Baada ya mabusu motomoto arushiwa chupi mikutanoni

Charles Zevallos, miongoni mwa wanasiasa maarufu zaidi nchini Peru, amezipeleka siasa za nchi hiyo katika hatua nyingine mwezi uliopita.
Zamani, akifahamika kwa tabia yake ya kupenda kubusiana na washabiki wake, hususani wale wa kike, sasa mwanasiasa huyo ameanza kurushiwa nguo za ndani (chupi) na akinadada na akinamama wanaohudhuria mikutano yake.
Matukio haya ya karibuni yameitikisa nchi hiyo masikini ya Amerika Kusini, ambako mambo kama yanayotokea kwenye mikutano ya Zevallos yanaonekana kama miujiza.
Lakini Zevallos si mwanasiasa wa kawaida. Katika mikutano yake mingi, alikuwa na tabia ya kugawa hata zawadi na fedha kwa ajili ya watu watakaokuwa tayari kumbusu uso kwa uso au kumrushia mabusu wakati akiwa jukwaani akihutubia.
Katika nchi zilizoendelea, kitendo cha akinadada na akinamama kumrushia nguo za ndani mwanamume hutafsiriwa kama ishara ya mapenzi lakini nchini Peru wachambuzi wanasema hawajapata tafsiri halisi ya vitendo hivyo.
“Pengine wanampenda kweli Zevallos na ndiyo maana wanafanya hivi. Lakini, inawezekana pia watu wanataka kupewa naye zawadi kubwa zaidi kuliko alizokuwa akitoa awali. Hebu fikiria, kama mtu anakupa fedha nyingi kwa kumbusu ukiwa mbali naye, je ukimrushia chupi yako unafikiri atakupa nini,” alisema Esteban Solazo, mchambuzi wa siasa za Peru.
Zevallos ambaye sasa anawania nafasi ya umeya wa jimbo la Maynas lililopo Kusini mwa nchi hiyo, huwa na utaratibu wa kugawa vitu kama saa na mipira kwa ajili ya watu wanaohudhuria mikutano yake ya hadhara.
Zawadi zake hizo ndizo hasa zinazodaiwa kuwafanya mabinti wapagawe na kufanya mambo ya ajabu katika mikutano yake ya chama cha 1000 Movimiento Integracion Loretana.
Mwanasiasa huyo amesema si vizuri kumfananisha yeye na mwanamuziki maarufu wa Wales, Tom Jones, ambaye imekuwa kawaida kwa wanawake kumrushia chupi zao wakati anapokuwa akitumbuiza.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa katika mji mkuu wa Peru, Lima, uliopo umbali wa maili 990 kutoka Maynas anakoishi Zevallos, wamedai kwamba matukio ya kurusha chupi jukwaani ni aibu kwa nchi hiyo.
"Kwa kweli ilikuwa ghafla sana na hata mimi nilishangaa. Sikumwomba hata mtu mmoja anirushie chupi wakati nikihutubia. Lakini ghafla nikarushiwa chupi ya njano na ghafla rundo la chupi likarushwa kwangu. Ni mshangao hata kwangu,” alisema Zevallos.
Hata hivyo, Zevallos amesema yeye hawezi kulaumiwa kwa ajili ya watu wanaorusha chupi majukwaani. Hawa wote wananipenda. Hivi unawezaje kumzuia mtu anayekupenda?
Ninaamini mapenzi yana nguvu kuliko kitu kingine chochote kinachoishi duniani, alijitetea.