ATCL: Reginald Mengi ameeleweka?

NI muhimu kufahamu ni kiasi gani kinahitajika kuliokoa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali, kiasi cha dola milioni 507.7 (Sh bilioni 760) kinahitajika.
Kiwango hicho ni zaidi ya mara 25 ya kilichotengwa kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji maji chini ya mpango wa “Kilimo Kwanza” katika bajeti ya mwaka huu.
Kiwango hicho kinaweza kuhudumia walau wizara ndogo ndogo nne hadi sita za serikali. Ni kiasi kikubwa sana cha fedha.
Mwaka uliopita, serikali ilitenga kiasi cha Sh bilioni moja kwa ajili ya kulisaidia shirika hilo. Kwa mahitaji ya ATC, kiasi hicho ni sawa na tone la maji ndani ya mto.
Lakini bado serikali imeonyesha nia kubwa ya kutaka kulifufua shirika hilo, hususani iwapo itapata mwekezaji wa maana kutoka nje ya nchi.
Hata hivyo, miaka nane iliyopita ATC ilipata mwekezaji kutoka nje; Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) lakini kilichotokea ni shirika la ndege Tanzania kuachwa katika hali mbaya kuliko iliyokuwapo awali.
Wiki iliyopita, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, alitoa wazo kwa serikali kwamba serikali iliwezeshe Shirika la Ndege la Precision ndilo liwe la taifa badala ya ATC.
Kwa kufanya hivyo, kwa mujibu wa Mengi, serikali ingekuwa imefanya mambo mawili kwa mpigo; lingepunguza hasara ya kuendesha ATC na pia lingetoa imani kwa wawekezaji wa ndani.
Shirika la Precision lilianzishwa na Mtanzania, Michael Shirima, na kwa serikali kuliunga mkono, picha ambayo itajitokeza ni kwamba iko tayari kusaidia wazalendo.
Ninafikiri serikali inatakiwa kulichukulia wazo hili la Mengi kwa umakini wa hali ya juu. Kuna fursa hapa ya serikali kutengeneza fedha badala ya kupoteza fedha zake ATC.
Hisa za Precision
Mwishoni mwa mwaka huu, Precision ina mpango wa kuanza kuuza hisa zake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), lengo likiwa kukusanya kiasi cha dola milioni 25 (karibu Sh. milioni 37.5).
Kama serikali itaamua kununua hisa ambazo Precision itaziuza, inawezekana ikawa na uhakika wa kupata gawio kila mwaka.
Serikali inaweza kuamua kununua walau hisa za asilimia 20 au 30 za shirika hilo na kuwa mmoja wa wamiliki. Kwa kufanya hivyo tu, Precision inaweza ikageuka kuwa shirika la taifa la ndege.
Badala ya serikali kutumia Sh. bilioni 760, na ambazo bado hazina uhakika iwapo zingetoa matunda yanayotarajiwa, inaweza kutumia kiasi kidogo zaidi na kupata faida kwa muda mrefu.
Inaweza kuamua kuunganisha utaalamu na soko la ATC ndani ya Precision kama sehemu ya makubaliano ya kununua hisa hizo. Hii itakuwa na maana kwamba baadhi ya watumishi wa ATC wataajiriwa Precision.
Serikali pia itahakikisha inalipa stahili za wafanyakazi wa ATC ambao ajira zao zitaota mbawa kwa sababu ya muunganiko wao huo na Precision.
Bila shaka, Precision nao watatakiwa kufanya maamuzi magumu dhidi ya watumishi wao wa sasa. Nina imani hakutakuwapo na athari kubwa kwa vile muungano huo wa mashirika hayo mawili utaongeza pia ukubwa wa shirika jipya.
Kama Watanzania watafahamu kwamba Precision ni shirika lao kwa maana ya hisa za serikali na za kwao binafsi walizonunua, watakuwa na kila sababu ya kutumia usafiri huo.
Wananchi watafahamu kwamba kwa kila shilingi mpya inayoingia katika makabati ya Precision, wao wanajihakikishia shilingi nyingine kama gawio wakati utakapofika.
Shirika kubwa na maarufu kuliko yote katika eneo la mashariki ya Afrika, Kenya Airways, linamilikiwa na serikali kwa asilimia 23 tu.
Asilimia nyingine zinashikiliwa na wadau wengine. Inachofanya serikali ni kushiriki katika kuhakikisha shirika linaendeshwa vizuri na wao kusubiri gawio lao tu.
Na kwa matatizo ya kiutawala yaliyoikumba ATC na ATCL, nadhani serikali yetu haina rekodi nzuri ya utawala. Itafaidika zaidi na kuwaachia wengine mambo ya biashara na yenyewe ikibaki na kazi ya kuweka mazingira mazuri ya biashara kufanyika.
Serikali, kwa kufanya hivyo, itajihakikishia kutokuingilia mambo ya uendeshaji na kujiepusha na lawama. Kwa kazi hiyo ndogo, serikali itajikuta ikiingiza fedha.
Fedha hizo ndizo zitakazotumika katika kujenga barabara nzuri na kuimarisha mawasiliano. Zitanunua madawa na madawati kwa wanafunzi.
Zile zama za kuamini kwamba shirika la taifa ni lazima limilikiwe na serikali kwa asilimia 100, huenda hazifai tena kwa sasa. Kinachotakiwa ni kufanyia kazi kile kilichopo.
Sioni dalili za ATC kuja kuwa shirika kubwa huko tuendako. Hii ni kwa sababu kuna mambo makubwa yanayohitajika kufanyika ili lirejee kileleni.
Na japo wapo ambao wangependa ATC ya zamani irejee, nafikiri itakuwa ni matumizi mabaya ya rasilimali kulazimisha jambo lisilo na tija.
Precision tayari imeshavuka vikwazo vya awali. Kwa hatua iliyopo sasa, serikali inahitaji kuwekeza kidogo tu na kupata faida; jambo linalokubalika kibiashara.
Uwekezaji katika kufufua ATC ni wa gharama na unaweza kuwa wa hasara kubwa kwa taifa. Unaweza kuchukua muda mrefu pia.
Mimi si mtaalamu wa masuala ya ndege na ninaamini serikali itachukua uamuzi ulio sahihi na wa kitaalamu. Jambo la kuzingatia hapa ni kuangalia changamoto hii iliyotolewa na Mengi.
Kama itaona kwamba wazo hilo halifai, jamii iambiwe sababu. Kama itaona ni wazo zuri, na ifanye haraka kulitekeleza. Hakuna wakati wa kuchelewa kwa vile wengine tayari wanakimbia wakati Tanzania wanatembea.