Bahi wazomea waziri, wataka uhakika


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 25 August 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Naibu Waziri wa Nishati na Madini , Adam Kighoma Malima

KILA panapogunduliwa madini nchini na makampuni ya nje kuanza kuchimba, mara moja maisha ya wananchi hubadilika kutoka kuwa ya bahati na kuwa ya balaa.

Ndivyo ilivyo Bulyanhulu, Geita, North Mara na sehemu nyingine ambako madini yamegunduliwa. Wachimbaji wadogo hutupwa nje. Wakazi karibu na migodi hufagiwa kama takataka. Ufukara huwa njia ya maisha mdomoni mwa migodi iliyosheheni madini ya thamani ya mabilioni na mabilioni ya shilingi.

Hii ndio maana katika baadhi ya maeneo nchini ambako madini yamegunduliwa au kuna uvumi tu wa kupatikana kwa madini, basi hofu huanza kuwazonga wakazi wa maeneo hayo.

Hofu hii sasa imeanza kukabili wananchi wanaoishi katika Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma baada ya kutangazwa kwa taarifa bungeni hivi karibuni kwamba kumegunduliwa madini aina ya uranium wilayani Bahi.

Hatua ya kwanza, na hasa baada ya kukuta watafiti wamefika na kuingia kinyemela kwenye maeneo yao, wananchi hao walituma viongozi wao kuita uongozi wa juu wa serikali ili ukatoe maelezo juu ya hofu iliyowazonga.

Ndipo uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini ulipomtuma Naibu Waziri, Adam Kighoma Malima. Alikwenda Bahi wiki iliyopita na kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara.

Hoja ya wananchi wa Bahi kudai majibu ya kina ilitokana na kutoridhika na majibu aliyotoa kutokana na swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Margret Mkanga, katika mkutano wa Bunge uliopita.

Alipotoa maelezo ya hakikisho la usalama wa wananchi wanaoishi na kutumia maeneo ya ardhi yalipogunduliwa madini hayo, hakukidhi kiu ya wananchi.

Kwa bahati mbaya sana, Malima hakusoma alama za nyakati. Alijiendea Bahi na utamaduni uleule wa kutaka kuwasilisha tu maamuzi ya serikali na siyo kusikiliza wananchi waliomuita.

Naibu Waziri Malima alirejea kusoma maelezo yaleyale katika majibu yake ya swali aliloulizwa bungeni. Ni tatizo lake mwenyewe na aliyemtuma kwenda kuzungumza na wananchi wenye hofu.

Wana Bahi wanataka kuhakikishiwa hatima na usalama wao. Moja ya maswali yao kwa Malima ni kutaka kufahamu ni vipi maslahi yao yatazingatiwa na serikali wakati ikifikiria kuwahamisha ili kupisha wachimbaji.

Malima hakufanya hivyo. Kwa sababu alishindwa kukidhi kiu yao na hivyo kuwaacha wabaki na hofu yao ya kutokomezwa na serikali kama waonavyo serikali inafanya kwa wananchi wengine, basi wakamshukia.

Kama vile wananchi wamepigiwa kipenga, kwa pamoja walianza kumzomea waziri. Uamuzi wao unaonyesha msimamo wao. Ni matokeo ya kuchoka kuvumilia. Wameondoa uvivu.

Na hiyo ndiyo nguvu ya wananchi wanapochoka kuburuzwa na viongozi wao. Wanafalsafa wanasema siku zote kwamba “kumtaja” na “kumfedhehesha” muovu ni moja ya njia sahihi za kulazimisha mabadiliko.

Siku zote mawaziri wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakiamini kuwa wanayo haki ya kudhihaki wananchi ikiwemo kutoa majibu yasiyo na kichwa wala miguu ndani ya bunge. Wanadhani hata wakija majukwaa ya uraiani, watakubaliwa kuchapa siasa badala ya kutoa majibu ya kuridhisha wananchi.

Hili ndilo wananchi wanalitakataa. Hawako tayari kutumika kama ngazi. Hawako tayari kusikiliza porojo au kupokea amri za wanasiasa wanaoitwa mawaziri na wasaidizi wao.

Wana Bahi wamesikia yaliyowakuta wenzao Loliondo, North Mara, Bunda, Serengeti na Geita. Wanaumizwa nayo. Sasa wanapoona kumbe yanawakaribia, hawataki kufika hapo. Kuzomewa kwa waziri ni ujumbe rasmi kwamba wananchi wanakataa mapema kufanywa wakimbizi katika nchi yao.

Kuzomea waziri ni kumgomea. Ni ujumbe kwa serikali kwamba wao si kondoo au ng’ombe wa kuvutwa shemere ili kufika kule mchunga anakotaka waende. Wanataka wawe sehemu ya majadiliano na kufikia maamuzi.

