Bajeti mpya ndani ya usiri mchafu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MPAKA naandika makala hii, sifahamu vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika bajeti ya kwanza itakayotekelezwa na serikali ya umoja wa kitaifa.

Kupata taarifa za mwelekeo wa bajeti imekuwa jambo gumu isivyofikirika. Hakuna kiongozi aliyetayari kujitolea kueleza.

Waziri wa Fedha na Maendeleo ya Uchumi, Omar Yussuf Mzee hakuwa tayari hadi juzi Jumatatu kueleza mwelekeo wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.

Hata Katibu Mkuu wake, Khamis Mussa Khamis, naye hakupenda kuzungumzia suala hilo.

Iwapo waziri mwenye dhamana ya fedha na uchumi amenyamaza, na katibu mkuu wake afanyeje? Sasa ofisa gani mwingine wa kuthubutu kusema.

Usiri wa kupindukia na kwa kweli usio sababu, ni miongoni mwa matatizo yanayochafua taswira ya serikali inayoendeshwa kwa ushirikiano wa vyama viwili vikuu vilivyoafikiana kuendesha siasa pamoja kama hatua ya kufukia siasa za chuki, hasama na tenganishi zilizotawala Zanzibar kwa miaka mingi.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vilifikia maridhiano yaliyowezesha katiba ya Zanzibar kufanyiwa mabadiliko ili kujumuisha vifungu vinavyoruhusu uundwaji wa serikali ya pamoja.

Mabadiliko hayo yaliyoidhinishwa na wananchi kupitia kura ya maoni iliyopigwa 31 Julai, 2010, na baadaye kufanyika kwa uchaguzi mkuu Oktoba, ambao pamoja na kuacha manung’uniko kwamba matokeo yalichezewa, yamesaidia kurudisha utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Kwa jumla, wananchi tangu awali walijenga matumaini makubwa ya serikali ya umoja wa kitaifa kufanya kazi kwa ufanisi ili kufufua uchumi na kuimarisha utoaji wa huduma za jamii.

Lakini, haikuchukua muda mrefu serikali iliyoundwa na rais Dk. Ali Mohamed Shein akiteua makamu wawili wa kumsaidia – wa kwanza atokaye CUF kilichochukua nafasi ya pili, na wa pili aliyetoka CCM, ilikabiliwa na mvutano.

Si rahisi viongozi wenyewe wakuu hao kukubali hilo, kwani mara kadhaa wamejinasibu kuwa wanafanya kazi kwa ushirikiano na maelewano. Zipo taarifa za kutosha kuwa mambo hayaendi vizuri.

Kinachotatiza wananchi ni kule kuamini sasa kwamba kuwepo kwa serikali ya umoja kumezidisha ugumu wa maisha kutokana na mfumuko wa bei kupanda kwa kasi ukichochewa na ongezeko lisilodhibitiwa na serikali la bei ya mafuta.

Ingawa bidhaa za vyakula zipo kwa wingi, serikali ni kama vile haina meno au inaona muhali kudhibiti wafanyabiashara wakorofi wanaohodhi bidhaa kwa lengo la kupandisha bei watakavyo pamoja na wale wanaoingiza bidhaa mbovu.

Matatizo hayo yamerithiwa. Lakini ni kitu cha kusikitisha kuwa serikali iliyoingia nayo imegoma kushughulikia ipasavyo, badala yake viongozi wake wamebaki kutoa ahadi tamtam za kuchukua hatua.

Kwa mfano, wakati viongozi wanajua fika kupanda holela kwa bei ya mafuta ni kichocheo kikuu cha kupanda bei za bidhaa nyinginezo, walibaki kimya wakati mafuta yalipopandishwa bei mara mbili ndani ya mwezi Aprili.

Si waziri wa fedha na maendeleo ya uchumi, Mzee, si waziri wa biashara, uwekezaji na utalii, Nassor Ahmed Mazrui, wala makamu wawili wa rais waliofunua vinywa na kuongoza njia.

Unapata picha kwamba serikali haikuwa na umoja katika suala hili. Labda wa CCM waliona vyao, tofauti na walivyoona wenzao wa CUF.

Ni mtindo wa viongozi kuviziana – wale waliotoka CCM wanaachia wa CUF waseme maana wanasema, “wao walizoea kusemasema.”
Nao viongozi wa CUF kwa kutambua msisitizo wa Dk. Shein wa kutaka viongozi wazingatie misingi ya uongozi wa pamoja, wakaamua kubana.

