AU yaasisi mbinu za kulindana

VIONGOZI wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) chini ya mwenyekiti wao Jakaya Kikwete wameanzisha mbinu mpya ya kulindana ili waweze kubaki madarakani kwa muda wanaotaka.
Hii ni mbinu ya kuiba kura au kuingia madarakani kwa mabavu na kisha kuhalalisha wizi huo kwa kugawana madaraka kwa mtindo wa serikali ya mseto.
Hapa wana maana kwamba, kuanzia sasa kuiba kura na kuingia madarakani kwa staili yoyote si haramu kama ilivyokuwa inachukuliwa hapo awali.
Kwamba ukiweza kuingia madarakani kwa mtutu wa bunduki au kwa ubabe wowote ni ruksa. Ukitumia mbinu nyingine za 'kisayansi' hakuna shaka, ili mradi uwe mwepesi wa kushawishi na kuitisha mazungumzo yatakayozaa mgawano wa madaraka kwa wapinzani wakubwa.
Kabla mbinu hii kuhalalishwa kwenye mkutano wa AU uliofanyika nchini Misri wiki iliyopita, ilikuwa imetumiwa kuhalalisha utawala wa kimabavu uliomwingiza madarakani Mwai Kibaki wa Kenya.
Kibaki anaripotiwa kuiba kura. Hata baada ya mchakato wa uchaguzi kumalizika, wizi huohuo uliendelea. Anadaiwa kutumia mabavu kushinikiza mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Samuel Kivuitu ili amtangaze kuwa mshindi wakati kura zake zilikuwa hazitoshi.
Kivuitu alikaririwa na vyombo vya habari akisema alilazimishwa kutangaza kuwa Kibaki ndiye mshindi kutokana na vitisho vya rais huyo aliyekuwa anawania kipindi cha pili ikulu.
Wakati Kivuitu anakiri kutishiwa na kuwa mwoga; hatua ambayo ilisababisha kuchelewa kutangaza matokeo, shauku ya wananchi iligeuka kuwa hasira na mashaka makubwa kuwa ilikuwa njama ya kuwachagulia rais.
Kwa hiyo, hatimaye Kibaki alipotangazwa kuwa mshindi na matumaini ya waliyetarajia kushinda kuyeyuka, ukawa mwanzo wa tafrani kubwa na hata kufikia hatua ya mauaji na mapambano makubwa kati ya polisi na wafuasi wa Raila Odinga wa chama cha upinzani cha ODM.
Odinga alisikika akijitangaza kuwa ndiye mshindi na kuweka hadharani msimamo wake wa kutomtambua Rais Kibaki na hata kufikia hatua ya kuwazuia wabunge wa chama chake, ambao ni wengi kuliko wa PNU cha Kibaki, kuingia bungeni.
Mvutano ulizua vurugu kubwa hadi wasuluhishi kutoka nchi mbalimbali walipoingilia kati na kuamua kuwapatanisha mahasimu hao. Ni hapo Odinga alipokubali kumegewa nafasi ya Waziri Mkuu ambayo awali alikuwa ameikataa.
Inavyoonekana Kenya ilikuwa jaribio la kwanza la mbinu hii na baada ya kuonekana inawezekana, viongozi wa AU wameafiki na kuhalalisha njia hiyo kuwa muruwa ya kukabiliana na upinzani wa wanaoibiwa kura.
Hilo linaweza kuthibishwa na maamuzi yaliyofikiwa katika kusaka suluhu ya vurugu za uchaguzi nchini Zimbabwe kati ya Robert Mugabe na mpinzani wake Morgan Tsvangirai, kiongozi wa Movement For Democratic Change (MDC).
Mugabe aliingia madarakani kwa kuiba kura katika uchaguzi wa kwanza uliofanyika Machi 29 mwaka huu. Hata hivyo hakupata kura za kutosha.
Uchaguzi ulipoonekana batili, ukarudiwa. Hapo akafanya ujambazi mkubwa wa kisiasa; utawala wake ukaua wafuasi 70 wa MDC; ukajeruhi wengine 25,000 na kusababisha wakimbie makazi yao.
Kabla ya uchaguzi kurudiwa, Mugabe alitangaza vita. Aliibua ugomvi wake na wakulima wa kizungu. Akachochea wapigania uhuru wa zamani kwamba nchi waliyopigania ilikuwa inarudi mikononi mwa wakoloni.