Wanao uzoefu wa kutosha wa yanayotokea kwingineko. Wanajua wawekezaji wamekuwa wakidharau utu na maslahi ya wananchi; bali wakithamini madini wachimbayo na wanyamapori wawindao.

Wanajua imekuwa ni tabia ya wawekezaji kupanga mambo yao bila ya kuzingatia maslahi ya wananchi ambao ndio wanaopaswa kuwa walinzi wa mali zao.

Wana Bahi wanakataa mtindo huo wa wawekezaji kuona heri binadamu afe na kuzikwa lakini madini yachimbwe na wanyamapori wahifadhiwe ili waweze kuwindwa. Kwao na serikali, madini na wanyamapori ni muhimu zaidi ya binadamu.

Kule Loliondo wananchi wa familia za wafugaji wa Kimasai wanafukuzwa kwa nguvu za dola. Kwa kutumia polisi, wanachomewa makazi yao; wanaporwa mifugo yao. Wanahatarishiwa maisha yao.

Kwenye mgodi wa North Mara wananchi wanafanywa kunywa maji yaliyojaa kemikali zitokazo mgodini. Wanakamatwa wao na watoto wao na kushitakiwa na hatimaye kufungwa kwa sababu tu wamenywesha mifugo kwenye mto Tigithe ulio karibu na mgodi.

Malima anasema kuanzia mwaka 2007, kumekuwa na ongezeko kubwa la shughuli za utafutaji wa madini ya uranium nchini na makampuni makubwa ya wageni yanaendelea na utafiti wa madini hayo katika mikoa ya Kusini, mabonde ya Ruhuhu na Selous, Namtumbo na Mbambabay mkoani Ruvuma na Kanda ya Kati, ikihusisha mikoa ya Dodoma na Singida, sehemu za Manyoni.

Wananchi walimwambia waziri juu ya kutoarifiwa kuhusu shughuli hizo, bali wanaona watu wakifika vijijini mwao, hata usiku, na kuvamia mashamba wakichimba kisichojulikana.

Masikini Malima ameshindwa kuheshimu wananchi. Hakuona haki zao kama raia huru. Akashindwa kuomba radhi wala kuwaahidi kusimamia watafiti hao ili wafanye shughuli zao kistaarabu na kiutaratibu.

Wananchi wanajiuliza hivi hayo yanayoitwa makampuni makubwa ya wawekezaji wa kigeni ndiyo nini. Walitumaini watatolewa hofu na waziri. Hakufanya hivyo. Wanaona simulizi na vitisho.

Kusema tu kwamba utafiti unaofanywa umepata majibu yanayoashiria kuwepo madini yanayotumika kutengeneza nishati ya umeme, hakutoshi.

Tanzania ina historia mbaya katika kusimamia shughuli za uwekezaji hasa kwenye sekta ya madini. Mara kadhaa imeshuhudiwa wawekezaji wakikiuka masharti ya mikataba iliyowaruhusu kuendesha shughuli zao.

Wanasafirisha udongo nje ya nchi kwa kisingizio cha kwenda kuchunguza lakini hakuna majibu yanayotolewa. Zimetolewa taarifa za kuibwa kwa vinoo vya dhahabu lakini haielezwi wezi hao walipitaje kwenye milango minne hadi kufikia chumba kilichohifadhiwa vinoo hivyo.

Wanaokamatwa baada ya kilichodaiwa kuwa ni wizi, ni vibarua Watanzania peke yao, licha ya kujulikana fika kwenye milango hiyo hakuna mlinzi wa Kitanzania, bali wazungu watupu.

Watu wa Bahi hawataki kuja kushuhudia uharamia kama huo unafanyika mbele ya macho yao. Na wakati huo wanaoathirika watakuwa ni watoto wao.

Wawekezaji wengi wamekuwa na vitendo viovu kiasi cha kujenga uadui na wanavijiji walio karibu na maeneo ya shughuli zao. Watanzania, kama walivyo Bahi, wameshaumwa na nyoka, sasa wakiona hata mjusi tu wanaogopa.

Hofu ya wananchi wa Bahi ina msingi. Wanajifunza kutokana na yanayotokea kwa wenzao. Kila anapogusa mwekezaji panazuka balaa, kuanzia kwenye madini, ukodishaji ardhi na maliasili na utalii. Wananchi wa Bahi wanajitahidi kuepuka adha hizi.

Kilichobaki ni juu ya serikali kutambua au kutotambua kuwa hakuna tena wakati wa kudhalilisha Watanzania nchini pao. Shughuli za kiuchumi lazima ziende sambamba na kutambua utu na heshima yao.

Malima anaposema amefadhaishwa na kitendo cha kuzomewa na wananchi Bahi, hajakamilisha sentensi. Angeishia na jibu la kilichomfanya ashindwe kwenda Bahi na jipya, zaidi ya yale aliyoyasema bungeni. Watu wamechoka majibu ya kilaghai.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: