AU inasubiri hadi Kagame apinduliwe?

HALI ya mambo nchini Rwanda haipendezi. Kama vile amesahau athari za mauaji ya halaiki yaliyoibomoa nchi iliyotaliwa na Wabelgiji, rais wake, Paul Kagame amefikia hatua mbaya katika kusakama wapinzani wake wa kisiasa.
Huku akisifika kwa kufuta historia mbaya iliyokuja kwa mauaji ya kiasi cha watu milioni moja mwaka 1994, wengi wao wakiwa Wahutu, Kagame sasa anatajwa kama mkandamizaji mkubwa wa haki za kiraia.
Kwa miaka minane sasa, rais Kagame ambaye ni mwanajeshi akiongoza chama cha Rwandese Patriotic Front (RPF), amekuwa akigombana na kila anayempinga kisiasa.
Kagame, Mtutsi kiasili, alianza na Pasteur Bizimungu, mshirika wake mkubwa katika serikali iliyoundwa baada ya mauaji ya kimbari yaliyochochewa na chuki za kikabila zilizopandikizwa kwa makabila makuu mawili likiwemo la Wahutu, asili ya Bizimungu.
Kagame na Bizimungu walianza kufahamiana kama viongozi wakuu mwaka 1994 na kudumu hivyo hadi mwaka 2000 walipohitilafiana na hatimaye kutengana.
Bizimungu alikuwa rais na Kagame akawa ndiye makamu wake. Ushirika wao ulikuwa muhimu katika kuijenga upya Rwanda.
Zipo taarifa kwamba Bizimungu hakufurahishwa na baadhi ya mienendo ya Kagame ikiwamo namna alivyokuwa akiwachukulia wapinzani wao. Waligombana na mwaka 2001 Bizimungu aliachana na Kagame na kuanzisha chama chake cha PDR.
Hata hivyo, chama hicho hakikudumu kwani Kagame wakati ameshatwaa wadhifa wa urais, alikipiga marufuku kwa kudai kinachochea ukabila.
Mwaka 2002, Bizimungu alikamatwa kwa tuhuma za kuhatarisha usalama wa nchi. Hatimaye alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.
Alikuja kuachiwa mwaka 2007 kwa msamaha wa Kagame mwenyewe si mahakama. Kwa ufupi, Kagame (Mtutsi) na Bizimungu (Mhutu) walikuwa washirika hadi alipotofautiana naye.
Wachambuzi wa masuala ya siasa-jamii wanasema kwamba staili kama hiyo ya uongozi ni dalili mojawapo ya udikteta. Kiongozi wa kidikteta huwa havumilii yeyote anayeonekana kupingana naye.
Kwa asili, madikteta wanaposhika madaraka ya serikali, hutaka waonekane peke yao kama viongozi mahiri na wenye huruma kwa wananchi. Hali huwa tofauti na wanavyoieleza.
Majuzi hapa, mwanamama aliyekwishatangaza kuwa atagombea urais utakapofika uchaguzi, Victoire Ingabire, alipatwa na masahibu katika kampeni zake za kujitangaza.
Ingabire aliyekuwa anaishi uhamishoni nchini Uholanzi, akiwa katika safari za kujitangaza, msafara wake ulizuiwa na polisi kwa madai kuwa ulijumuisha madereva wasio na sifa.
Wiki chache baadaye, Ingabire alivamiwa na kupigwa na watu wasiojulikana katika ofisi za serikali. Mwenyewe amekuwa akilaumu vitendo hivyo kama mbinu za kumtishia maisha.
Wakati yote hayo yanafanyika, viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) na wale wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamenyamaza kimya.
Hawajui kwamba ule msemo wa kwamba “Usipoziba ufa utajenga ukuta” una nguvu zake licha ya kwamba ulitungwa enzi za zamani.
Inaonyesha utamaduni wa kinafiki na kuendeleza historia ya kisingizio cha kutoingilia mambo ya ndani ya taifa wakati kuna kiongozi wa taifa moja anaendesha nchi kinyume na misingi ya kidemokrasia na hivyo kutishia usalama wa wananchi.
Tangu enzi zile umoja huu ukijulikana kama Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), sifa yake kubwa ilikuwa ni viongozi kutolaani matendo mabaya yanayofanywa na viongozi wenzao katika mataifa wanachama.
Hata pale kiongozi wa taifa fulani alipokuwa ananyanyasa na kukandamiza raia anaowaongoza, viongozi wenzake walikaa kimya kwa sababu tu ya kutambua sera hiyo.