Mugabe akaapa kwamba hataweza kukabidhi serikali kwa 'vibaraka wa wakoloni na mabeberu,' akiwa na maana kwamba Tsvangirai anatumiwa na Uingereza na Marekani.
Hakukomea hapo. Alisema na alituma wakuu wa polisi na jeshi la ulinzi kuongea kama wanasiasa kwa kudai kuwa 'wako tayari kurudi msituni' kama Tsvangirai atashinda.
Ni hatua hii iliyosababisha MDC kujiondoa kwenye uchaguzi, ikimwacha Mugabe kuwa mshindani wake mwenyewe – akifukuza upepo kama punguani – katika nyakati hizi za ushindani wa kisiasa wa mfumo wa vyama vingi.
Hapa ni Mugabe aliyeamua kuwa ataendelea kuwa rais wa Zimbabwe, hata kama Tsvangirai angeshiriki uchaguzi na kushinda. Kwa hali hii, Mugabe hakushinda. Amebaki ikulu kwa ubabe tu.
Sasa viongozi walioketi Sharm–El-Sheikh, wamebariki wizi aliofanya Mugabe, ingawa kuna wachache ambao walisikika wakiweka misimamo mikali ya kutaka kumtoa madarakani kwa nguvu.
Kwa hiyo uamuzi wa kutaka Mugabe akae na wapinzani wake na kufikia maafikiano kama ilivyokuwa Kenya, ni makubaliano ya kinyonge. Wana maana kwamba aliyeibiwa mali yake anagawana na mwizi kilicho chake. Hii si sahihi.
Kama hayo hayatoshi, Mugabe anaachwa atambe na kutoa kauli zake kwamba 'ameteuliwa na Mungu na wala si Waingereza,' huku akijiapiza kuwa hataachia madaraka hadi kifo.
Hata katika msimamo huo mweroro wa AU wa kutafuta kugawana madaraka kati ya mwizi na aliyeibiwa, bado Mugabe anaweka mikwara kwamba ili akae na kuzungumza, sharti mpinzani wake amtambue kuwa ni rais wake.
Je, katika mazingira haya inaweza kupatikana suluhu, angalau kama ile iliyopatikana Kenya? Rais Jakaya Kikwete amenukuliwa akisema kwamba mfumo uliotumika Kenya unaweza kuleta suluhu Zimbabwe. Je, hilo linawezekana kweli? Inaonekana kuwa ndoto.
Hapa sasa ndipo tunapobaini kwamba kumbe suala hili halikuanzia Kenya wala Zimbabwe, bali liliaasisiwa Tanzania Visiwani.
Ilikuwa ni wakati wa chaguzi za vyama vingi ambapo inadaiwa Chama cha Wananchi (CUF) ndio walikuwa washindi wa chaguzi zote ingawa walikuwa wanahujumiwa na wapinzani wao, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
CCM ambao ndio wanatuhumiwa kula njama za kuiangusha CUF, kwa sasa wapo kwenye harakati za kuwashawishi wapinzani wao kuunda serikali ya mseto baada ya kutuhumiwa kuiba kura kwenye chaguzi zote.
Nia ya CCM ni kuendelea kuwa madarakani, ikishika nafasi ya rais, huku ikitoa nafasi ya Waziri Kiongozi kwa CUF. Hapa pia kunadaiwa kutakuwepo mgawanyo wa wizara kwa pande mbili.
Na hiyo wanaamini ndio silaha tosha ya kuwadhibiti wapinzani na kuwakata makali. Kwa hili bila shaka utaratibu huu unaweza kupendwa na viongozi wa Afrika ambao wengi wao wanaonekana waziwazi kuwa na uchu wa madaraka.
Uamuzi wa AU, hata hivyo, unakinzana na hatua ambayo tayari uliishachukua. Ni AU iliyopeleka majeshi Anjwani, Comoro kung?oa kisiki – Kanali Mohammed Bakari.
Kuna maswali mengi kwa nini dawa ya Comoro isitumike Zimbabwe ambako raia wenyewe wamethibitisha, kwa kura, kwamba hawamuhitaji Mugabe.
Watawala Afrika wakubali kwamba kuna kushinda na kushindwa; lakini pia kuna kuchoka. Alipofikia Mugabe ni mchoko mtupu. Kupumzika ni halali yake; na Zimbabwe haina uhaba wa wenye uwezo wa kutawala.