Bajeti 2010/11: Serikali ni jeuri au kiziwi

NI vigumu kuamini kwamba Serikali ya Awamu ya Nne kwa miaka mitatu sasa, ama imekataa au imebeza maombi muhimu ya wafanyakazi ya kuboresha maisha yao.
Serikali imeshindwa kufanya uamuzi mdogo sana, kutazama upya mfumo wa ulipaji wa kodi ya mapato maarufu kama PAYE yanayokatwa kila mwezi kwenye mishahara.
Hakuna shaka kwamba miongoni mwa mambo ambayo yanaumiza vichwa wafanyakazi wa nchi hii, ni mfumo huu wa PAYE.
Vyama mbalimbali vya wafanyakazi vilikwisha kukutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, pamoja na mambo mengine, kuwasilisha kilio chao juu ya makali ya PAYE.
Lakini kama hitoshi vyama hivyo kupitia Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (Tucta) moja ya hoja zao kwa serikali wakati mjadala wa kutaka nyongeza ya mshahara ili kufanya kima cha chini kuwa zaidi ya Sh. 300,000, walipendekeza kupitiwa upya mfumo wa PAYE.
Wafanyakazi wa nchi hii wamekuwa wanabeba mzigo mkubwa wa kodi kwa maana mbili. Kwanza, wenyewe wanalipa kodi kubwa inayotokana na jasho lao kupitia PAYE.
Lakini pili, wanakamuliwa kupitia kwa wafanyabiashara wanaotoa huduma na kuuza bidhaa mbalimbali ambako pia hulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat).
Hakuna mashaka kwamba wafanyakazi ni watu wa kuumizwa, wawapo ofisini mwao hata waendapo mitaani kwao kutafuta huduma yoyote, kodi! kodi kila kona!
Ni kwa maana hiyo, wafanyakazi hawa kupitia ama vyama vyao vya wafanyakazi au hata kwa mtu mmoja mmoja hoja imekuwa ikijengwa kwamba mfumo wa kodi nchini si mzuri kwao, unawaumiza.
Ni jambo la kawaida kabisa kwa mfanyakazi anayepata mshahara wa Sh. 2 milioni kwa mwezi kulipa kodi kubwa kuliko mfanyabiashara anayefanya biashara ya mamia ya mamilioni.
Kwa kuonyesha jeuri wafanyakazi ama kwa sababu walitingisha kibiriti kwa kutishia kugoma 5 Mei 2010, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, aliwasilisha bajeti ya serikali wiki iliyopita, akionyesha wazi kwamba serikali haina nia ya kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa kodi.
Mkulo alisema kwamba asilimia ya PAYE kwa wafanyakazi itapungua kutoka asilimia 15 hadi 14, lakini ni kwa wale wanaolipwa mshahara wa kuanzia Sh. 100,001 hadi 360.000 tu.
Ngazi wa kodi kwa mishahara ya wafanyakazi kama ilivyopitishwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2009/10, mshahara usiozidi Sh. 100,000 hautozwi kodi; kati ya Sh 100,001 hadi 360,000 inatozwa asilimia 15.
Kwa wanaolipwa kuanzia mshahara wa Sh. 360,001 hadi 540,000 unatozwa asilimia 20 na kiwango cha ziada cha Sh. 39,000; wakati wa mshahara kuanzia Sh. 540,001 hadi 720,000 unatozwa kodi ya asilimia 25 na nyongeza ya Sh. 75,000.
Mshahara kuanzia Sh.720,001 na kuendelea kodi ni asilimia 30 na nyongeza ya Sh. 120,000.
Kwa kauli ya Mkulo, watakaonufaika na punguzo la asilimia moja ni wale walioko kwenye kundi la Sh. 100,001 hadi 360,000 tu, huku makundi mengine yakiachwa kama yalivyo sasa katika bajeti ya mwaka wa fedha mpya wa 2010/11.
Kwa maneno mengine serikali imeendelea na utaratibu wake wa kuwaachia makali wafanyakazi hata kama wana hoja ya msingi juu ya malipo yao.
Nini maana ya jeuri hii ya serikali? Kuna dhana mbili kubwa zinazoweza kujengwa juu ya msimamo wa serikali. Mosi, inaweza kutafsiriwa kwamba ni jeuri.
Kwamba serikali haijali, haitishwi na wala haina habari na wafanyakazi, kwani kwa wastani wanaweza kuwa na kura 300,000 ambazo ukilinganisha na watu milioni 14 waliojiandikisha ni nguvu ndogo mno kuleta mamdhara katika uchaguzi mkuu ujao. Hivyo, haiwatishi wala kuisumbua!
Lakini jeuri hii pia inaweza kuwa inachangiwa na dhana ya pili, kwamba kutokana na serikali kushindwa kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa sababu haitaki kufanya hivyo, imeamua kufa na vile vile vyanzo vyake vya jadi.
Ndiyo maana ukichambua bajeti ya mwaka baada ya mwaka serikali inajua tu kuongeza kodi kwenye soda, bia, sigara na pombe kali; ingawa mwaka huu wamepumzisha mafuta ya petroli.
Kwa hiyo, dhana ya pili ya kushindwa kuwa wabunifu, au kuogopa kujaribu kwenye maeneo mengine imeifanya serikali kushindwa kutambua kwamba kuendelea na mfumo wa sasa wa kuwakamua wafanyakazi wake mwaka baada ya mwaka, kimsingi hata hizo juhudi zake za kupambana na umasikini haziwezi kuzaa matunda.
Kibaya zaidi katika mfumo huu wa kuwatwanga wafanyakazi PAYE kubwa ni kuwakamua wanaofanya kazi zaidi kwa kujituma zaidi; wale wanaojitahidi kiasi cha kujikuta wakipanda kutoka ngazi moja ya mshahara hadi nyingine, na kwa kweli wengi wa watu hawa si watumishi serikalini.
Watumishi serikalini kwa kawaida hawalipwi mshahara wowote wa maana, hawa wanaishi kwa semina, safari na viposho vingi vingi vya uficho na uongo uongo.
Kimsingi wanaoumizwa na kodi hizi za kukomoana si watumishi wa serikalini ambao ninaamini ni wahusika wakuu wa kuandaa bajeti hizi.
Ni watumishi hao hao ambao licha ya kutambua utajiri uliosheheni ndani ya nchi hii wameshindwa kutafuta vyanzo vipya vya kodi. Matokeo yake, kila mwaka waziri wa fedha anaposimama bungeni anaishia kusoma kitu kile kile!
Ndiyo maana kila tafakari inayofanywa juu ya uamuzi wa huu wa serikali wa kupuuza na kuwaacha wafanyazi njia panda katika bajeti hii, inaonyesha kuwa kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Nnne – ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’ ni maneno matupu yasiyokuwa na tija.
Hata hicho ambacho Mkullo anachoita, “nyongeza ya mshahara wa kima cha chini” ambacho kitatangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, atakapowasilisha makadirio ya ofisi yake, bado ni kiini macho.
Ni vigumu kuwasadikisha watu kwamba kuna nia ya kuwajengea maisha bora wananchi kwa hatua kama hizi za kuwashughulikia kwa kodi kubwa wale wote ambao wanafanyakazi kwa bidii.
Ni vigumu kuwaaminisha wananchi, kwamba hiki kinachofanyika sasa, si kuwakatisha tamaa na kuwaondolewa morali wa kujituma wafanyakazi iwapo kila nyongeza ya kipato cha mtu mwisho wa siku kinaishia kwenye kodi za serikali.
Utamaduni huu ni mbaya na unajikita kwenye kitu kimoja tu, serikali kukosa ubinifu wa kutambua vyanzo vipya vya mapato. Maamuzi ya kuendelea na PAYE inayolalamikiwa kila kukicha ni maamuzi ya kiimla na kinyonyaji.
Serikali inaliyoingia madarakani kupitia sanduku la kura ni lazima ijifunze kusikiliza kilio cha wananchi wake, vinginevyo kuna kila sababu ya kushuku mfumo wa kutumia sanduku la kura kama kweli ndio unaoingiza watu madarakani.