Asasi ya CORDS rafiki wa jamii


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly versionSend to friend

NI rafiki. Ni mwalimu. Ni asasi ambayo imefanikiwa kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi kupitia utafiti na huduma. Ni Shirika la Utafiti, Maendeleo na Huduma kwa Jamii au kama walivyosajiliwa, Community Research and Development Services (CORDS).

Wananchi katika mikoa ya Arusha, wilaya za Longido, Monduli na Arumeru; na Manyara katika wilaya za Kiteto na Simanjiro, ndio mashahidi wa urafiki wa kweli kati yao na CORDS.

Christopher Lemoyani Mollel, Kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kimana katika halmashauri ya wilaya ya Kiteto anasema, “CORDS wametufundisha jinsi ya kuboresha ardhi katika kilimo na hifadhi ya misitu. Hili limesaidia kuvuta mvua, hivyo kuondoa hali ya ukame na kulinda vilima na vyanzo vya maji.”

Elimu ya matumizi bora ya ardhi na hifadhi ya mazingira, vimeleta ufahamu wa sheria, taratibu na kanuni za ugawaji ardhi ya kilimo; umilikaji ardhi kimila na umuhimu wa masjala ya kijiji itakayotumika kutoa na kuweka kumbukumbu za hatimiliki ya ardhi kimila.

Mollel anasema kutokana na mafunzo ya wataalamu wa CORDS, jamii imejenga misingi ya fursa sawa katika kumiliki ardhi na usawa katika madaraka na uongozi; bila ubaguzi wa kijinsia.

Awali, hasa katika jamii ya Kimaasai na baadhi ya makabila nchini, wanaume walikuwa na tabia ya kujitwalia mashamba na kisha kuyauza watakavyo bila kushirikisha wake zao.

Hivi sasa suala hilo halipo tena. Ushirikishwaji umekuwa mkubwa katika jamii na wanawake na wanaume wana haki sawa katika maamuzi juu ya ardhi.

“Wataalam wa CORDS wametusaidia kuchochea mwamko wa haki sawa kijinsia na hamasa ya ujenzi wa ofisi ya kijiji yenye masjala ya ardhi,” anaeleza Mollel na kuongeza kuwa jamii sasa imeelewa umuhimu wa kuwa na hatimiliki.

Anasema hatimiliki ya ardhi inasaidia kuombea mikopo benki na mmiliki anakuwa na uhuru wa kutumia eneo analomiliki kwa uhakika na bila usumbufu, kwani anatambuliwa na masjala katika ofisi ya kijiji na jamii yote anamoishi.

Shirika la CORDS lilianzishwa mwaka 1997. Linaendeshwa na vijana wananchi, wasomi wenye uchungu na maendeleo ya wananchi. Makao yake makuu yako mjini Arusha. Linahusika na utafiti na utoaji huduma kwa jamii za wafugaji, wawindaji, warina asali na wavuna matunda katika eneo hili.

Hadi sasa, shirika ambalo linatumia utafiti wake kuelekeza maisha kwa vitendo, lina uwakilishi katika wilaya za Longido, Monduli, Arumeru, Manyara, Kiteto na Simanjiro.

“Kutokana na mafunzo ya CORDS, kijiji kimetenga na kuweka alama mahsusi kuonyesha lipi ni eneo la kilimo, eneo la mifugo, chanzo cha maji, mapario na hifadhi ya misitu. Hili limesaidia kuondoa migogoro kati ya wafugaji na wakulima,” anaeleza Mollel.

Kupitia elimu wanayotoa wataalam, migogoro ya muda mrefu juu ya mipaka ya vijiji imetatuliwa. Kwa mfano, mgogoro wa mpaka kati ya vijiji vya Kimana na Mbigiri katika wilaya ya Kiteto umetatuliwa; alama za mpaka zimewekwa na viongozi wa serikali za vijiji wamepatanishwa.

Katika kitongoji cha Napilikunya, CORDS imetoa misaada mbalimbali ikiwemo mbuzi wa kufuga na chakula. Hapa ndipo inaishi jamii ya watu maskini – wawindaji na warina asali wanaohamahama kutafuta chakula.

Awali jamii hii ilikuwa ikitegemea zaidi mawindo na asali kwa chakula (AKIYE). Sasa imeelimika na kubadilika. Inalima na kufuga mbuzi, ng’ombe na kuku. Imeachana na kuhamahama.

Hata hivyo, kwa wengine ambao siyo AKIYE, lakini ni maskini, wamenufaika kwa kupewa mbuzi. Hivi sasa wana vipato: wanakunywa maziwa, wanakula nyama na wanapata fedha za kujikimu. Wametambua umuhimu wa kuwa na mifugo.

Shirika la CORDS limetoa mafunzo na vitendea kazi kwa mabaraza ya ardhi ya vijiji. Hivi sasa wajumbe wa mabaraza wana uwezo wa kushughulikia mashauri yaliyokuwa yakisuluhishwa mahakamani. Hili limepunguza pia malalamiko kuhusu miliki ya ardhi katika ofisi ya afisa mtendaji wa kijiji.

Shirika limetoa bure vitabu na vipeperushi vinavyohusu Sheria ya Ardhi Na. 4 na Na. 5 ya mwaka 1999. Mollel anasisitiza, “Vipato vya wanakijiji vimeongezeka; wametambua thamani ya ardhi, jinsi ya kuitumia na umuhimu wa kuwa na hatimiliki ya ardhi kimila.”

Naye Papayai Nang’utut, mwenyekiti wa kijiji cha Partimbo, wilayani Kiteto anasema tangu shirika la CORDS liingie kijini mwake, wananchi wamepata elimu juu ya sheria ya ardhi na wajumbe wa baraza la ardhi la kijiji na lile la kata, wamepewa elimu juu ya kutatua migogoro ya ardhi.

“Wanakijiji wamejua matumizi bora ya ardhi na hasa upangaji maeneo kwa shughuli mbalimbali kama vile eneo la makazi, kilimo, mifugo, hifadhi na vyanzo vya maji,” anaeleza Nang’utut.

Mwenyekiti anasema CORDS ilipeleka Mbeya, wilayani Mbozi na Handeni mkoani Tanga, baadhi ya wanakijiji, kuona maendeleo kwa waliokwisha anzisha masjala za vijiji.

Miongoni mwa mabadiliko ambayo Nang’utut anayaona sasa, ni pamoja na kuona akina mama wengi wakielewa haraka jinsi ya kumiliki ardhi kisheria na katika taratibu za kimila.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Namelock, Yohana Bakari, anasema kijiji chake kimepewa mafunzo na kushirikiana na CORDS katika mipango ya hifadhi ya mazingira, haki za ardhi, jinsi ya kupambana na UKIMWI, matumizi bora ya ardhi, umuhimu wa masjala na Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999.

Anataja mafanikio ya kijiji kutokana na ushirikiano huo kuwa ni pamoja na jamii kuelimika katika nyanja ya hifadhi ya mazingira;

kupata elimu juu ya umuhimu wa masjala ya kuhifadhi kumbukumbu za hatimiliki; matumizi bora ya ardhi na kupima afya ya mwili kwa hiari katika mapambano dhidi ya ukimwi.

Bakari anataja baadhi ya mahitaji ya sasa ya kijiji chake kuwa ni mafunzo kwa halmashauri ya kijiji na baraza la ardhi; mipaka ya maeneo kwa matumizi tofauti ya ardhi; uwekaji mipaka kati ya kijiji na kijiji ili kuondoa migogoro; na elimu juu ya usimamizi wa Emboley Mutangos – pori tengefu kwa ajili ya mifugo, misitu na wanyamapori.

0
No votes yet