BAJETI 2013: Wakulima walia, wenye viwanda hoi, ajira kaputi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
Gumzo

HUYU waziri wa fedha vipi? Saa mbili na nusu zote amesahau kuwa nchi yetu ni ya wakulima; tena wengi kuliko wawekezaji wanaowaabudu?

Huo ni ujumbe kupitia simu ya mkononi kutoka kwa mtumaji aliyesema anaishi Mbarali, mkoani Mbeya.

Anasema, “Mhariri, naomba mjulishe waziri huyu wa serikali ya CCM; kuwa hajatusaidia sisi wakulima wa mpunga. Sasa ajue hatuna imani na bajeti aliyoisoma jana (Alhamisi iliyopita).”

Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, aliwasilisha bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2012/13 bungeni mjini Dodoma, Alhamisi kuanzia saa 10:05 alasiri.

Baadaye nikiwa kwenye baraza ya kahawa mtaa wa Idrisa, Kariakoo, alijitokeza kijana mmoja na kuchangia mjadala juu ya bajeti ya serikali.

“Nilitoka Arusha jana. Jamaa zangu walima vitunguu wa Mto wa Mbu wanalalamika jinsi wanavyolima bila msaada wa serikali. Pembejeo ni ghali, hawazimudu…” analalama.

Kijana anasema kuwa sasa wakulima wameingia utumwani…“Wafanyabiashara wa Kenya wanadhamini usafishaji mashamba, wanatoa mbegu, mbolea ya kupandia na kukuzia. Wanatoa dawa za kuulia wadudu na kulipia upaliliaji mashamba. Vyote hivi wanatoa kwao ambako vinauzwa bei nzuri.”

Anasema mazao yakifikia kuvunwa, Wakenya wanakuja kusimamia. Wanakuwa wameshapanga bei ya kununua vitunguu. Wanapakia kwenye malori. Wanaondoka na vitunguu vilivyolimwa Tanzania. Wanakwenda kuuza kwao….”

Alipofikia hatua jiyo nikamuuliza, sasa hapo tatizo ni nini? Anajibu, “Huu ni ukulima wa kitumwa. Afadhali manamba. Unafanywa mtumwa ndani ya shamba lako mwenyewe, ndani ya nchi yako…na unaambiwa kuna serikali.”

Hoja hizi za kijana zikapeleka akili yangu wilaya ya Tandahimba, mkoani Lindi. Aprili mwaka huu, wakulima wa korosho waliamka na kusakama viongozi wa vyama vya ushirika.

Kisa? Walitaka malipo yao ya pili ya mauzo ya korosho kwa chama cha ushirika tangu mwaka uliopita. Walitaka fedha au korosho zao – mojawapo.

“Hawa jamaa wamezoea kutunyonya. Miaka yote wanatunyonya. Tunalima kwa jasho letu... wanataka tuuze kwa utaratibu wao usiotija kwetu. Tunataka serikali kuu wajue tumechoka. Viongozi watuelewe sisi ni binadamu tunaofikiri,” alikaririwa mkulima wa kijiji cha Malamba akilalama.

Wananchi wanachukia mfumo wa ununuzi wa mazao ya kilimo uitwao “Stakabadhi ghalani.” Ni mfumo wa kukopa wakulima kwa kulipa malipo yao kwa awamu mbili.

Vyama vya ushirika havina fedha kwa hivyo mfumo ulioletwa kama njia mbadala, umeshindikana kutekelezeka kwa manufaa ya wazalishaji.

Wakulima wa mpunga, vitunguu wanalia. Hawasaidiwi na serikali. Wale wa vitunguu wanalazimika kukubali utumwa. Wenzao wa korosho wanalazimishwa kuuza korosho kwa mkopo.

Hali hiyo ndiyo inawakumba wanaolima pamba, kahawa, alizeti na mazao mengineyo.

Mfumo wa kilimo hauna tija kwa mkulima, bali hunufaisha wanunuzi wa mazao. Hao hujipanga na hata kuamua bei moja kwa nchi nzima.

Matarajio ya wakulima ni kwamba wakishavuna, watauza mazao kwa utaratibu wa ushindani, kwa kuwa uchumi sasa unaongozwa na nguvu ya soko.

Waziri Dk. Mgimwa hakushughulika na wakulima, pamoja na wafugaji, wavuvi na warina asali. Hata bajeti ya maeneo haya imepunguzwa kwa Sh. 400 milioni.

Bajeti ya serikali ya Sh. 15 trilioni haijibu tatizo la wafanyakazi; wafanyabiashara wadogo; na haiendi katika kuwezesha nchi kujitegemea.

Ahadi za waziri za “kusimamia vema matumizi ya fedha,” ni zilezile za miaka yote – maneno, siyo vitendo.

Ingawa serikali inadai kuwa imepunguza makali ya kukata kodi kwenye mishahara isiyofikia Sh. 170,000; bado haijaonyesha kuzingatia athari za mfumuko wa bei ambazo humpunguzia mfanyakazi uwezo wa kununua mahitaji ya lazima.

Bado mfanyakazi atalazimika kutumia karibu mshahara wake wote kwa ajili ya ununuzi wa chakula; bila kufikiria tiba na elimu kwa watoto.

Hataweza kutenga fedha za kuwekeza ili “kitegauchumi” chake – nyanya, pilipili, ukwaju pale barazani – kama kipo, kimzalishie mapato ya nyongeza.

Na kwa kuwa hata mafao ya kustaafu hayajaimarishwa vilivyo, atakapostaafu ataendelea kuishi katika ufukara wa kutupwa.

Wataalamu wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), na Felix Mosha (Mwenyekiti wa shirikisho la wenye viwanda nchini (CTI), wanakerwa na hali hii.

Prof. Lipumba anasema kushuka kwa mgao wa fedha za bajeti katika kilimo ni ushahidi jinsi serikali isivyotilia uzito uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

“Serikali inapothibitisha ongezeko kali la mfumuko wa bei, maana yake hatuzalishi chakula cha kutosha nchini. Lakini tatizo huzidi pale isipowekeza, kwani shughuli za ugani na upatikanaji pembejeo hautaimarika. Sasa huu ni mzaha,” anasema Prof. Lipumba.

“Mimi nawaasa Watanzania wasiweke matumaini kwa bajeti hii. Hakuna matunda. Tuna tatizo kubwa la kukosa uongozi imara wa kutekeleza bajeti inayotangazwa. Hawa waliopo hawawezi kusimamia hata yale wanayoahidi,” anasema Lipumba.

Dk. Mosha ambaye pia ni mwenyekiti wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), anasema serikali isipoweka mkazo katika kukuza kilimo itaongeza tatizo la ajira na maisha magumu kwa wananchi.

Maoni ya wanauchumi hao yamechotwa kwenye mjadala wa bajeti ulioendeshwa na kituo cha televisheni cha Star Tv asubuhi, Jumamosi iliyopita.

Godfrey Simbeye, mtendaji katika taasisi ya sekta binafsi nchini (TPSF), anasema hawakushiriki katika maandalizi ya bajeti hiyo na ushauri wanaoutoa umekuwa ukipuuzwa na serikali.

“Serikali inasahau jukumu lake kwa biashara za wananchi… hasa inapojigamba kulenga kukuza ushirikiano kati yake na sekta binafsi, huku  ikikataa kushirikiana nao. Hilo ni tatizo. Matokeo ni kujinyima fursa muhimu ya kuinua uchumi,” anasema.

Kupanda kwa gharama za maisha kumeendelea kulalamikiwa kwa miaka yote saba tangu Rais Jakaya Kikwete apange ikulu.

Takwimu zinaonyesha bei za vyakula zilipanda kwa wastani wa asilimia 24.7 kufikia Aprili mwaka huu.

Wataalamu wa kimataifa wa masuala ya usalama, wanaamini kuwa ukosefu wa ajira na chakula cha kutosha katika nchi za Afrika, ni baadhi ya sababu kuu zinazochochea vurugu.

“Ukosefu wa ajira unakua mwaka hadi mwaka nchini. Hilo lisingekuwa tatizo kama tunaona mipango ya kulipunguza. Ukweli ni kwamba serikali haionyeshi kwa dhati kupambana na tatizo hili,” anasema Dk. Honest Ngowi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro.

Anasema serikali ingewekeza ipasavyo katika kilimo, uzalishaji ungeongezeka kwenye viwanda… kukua kwa sekta ya viwanda kungeongeza nafasi za ajira, hasa kwa vijana ambao idadi yao inazidi kuongezeka kila mwaka,”

Anasema taifa linalokosa mipango ya kuzalisha ajira linakaribisha balaa; hasa kwa vile vijana ndio wasaka kazi wakubwa kutokana na kuanza maisha baada ya kuacha kulelewa na wazazi na wasimamizi wao.

Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini, ametafakari bajeti ya serikali na kuja na uchambuzi alioita “Mafukara milioni 30.”

Katika makala yake kwenye mtandao binafsi wa kompyuta (blogu) uitwao Zitto na Demokrasia, anasema “mipango ya kukuza uchumi inazalisha masikini zaidi.”

Anasema, masikini wa Tanzania wapo zaidi vijijini. Uchumi wa vijijini kwa kipindi cha muongo mmoja umekua kwa wastani wa asilimia moja tu.

Anasema uchumi unaokua sasa si uchumi wa Watanzania bali wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano na ujenzi; huku wananchi wengi vijijini wakiendelea kuandamwa na ufukara bila juhudi mahususi za kuwakwamua.

Zitto ameandika pia kuhusu bajeti ya serikali kuwa yaweza kuwa bajeti ya kulipa madeni zaidi kuliko kuchochea maendeleo.

Ikiangaliwa kwa kasma, bajeti inaonyesha kuwa kasma yenye kiwango kikubwa zaidi cha fedha kuliko vyote ni Kasma Na. 22 ambayo ni kwa ajili ya malipo kwa deni la taifa.

Bajeti yaweza pia kuwa ya kukopa maana jumla ya Sh. 5.1 trilioni (Dola 3.19 bilioni) ni mikopo kwa serikali.

Vurugu za Tandahimba

KATIKA kinachoitwa “vurugu za Tandahimba,” wananchi waliamuru kufungwa shule ya msingi na sekondari katika kijiji cha Mihambwe; wakaamuru walimu wachapwe viboko; walivamia na kuchoma moto kituo cha polisi cha kijijini hapo; walipiga polisi wawili waliowakuta kaunta.

Walichoma moto nguzo 10 za umeme katika vijiji vya Mihambwe, Miule, Mahuta na Matogoro. Miji ya Tandahimba, Nahyanga na Mahuta ikakosa umeme.

Walifunga barabara kuu ya Mtwara, Tandahimba hadi Newala kwa kuweka magogo na kuchimba mashimo.

Walivamia makazi ya askari polisi na makazi ya watumishi wa halmashauri. Inadaiwa baadhi ya mali za polisi na watumishi ziliporwa wakati huo. Iliripotiwa pia kuwa gari la Taasisi ya Kupambana na kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Wilayani lilipigwa mawe.

Wakulima wanadaiwa kuvamia nyumba wanazoishi mhandisi na mwanasheria wa halmashauri na kupora mali. Wanadaiwa pia kuvunja ofisi kuu za chama kikuu cha ushirika Tandahimba/Newala (TANECU); na ofisi za chama cha walimu wilaya na kuchukua vifaa.

Hii la ununuzi wa mazao ya wakulima – mara hii koroshoni, linahitaji majibu au dawa haraka. Kama ya Tandahimba yatatandawaa nchi nzima, kutawalika kutakuwa hadithi ya kubuni.

‘Deni la Taifa’ hili hapa

KUNA deni la taifa litokanalo na mikopo kutoka nje. Lakini kuna deni la ndani ya nchi litokanalo na watawala kutotenda wajibu wao. Hili la pili, tunaloweza kuita “Deni la Watawala,” linakua kwa kasi:

 • Elimu ya Msingi: Walimu hawatoshi, madarasa hayatoshi; vifaa vikiwemo vitabu vya ziada na kiada havitoshi. Bajeti kimya!
 • Elimu ya Sekondari: Walimu wa sayansi na hisabati hawatoshi; vitabu vya kiada havipatikani na maabara za sayansi ama hazipo au zilipo ni majengo tu.
 • Elimu ya Juu: Serikali inashindwa kulipia wanavyuo iliowadhamini; inasababisha vurugu. Bajeti kimya!
 • Rushwa, wizi na ufisadi serikalini unazidi – raslimali, maliasili na vitendea kazi vinafujwa. Bajeti “ola!”
 • Mishahara ya wafanyakazi wa umma na sekta binafsi ingali duni. Kuongezewa chochote sharti wagome na kuandamana.
 • Pensheni za waliostaafu zingali za viwango vya chini, wakati mashirika ambayo yanazisimamia yanaogelea katika mamilioni ya mabilioni ya shilingi na kumeremetesha wachache.
 • Wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wangali mitaani wakidai mafao yao, miaka 35 tangu jumuiya kuanguka. Wao wanadai serikali inakaa kimya mpaka wote wafe. Bajeti kimya!
 • Kilimo: Huu ni wimbo tu. Hapaonekani mipango wala juhudi za makusudi za kukuza kilimo cha mtu mmojammoja au mashamba makubwa.
 • Ujasiriamali: Huu nao ni wimbo. Biashara bila mikopo ni kupigia ngoma majini. Viwango vya riba haviruhusu machinga kukopa. Bajeti kimya!
 • Karibu Sh. 2 trilioni ambazo zingekuwa mapato ya taifa kila mwaka, hazikusanywi katika sekta nyeti ya madini na kodi.
 • Migogoro ya ardhi inaongezeka – serikali inajali wawekezaji kuliko wananchi kiasi cha kushiriki kuwaondoa makazini mwao kwa ukatili mkubwa: kuharibu mali zao na kufuta kabisa matumaini yao kiuchumi.
 • Ardhi yenye madini mbalimbali imeuzwa kwa wakuja kutoka nje ya nchi. Wanachota wanavyotaka na kuiachia makombo serikali. Bajeti kimya!
 • Bandari zimekodishwa kwa watu binafsi wanaovuna matrilioni ya shilingi kila mwaka na kulipa serikalini fedha kiduchu.
 • Mafisadi papa, raia na wageni, wanaogopwa. Hawashtakiwi.
 • Umeme: Taifa ni kama likjo gizani. Ukosefu wa umeme wa uhakika unaathiri vibaya uzalishaji na uchumi kwa jumla.
 • Uhuru wa habari na ule wa vyombo vya habari haujapatikana, ili kuwezesha upitiaji wa nyaraka za serikali na kuchimbua vyanzo vya vikwazo vikuu kwa kukua kwa uchumi wa nchi.
0
Your rating: None Average: 3.4 (7 votes)