Ni hadithi ya “nani amfunge paka kengele.” Na mwenendo huu umezidisha matatizo katika jamii na hatimaye mrejesho ni wananchi kuanza taratibu kukosa imani na serikali waliyoitumainia sana.

Hivi karibuni, akizungumza na viongozi watendaji wa serikali, Dk. Shein alihimiza wajifungue na kujieleza kwa umma. Alitaka wawe rafiki wa vyombo vya habari. Wapi bwana!

Hakuna aliye tayari kujitokomeza mapema. Ukiteta na viongozi mmoja mmoja unaambiwa wazi wanacheza ngoma kwa uangalifu kwani manju – wakiwa na maana ya rais – hatabiriki.

Yaweza kuwa kweli Dk. Shein hatabiriki. Ameonyesha mwanzo wakati akiunda serikali. Kama alisikiliza maluteni wake wawili, hakuzingatia ushauri wao.

Wala hili si la ajabu au la kuzua; mwenyewe alipata kusema: “Mimi ndiye rais, ninao wasaidizi wangu. Wao wananishauri lakini mimi ndiyo mwamuzi wa mwisho.”

Alitoa kauli hiyo baada ya kubaini shutuma zikimwangukia kuhusu alivyokuwa anateua watendaji wa serikali.

Dk. Shein aliteua serikali kubwa isivyo kawaida na isiyoendana na uwezo wa uchumi. Aliamua kuingiza hata watumishi waliokwishastaafu kazi na kulipwa mafao yao. Wengi wao si wanataaluma mahsusi.

Alikumbana na msukosuko wa kuteua majaji walioitwa baadhi yao “hawana uwezo na waliokosa uadilifu.” Aliposhauriwa kutowaapisha, aligoma na kusingizia kuwa yeye aliletewa tu majina.

Serikali yake ikapata mtihani wa tishio la kushtakiwa kikatiba na Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) wakipinga mwenendo mbaya wa mwanasheria mwenzao, Hamid Mahmoud Hamid aliyeachia ngazi ya ujaji mkuu.

Hamid alilaumiwa kupendekeza majina ya majaji kibinafsi huku akikiuka utaratibu wa kikatiba wa sharti la kufanya mashauriano na Tume ya Utumishi ya Mahakama (JSC) ambayo jaji mkuu ndiye mwenyekiti.

Dk. Shein alichelewa kuwaapisha. Mgogoro ulipozidi huku wanasheria wakiwasilisha notisi ya kushitaki, rais alikataa maombi mapya ya Hamid kutaka aongezewe muda wa kuwa jaji mkuu kwa kisingizio ati “hajamaliza kazi alizopangiwa.”

Hili lilitiliwa shaka sana na wanasheria kwani kwa uhakika kabisa, mkataba wake wa awali alipostaafu kwa hiari kabla ya muda Novemba 2009, ulisainiwa kinyemela na uongozi wa Amani Abeid Karume.

Tatizo hilo lilifungamana na udhaifu wa serikali kufuata misingi ya utawala bora. Na baada ya kujifichaficha, hatimaye ikathibitika, serikali inadharau utawala bora.

Katika kesi iliyofunguliwa na wamiliki wa makontena ya Darajani, mahakama ilitoa amri makontena hayo yaliyofungwa kwa zaidi ya miezi miwili sasa yafunguliwe wakati uamuzi wa kesi ya msingi unasubiriwa.

Serikali imekaidi na kugoma. Ikaongeza ulinzi wa askari wake kuzunguka eneo la makontena. Wafanyabiashara walipotaka kulazimisha kufungua maduka yao, wakatunishiwa misuli. Wakaufyata na mahakama haijaita kiongozi mkorofi kujieleza.

Nimeeleza hayo makusudi ili kuonyesha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wakati serikali ikitarajiwa kutoa bajeti yake ya kwanza wiki ijayo.

Kuna tatizo la ufisadi kwa viongozi serikalini. Linahitaji nidhamu na uzalendo wa kweli. Linahitaji viongozi waamuzi kuchukua hatua kulikomesha kwani linakula raslimali za umma zilizolenga kunufaisha umma badala watu wachache walafi.

Nitashangaa iwapo elimu na tiba havitapewa uzito wa juu kibajeti kama ilivyo kwa miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi. Maji, nishati na matumizi bora ya ardhi ni vipaumbele vingine muhimu. Kipaumbele cha msingi zaidi ni uongozi mwema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: