Bajeti ya serikali hii hapa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 09 June 2010

Printer-friendly version
Mustafa Mkullo, Waziri wa Fedha

KODI! Kodi! Kodi, ndio mwelekeo wa Bajeti ya Taifa inayotarajiwa kutangazwa kesho.

Baada ya kulaumiwa na wanauchumi nchini na hata wafadhili kufikia hatua ya kukata sehemu ya misaada yao, sasa serikali imekuja na “panga” la kodi.

Kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo na nyaraka nyingine za serikali ambazo gazeti hili limeona, vinathibitisha mwelekeo wa ongezeko la vyanzo vya kodi na kodi yenyewe.

Mkullo aliiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge, Fedha na Uchumi, wiki iliyopita kuwa serikali inaimarisha mfumo wa makusanyo yake ya kodi kwa kuhusisha vyanzo vipya.

Inatarajiwa maeneo ambako kodi itauma ni pamoja na pale ambako kulikuwa na misamaha ya kodi na kwenye bidhaa ambazo serikali imejenga utamaduni wa
kupandisha bei zake kila mwaka.

Katika mwaka wa fedha wa 2010/2011, serikali inatarajiwa kutumia Sh. 11.1 trilioni, kiasi ambacho ni Sh. 1.6 trilioni zaidi ya bajeti ya mwaka jana.

Kwa mujibu wa mwelekeo wa bajeti, Sh. 7.9 trilioni ni kwa matumizi ya kawaida na Sh. 3.2 trilioni ni kwa ajili ya maendeleo.

Hata hivyo, nyongeza ya Sh. 1.6 trilioni kwenye bajeti ya mwaka huu ina umuhimu kidogo kwa kuwa kilicholipua bajeti ni kushuka kwa shilingi na kupanda zaidi kwa dola ya Marekani.

Wakati wa bajeti mwaka jana thamani ya dola ilikuwa Sh. 1,250. Leo ni zaidi ya Sh. 1,400.
Bajeti ya sasa inakuja wakati serikali ya Rais Jakaya Kikwete inalaumiwa kwa kutofanya vizuri au kuzembea kukusanya kodi.

Kuzorota katika kukusanya kodi kulivunja kimya cha rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kwenye mkutano wa uchumi duniani miezi miwili iliyopita.

Alisema anashangaa nchi zinazoendelea ambazo zinakaa kimlegezo zikisubiri misaada kutoka kwa wafadhili na kusisitiza kuwa “watu wanajiendeleza wenyewe;” hawasubiri kuendelezwa na wengine kutoka nje.

Mkullo anatarajiwa kulieleza bunge pigo lililoipata serikali kutokana na kushuka kwa kiwango cha mikopo kutoka nchi wahisani na marafiki wengine.

Kiwango hicho cha mikopo kimepungua kutoka dola 840 milioni hadi dola 534 milioni.
Ni kutokana na pigo hilo, serikali imelazimika kukopa Sh. 983.7 bilioni kutoka kwa mabenki ya biashara kwa masharti ya kibiashara, jambo ambalo linazidi kuteteresha uchumi.

Ukopaji huo wa serikali katika mabenki ya biashara umewatisha wachumi wengi nchini akiwamo Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kama fedha hizo zinakopwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida basi ni hatari, kwa sababu benki binafsi zinakuwa na riba,” amesema Profesa Semboja.

Amesema unaweza kuanza kuhisi kuna mazingira fulani ya kushawishiwa kwenda kukopa kwenye mabenki binafsi kwa maslahi fulani binafsi yasiyosaidia nchi.

Msomi huyo amesema kama serikali ilishindwa kupata fedha kwa njia nyingine kama za treasury bills (hati fungani), ingeshirikisha sekta binafsi na kuwataka waanze kulipa kodi ambazo walisamehewa.

“Mfano mwaka jana tumeona misamaha mingi ya kodi. Katika sekta ya madini kwa mfano, hawalipi kodi ya mafuta wanayotumia na mara ya mwisho ilipendekezwa waanze kulipa.

“Migodi inapata faida kubwa na inapanuka kibiashara; sasa wako kwenye soko la dhahabu la dunia…wanatengeneza faida kubwa,” amefafanua prfesa Semboja.

Anasema ilitarajiwa serikali iangalie suala hilo kwa makini na si kuwaomba, bali kuwaelekeza tu kwamba ile kodi ambayo hawakuwa wakilipa, sasa waanze kulipa kwa kuwa hali ya uchumi siyo nzuri.

Mwalimu huyo wa chuo kikuu ametoa mfano wa Marekani ambako alisema uchumi ulipoyumba, rais aliwaomba wawekezaji wakubwa binafsi kuanza kulipa baadhi ya kodi na ilisaidia.

Alisema hapa nchini “ni barua tu kutoka kwa rais kuwaelekeza wenye migodi.”
Kuhusu uamuzi huo kutafsiriwa kuwa Tanzania ni kigeugeu kwa wawekezaji alisema, “Hakuna kigeugeu. Ni suala la kuelekezana.

Kutolipa kodi hii si sehemu ya mkataba wa wawekezaji na serikali.
“Nchi zao ndio zimepunguza misaada lakini kampuni kutoka nchi hizo ndizo zinatengeneza faida kubwa hapa nchini; kwa hiyo ni kuelekezana.

Kama sisi tuliwasaidia kutolipa kodi ili biashara iwe nzuri kwa nini wasisaidie wakati huu biashara yao imekua,” amehoji Semboja.

Alisema serikali ikichukua mkondo huo, inaweza kupata dola 250 milioni ambazo wafadhili wamepunguza.

Taarifa ya waziri kwa kamati ya bunge inaonyesha jinsi serikali ilivyo na matumizi makubwa ya kawaida. Takwimu zinaonyesha matumizi ya kawaida ya serikali yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.

Kwa mfano, mwaka 2007 matumizi ya kawaida yalikuwa asilimia 14.9 ya pato la taifa; mwaka 2008 yakawa asilimia 17.7; mwaka 2009 ikawa asilimia 21.5.

Makadirio ya sasa yanaonyesha mwakani matumizi ya kawaida yatakuwa asilimia 22.7 ya pato la taifa.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha uliokwisha, matumizi makubwa ya serikali yako kwenye malipo ya posho, masurufu ya safari za nje na ununuzi na utunzaji wa magari ya kifahari ya serikali.

Katika hali ambayo haijaweza kuelezwa hata na serikali yenyewe, kiasi cha fedha kilichopangwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida, kimezidi kile kinachokusanywa na serikali yenyewe.

Hii ina maana kwamba serikali italazimika kutumia hata fedha za mikopo, misaada kutoka kwa wafadhili na michango mingine ya wahisani kugharamia matumizi yake ya kawaida.

Hata hivyo, baadhi ya ofisi za serikali zimetengewa fedha nyingi ikilinganishwa na zile ambazo ni uti wa mgongo wa taifa.

Kwa mfano, kwa mujibu wa jedwali la sura ya bajeti, Kiambatisho B1, ofisi ya Rais Ikulu, imetengewa kiasi cha Sh. 171 bilioni, wakati Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inayosimamia mradi mkuu wa “Kilimo Kwanza,” imetengewa Sh. 103.7 bilioni.

Bajeti ya mwaka huu inakuja wakati deni la taifa limeongezeka kutoka Sh. 5 trilioni miaka minne iliyopita hadi Sh. 10.6 tirilioni hivi sasa.

Ripoti ya Mkullo kwa Kamati ya Bunge inaonyesha kuwa Tanzania imeporomoka katika vigezo vya urahisi wa kufanya biashara duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya 126 mwaka 2008 hadi 131 mwaka 2009.
Vigezo hivyo vya urahisi wa kufanya biashara hupangwa na Benki ya Dunia (WB)
Ripoti ya Mkullo inaonyesha kuwa Tanzania imepitwa na nchi nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwamo Rwanda.

Nchi hiyo ambayo ilikuwa imeingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka mitatu, kabla ya kukumbwa na mauaji ya halaiki ya mwaka 1994, inashika nafasi ya 26 kwa ubora duniani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: