Bajeti za woga wa maisha sasa basi


editor's picture

Na editor - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KESHO serikali inawasilisha bajeti yake bungeni. Kama kawaida, wananchi wataelekeza masikio yao Dodoma.

Bajeti huweka wananchi roho juu. Hukaa wakitegemea kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali kama soda, bia na sigara.

Wakati mwingine hurushiwa bomu; pale wanapoelezwa kuwa bei ya mafuta – ya petroli, dizeli na taa, imepanda kutoka juu kwenda juu zaidi.

Mara nyingi basi, bajeti ni balaa kuliko faraja. Tarakimu nyingi kama Sh. 15 trilioni mwaka huu, ni ngumu kueleweka, hata kusomeka pale zinapokuwa zimeandikwa kwa sifuri zote; lakini hazina maana kwa wananchi.

Kile ambacho wananchi wanatarajia kwenye bajeti – ziwe milioni, bilioni au trilioni kama sasa – siyo ukubwa na urefu wa tarakimu.

Mwananchi mmojammoja anataka kuona maisha yake kama yatabadilika kutoka yalivyokuwa jana. Kama ataweza kuhama kutoka kula mlo mmoja hadi miwili kwa siku.

Kama atapata karo kwa watoto wake wawili. Kama atakwenda hospitali na kukuta dawa. Kama ataweza kulipa nauli katika mabasi ili aende kazini au kuhemea.

Mkulima mmojammoja anataka kuona katika bajeti, kushuka kwa gharama ya pembejeo na uhakika wa kupanda kwa bei ya mazao yake.

Wananchi wanasikiliza hotuba ya bajeti kuona iwapo sasa wanaweza kujenga angalau vibanda vya bati; pale gharama ya bati itakaposhuka au itakapowekewa kiasi fulani cha ruzuku kutoka serikali au makampuni yanayochuma raslimali za taifa kila siku.

Lakini mwaka hadi mwaka, bajeti zimekuwa katili. Wakati mwingine zimekuwa mahali pa serikali kutambia kuwa itapata fedha nyingi kwa kodi na misaada.

Bajeti zimekuwa sehemu ya siasa – mahali pa kufanyia ahadi nyingine kama wakati wa kampeni za uchaguzi.

Tunajua fika kwamba bajeti iko tayari. Kinachosomwa kesho ni kiporo. Basi angalau wananchi wapate, katika kiporo hicho, afueni inayoleta matumaini kwa maisha yao na familia zao.

Haileti maana yoyote kuleta bajeti, mwaka hadi mwaka, ambayo inakuwa kitanzi kwa wananchi na kuwaongezea woga wa maisha badala ya faraja na matumaini. Tuone ya kesho.

0
No votes yet