Azzan: Wanaonichafua ni Guninita, Ng’enda


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azzan

SIASA za kukamiana, kuchafuana na kuzibiana nafasi za uongozi zinazidi kuota mizizi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azzan yuko kikaangoni.

Mbunge huyo, alijipalia makaa tangu Aprili mwaka huu alipotoa rai kutaka Kamati ya siasa ya Mkoa wa Dar es Salaam ijivue gamba. Kauli hiyo imemponza na sasa mustakbali wake ndani ya CCM uko shakani kwani wale aliotaka wajivue gamba wamemkali kooni.

Kwanza, wamepitisha uamuzi wa kumfungia kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika kipindi cha miezi 18 (mwaka mmoja na nusu).

Pili, mtendaji mkuu wa CCM Mkoa, Kirumbe Ng’enda akamtuhumu kuwa anajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.

Tatu, mbunge huyo ambaye nyota ya uongozi ilianza kung’ara alipokuwa mwenyekiti wa soka Kinondoni na baadaye mkoa wa Dar es Salaam, ameshutumiwa kwa kuvunja ndoa ya kada mwenzake Salim Chicago.

Lakini Azzan kwa kauli yake anasema tuhuma zote hizo dhidi yake ni za uzushi, fitina na mchezo mbaya wa siasa ulioandaliwa mahususi kumchafua asiimarishe kampeni zake za kuwania nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoa mwakani.

“Shutuma zote juu yangu ni za uongo. Kiini cha yote haya ni uchaguzi mkuu wa viongozi utakaofanyika mwakani. Mimi nilishatangaza nia kwamba nitagombea uenyekiti ambao kumbe watu wengine wamefanya ni ajira badala ya kutumikia chama,” alisema Azzan katika mahojiano na mwandishi wa makala hii mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwake, Dar es Salaam.

“Mwenyekiti wa sasa wa CCM Mkoa ni John Guninita. Anaona kuwa mimi ni kikwazo kwake, kwa hiyo, kinachofanyika ni mbinu za kunitoa nje ya wigo wa kuja kugombea.” 

Azzan anasema kwamba wanaomzushia tuhuma zote ni walioonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo; Guninita ambaye atatetea na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na Ramadhani Madabida.

Mbunge huyo anadai Guninita na Madabida mara zote wamekuwa wakihangaika kumpoteza kisiasa wakihisi kwamba yeye ni tishio katika uchaguzi ujao wa CCM utakaofanyika mwakani.

Alipoulizwa kwanini amejengewa chuki na wenzake Azzan anajibu: “Haya mambo yalianza mbali, pale meya wa zamani wa Kinondoni, Salum Londa alipong’olewa ujumbe wa NEC Taifa.”

Guninita hakupatikana kutoa ufafanuzi na Ng’enda alisema kwa kifupi alichotangaza kwenye vyombo vya habari kuhusu adhabu ya Azzan ndiyo hicho hicho, huo ni msimamo wa chama.

Kwa upande wake Madabida amesema ni mapema mno kuzungumzia uchaguzi. “Unavyonieleza inaelekea Idd Azzan analalamika mitaani, lakini chama chetu kina utaratibu kwamba manung’uniko na madai yote yanapelekwa kwenye vikao na ufumbuzi unapatikana kwenye vikao. Namshauri afuate vikao.”

Kwa mujibu wa Azzan uchaguzi wa viongozi wa CCM mwaka 2007, ndio uliochangia hali hii ya mpasuko kwamba yeye alitajwa kuwa katika kambi ya Londa katika mikakati ya kumtafutia ushindi awe mjumbe wa NEC. Hata hivyo, Madabida alishinda kiti hicho.

Anasema uhasama ule ulihamia katika kampeni za kuomba ridhaa kupitishwa na chama kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu mwaka jana. Mbunge huyo, aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005 anadai alifanyiwa njama aenguliwe lakini aliwashinda wapinzani wake Mustafa Muro na Shy-Rose Bhanji.

Aidha, jina lake lilipitishwa na NEC na katika uchaguzi mkuu alishinda kwa kishindo. Kushindikana kwa njama za wapinzani wake kumzuia kuwa mbunge kwa mara ya pili ndiko kumeibua mikasa yote hii.

Kuhusu madai kwamba anatembea na Mwanakombo Ramadhani Mwinyimbegu “MK”, Azzan alijibu, “Huo ni uongo kwa asilimia mia moja. Sina mazoea na mwanamke huyo. Sijawahi kuhusiana naye hata kwa kutumiana meseji wala kutaniana.”

Kuhusu madai kwamba yeye ndiye alimsaidia mama huyo kukata rufaa baada ya kuenguliwa kuwania nafasi, anasema aliwasaidia watu wengi wenye malalamiko akiwemo MK. “Kwa hiyo, siyo kweli kwamba mimi nina uhusiano wa kimapenzi. Nasingiziwa tu.”

Kuhusu madai kwamba anafanya biashara ya madawa ya kulevya, Azzan amesema anayeeneza habari hizo ni Ng’enda. Hatua anazokusudia kuzichukua kuhusiana na tuhuma hizo amesema anawasiliana na wanasheria wake ili amfungulie kesi mahakamani.

Azzan amesema anaacha mambo mengine yote chini ya chama kwani kinafahamu sekeseke hilo tangu alipotoa rai kutaka wasiowaadilifu katika uongozi wa mkoa wajivue gamba.

Mbunge huyo aliingia matatani pale alipounga mkono hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kutaka wanachama wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi au makosa mengine yaliyochangia kushusha hadhi ya chama wajivue gamba.

Hata hivyo, tamko la Azzan lilipokewa vibaya, vikao vilifanyika haraka vya kumtaka ajieleze na siku chache baadaye akafungiwa miezi 18 kuwania uongozi.

Alipoulizwa MK kuhusu tuhuma zinazomkabili alisema kwa njia ya simu, “Chicago aseme ukweli asimsingizie Idd Azzan. Nimetengana naye.”

Lakini Chicago anasema hajampa talaka makusudi na kwamba anamtaka mkewe huyo aende akalalamike Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) au Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa). Chicago akatangaza waziwazi kuwa Azzan ndiye mbaya wake katika mgogoro wa ndoa yake.

“Ukweli kuachana na mke wangu kulisababishwa na Azzan kwa asilimia 100. Mke wangu alibadilika ghafla nyumbani kimapato na kitabia. Nikagundua sehemu ya fedha alichukua zetu, lakini bila ridhaa yangu maana naye alikuwa akiwania udiwani wa viti maalum,” anaeleza Chicago.

Habari za kuwako kwa uhusiano wa kimapenzi kati ya Azzan na mwanamke huyo, zilienea zaidi wiki mbili zilizopita wakati wa msiba Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Ndugumbi, Ibrahim Chuwa.

Habari hizo zinamsosonesha Azzan ambaye anasema; “Mimi namwachia Mungu yote. Sijawahi hata kuzungumzia suala la mapenzi na mwanamke huyu. Ni shemeji yangu. Namheshimu na rafiki yangu Chicago namheshimu.

Pamoja na mitafaruku yote hiyo, Azzan aliyeingia bungeni baada ya kumwangusha Peter Kabisa aliyeko ubalozini Afrika Kusini, anasema azima yake kuwania uenyekiti iko palepale.

Mbunge huyo amewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na baadaye Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) nafasi zilizosaidia kujenga uwezo wa kujieleza na hatimaye akawania na kushinda ubuinge mwaka 2005 na mwaka 2010.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: