, hakuna timu yoyote itakayoizuia Stars isinyakue ubingwa wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, bila kujali inafundishwa na kocha gani.
Wapenzi wa soka waelewe kwamba, kutokana na mfumo wetu wa soka Simba na Yanga zina mchango mkubwa kwenye timu ya taifa.
Kama timu hizi mbili zisipokuwa na timu bora, tusitegemee Stars kuwa bora hata kama itafundishwa na Wenger wa Arsenal au Ferguson wa Manchester United.
Vinginevyo tuwe na wachezaji wengi zaidi wanaocheza mpira wa kulipwa Ulaya na nchi nyingine zilizopiga hatua kubwa katika soka.
Kuna mifano mingi ya Simba na Yanga zinapokuwa na timu bora na Taifa Stars nayo inakuwa bora. Nani anasahau Stars ya Mziray iliyochukua ubingwa wa nchi za Afrika Mashariki na Kati mwaka 1994.
Jeuri ya Mziray ilitokana na ubora wa vikosi vya Simba na Yanga vya mwaka 1993. Utaalamu wake ulichangia sehemu ndogo tu ya mafanikio ya Stars.
Kwa waliosahau nawakumbusha; Simba ya mwaka huo ndiyo iliyofika fainali ya kombe la CAF. Ilifungwa kwa “mizengwe” na Stella ya Abidjan Ivory Coast kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya suruhu ya 0-0 huko Ivory Coast, Simba ikiwa chini ya kocha Abdalla Kibaden ilikubali kulala mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Dar es Salaam. Mabao ya washindi yakifungwa na Bolizozo.
Kibaden aliitengeneza Simba kiushindani hasa, mpaka alipopokewa na Drankan Popadic mwaka 1994. Ingawa naye hakudumu sana baada ya “wenye sauti” ndani ya Simba, George Masatu, Mustapha Hoza, Hussein Masha na Mohammed Mwameja kumjengea majungu.
Yanga ya 1993 ikiwa chini ya kocha Nzoyisaba Tauzany ndiyo iliyochukua ubingwa wa klabu za Afrika Mashariki na Kati, katika fainali zilizofanyika Kampala, Uganda.
Baadhi ya nyota wake wa wakati ule ni pamoja na Steven Names, Suleiman Mkati, Kenneth Mkapa, Salum Kabunda ‘Ninja’, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, Ally Yussuf ‘Tigana’, Sekilojo Chambua, Said Mwamba, na Edibily Lunyamila.
Fikiria kombaini hiyo ya Simba na Yanga iunde Stars, kisha ipate makocha wazuri kama Popadic na Tauzany. Kwanini Mziray asipate jeuri?
Asante Phiri, Papic