Ndio kusema kwao, maisha ya watu hayakuwa na thamani yoyote bali yale ya viongozi wenzao.
Wakati Mengistu Haile Mariam akihilikisha raia wa Ethiopia, palepale kwenye makao makuu ya umoja, viongozi wenzake walipita na kuziba masikio kama vile hawakuona kibaya chochote.
Uganda vilevile; wakati Idi Amin Dada alipokuwa akiua wananchi, Jean Bedel Bokassa akifanya kama hivyo Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), OAU ilinyamaza eti kwa kuhofia “itaingilia mambo ya ndani” ya nchi hizo.
Lakini, OAU hiyohiyo ilikuwa ya kwanza kulaani Meles Zenawi alipompindua Mengistu. Aliyelaaniwa, ni yule aliyeondoa mateso kwa wananchi – ingawa naye amewageuka kwa kuwaongoza kidikteta.
Lakini kuna unafiki mwingine. Katika zama hizi na baada ya OAU kugeuzwa AU, kumebuniwa mfumo mpya unaoendekeza udikteta Afrika.
AU sasa inakubali uchaguzi uvurugwe na chama kilichokataa kushindwa kwenye kura kishirikiane na kilichoshinda waunde serikali ya umoja wa kitaifa.
Yametokea Zimbabwe mwaka 2007 baada ya Rais Robert Mugabe kukataa kushindwa kura. Kenya nako Rais Mwai Kibaki aling’ang’ania Ikulu licha ya kushindwa uchaguzi.
Nini kama si kituko chama kilichoiba kura kuachiwa kuendelea kuongoza kwa mgongo wa serikali ya umoja?
Sasa nchini Rwanda kuna tafrani mpya. Serikali ya Kagame imetangaza kumtafuta Meja Jenerali Faustin Kayumba Nyamwassa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi kwa kumtuhumu kutenda uhaini.
Jenerali Nyamwassa si mtu mwepesi. Amepigana vita vilivyomwingiza Museveni madarakani nchini Uganda mwaka 1986.
Akapanda vyeo hadi Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Uganda (CMI), ingawa ilikuwa ikifahamika alikuwa ni Mnyarwanda.
Alikuwa sambamba na Jenerali Fred Rwigema (sasa marehemu) katika hatua za awali za mapambano ya kundi la RPF lililomng’oa madarakani Rais Juvenal Habyarimana wa Rwanda.
Ndiyo maana haikuwa ajabu wakati RPF ilipoingia madarakani Nyamwassa kuchaguliwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda.
Mpaka mapema mwaka huu, alikuwa Balozi wa Rwanda nchini India. Ingawa binafsi anakana, sasa duru za kisiasa zinamtaja Meja Jenerali Nyamwassa kama mtu makini anayeweza kugombea urais kumpinga Kagame.
Anatuhumiwa kuhusika na milipuko ya mabomu iliyotokea wiki iliyopita jijini Kigali na kuua mtu na kujeruhi wengine kadhaa.
Tayari ameondolewa ubalozini nchini India na amekimbilia Afrika Kusini. Taarifa za karibuni zinadai kuwa familia yake inashikiliwa India kwa tuhuma zinazomhsu yeye.
Pamoja na matendo yote hayo yasiyojenga, hakuna kiongozi yeyote Afrika Mashariki wala AU aliyemlaumu hadharani rais Kagame.
Amekuwa akijitahidi kudhibiti wapinzani wake kwa kisingizio kuwa wanachochea chuki za kikabila.
Ni kweli Rwanda imepiga hatua ya maendeleo katika muda mfupi wa utawala wa Kagame baada ya mauaji ya halaliki. Lakini hiyo kamwe haiwezi kuwa sababu ya rais kukandamiza wapinzani wake.
Tatizo kubwa ni pale anaposakama wapinzani wake hata bila sababu ya msingi. Ni kuchokonoa makovu ya mauaji yaliyoivunjavunja nchi.
Lazima kutambua kuwa ni vigumu sana kujenga nchi lakini ni rahisi mno kuibomoa. Cheche ndogo tu zaweza kuimaliza kwa dakika chache.
Unajiuliza, yote hayo yanayotokea nchini Rwanda hayajagonga akili za viongozi wa Afrika Mashariki? Wanadhani ni sahihi rais Kagame aangamize wapinzani wake? Kimya chao ni uzembe mkubwa na watakuja kujuta watakaposikia Rwanda imechafuka tena.
Ni wakati wa kumbana rais Kagame aache fitna za kisiasa kabla hazijazua balaa.