Ayi, ayi, ayi, CCM

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye anatumia nguvu nyingi kutaja vibanzi katika macho ya wapinzani wake kisiasa huku akiacha boriti zikimea kwenye macho ya chama chake.
Madhara yameanza kuonekana. Kila akipuliza kibanzi kinamrukia. Amedai hawezi kuwa kiongozi wa chama cha CHADEMA kwa kuwa yeye si Mchagga. Hakujua kuwa, hiyo ilimaanisha pia yeye hawapendi Wachagga.
Nape itabidi atetee uaminifu wake ndani ya CCM baada ya kudaiwa ni msaliti kwani ni mmoja wa waasisi wa Chama cha Jamii (CCJ) akiwa ndani ya CCM.
Akifanikiwa itabidi atafute majibu ya boriti nyingine ya kushamiri koo takatifu ndani ya CCM. Wanasiasa nguli wanarithisha watoto wao nafasi ya kisiasa.
Ni kweli kwamba hiyo ni demokrasia au haki ya msingi ya kila binadamu awe mtoto wa maskini au kiongozi, lakini mbona kigezo ni kuwa mtoto wa fulani? Sifa hiyo imeanza lini ndani ya CCM? Je, itakuaje kwa asiye na sifa hiyo?
Aidha, kwa nini demokrasia ya koo takatifu haikuwepo enzi za Mwalimu Nyerere wala Ali Hassan Mwinyi? Enzi zile ilikuwepo vita kali dhidi ya watu walioajiri wafanyakazi kutoka makabila yao – ‘undugunaizesheni’.
Undugunaizesheni katika siasa haukuwepo kutokana na mfumo madhubuti wa kuchuja wagombea hadi kupata viongozi wenye sifa. Baada ya ‘mwenye nchi’ (Mwalimu) kufariki dunia na Mwinyi kuendeleza sera ya ruksa, mfumo umeharibika.
Uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM mwaka 2007 ulikuwa kama onyesho la Baba na Mwana. Kila mzazi alikuwa beneti na mwanaye.
Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inakataza kuundwa kwa tawi au kikundi chochote cha wanawake au vijana kuhusiana na chama chochote cha siasa katika maeneo yoyote ya kujisomea kama shule au vyuo, lakini mwaka 2009 CCM walikiuka sheria hiyo.
Walisimamia uchaguzi mkuu wa viongozi wa Chipukizi Taifa, ambako watoto kutoka koo takatifu waliibuka washindi.
Gabriel Makalla, mtoto wa aliyekuwa Katibu wa Fedha na Uchumi, Amos Makalla (Mbunge wa Mvomero), alichaguliwa mwenyekiti, huku Khalfan Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais Jakaya Kikwete akichaguliwa mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Glory Mwambeleko, mtoto wa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Rukwa, Alfred Mwambeleko, aliingia katika Kamati ya Uendeshaji Taifa upande wa Tanzania Bara. Hao ni wale ambao akili yangu imedurusu haraka.
Baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2005, kila mwenye jina la Kikwete amesafiria nyota ya Rais. Salma Kikwete, mke wa Rais Kikwete alishinda kiulaini nafasi ya mjumbe wa NEC kupitia Lindi.
Ridhiwani, mtoto mkubwa wa Rais amekuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la UVCCM, mjumbe kwenye chama cha mpira wa kikapu, na hivi karibuni alikuwa makamu mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa klabu ya Yanga.
Si hivyo tu. Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alipoondolewa akidaiwa yeye na wajumbe wa Kamati Kuu ni gamba, alipozwa. Mtoto wake, January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, aliteuliwa katibu wa Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa.
Humo yumo Nape, mtoto wa mwanasiasa mkongwe Brigedia Moses Nnauye.
Nape hawezi kuona boriti mpya; wajumbe watatu wa sekretarieti ya Kamati Kuu wanatoka Singida. Nape, naibu katibu mkuu Bara, John Chiligati na Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba, wote wanatoka Singida.
Koo takatifu zinaonekana hata katika nafasi za ubunge na uwaziri. Emmanuel Nchimbi (mtoto wa mwanasiasa John Nchimbi); Dk. Hussein Mwinyi (mtoto wa Alhaji Mwinyi), Adamu Malima (mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Prof. Kighoma Malima), wote ni mawaziri. Aaaaah!
- Login or register to post comments