Ban Ki-Moon aondoka kapa

- Waandishi walidodosa ya nje tu
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ameondoka nchini baada ya ziara yake ya kihistoria bila kujua mambo mengi yanayoikabili Tanzania.
Mwanadiplomasia huyu raia wa Korea Kusini, ameeleza mengi katika mazungumzo yake ya faragha na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete yaliyofanyika Ikulu, na kwenye mikutano ya wazi na watu wengine.
Alipotoa mhadhara hotelini Movenpick, Alhamisi, alieleza mambo mengi kama matatizo yanayoikabili dunia. Alitaja mabadiliko ya hali ya hewa; mgogoro wa Mashariki ya Kati na aliyoyaona alipotembelea Ukanda wa Gaza.
Alitaja mgogoro wa Sudan Kusini unaohusisha machafuko yaliyoko jimbo la Darfur ambako wanamgambo wanapigana na utawala wa Rais Omar Al Bashir; akataja migogoro kadhaa inayoitafuna Afrika na hatua za kuitatua.
Ki-moon ametaja changamoto zinazokabili Umoja wa Afrika (AU) katika utatuzi wa migogoro ya nchi wanachama wake; Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwenye vita na Guinea na Mauritania kwenye tawala za kijeshi.
Aligusia mifano ya mafanikio ndani ya Afrika. Akazungumzia misingi muhimu ya kuwepo kwa Umoja wa Mataifa: Amani, Usalama na Haki; Uwajibikaji; Utawala Bora na Utawala wa Sheria.
“Haya mambo ni ya lazima (hayana mbadala). Lazima yapiganiwe vilivyo na kulindwa kijasiri. Hayapaswi kuchezewa kwa namna yoyote ile,” alisema.
Aligusia malengo ya milenia yanayotiliwa mkazo na UN. Ni hapa ameisifia Tanzania inavyopiga hatua, hususan katika eneo la elimu. Anatambua mafanikio ya uandikishaji watoto wa kuanza mkondo wa elimu.
Ki-moon sasa anataja changamoto kwa Tanzania, akisema “Tunajitahidi kuisaidia serikali (ili) iimarishe utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa; ikabiliane na tatizo la mabadiliko ya hali hewa, mazingira machafu na uhaba wa chakula.
“Tunashirikiana ili iimarishe huduma za afya na elimu za maelfu ya watu wake wa hali za chini.” Alisema anaamini kuna ushirikiano madhubuti na wa mfano katika maeneo hayo.
Ki-moon alifika Zanzibar na kukutana na Rais Amani Abeid Karume. Hakuna taarifa juu ya walichozungumza.
Nachukulia Ki-moon anajua Zanzibar. Kama si kwa vielelezo vilivyoko UN, basi kwa kusoma. Tuamini anajua ni nchi ya visiwa na sehemu muhimu ya Jamhuri ya Muungano.
Anajua ilikuwa taifa lenye kiti kwenye Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1963 ilipoundwa Serikali ya Uhuru. Itakuwa anajua hali halisi ya Zanzibar.
Ninaamini Ki-moon, kama mwakilishi wake aliyepo Tanzania, Oscar-Fernando Taranco hakudanganya, anajua wapo Wazanzibari waliompelekea malalamiko ya hali mbaya ya kisiasa iliyoko Zanzibar na namna inavyoathiri vibaya jamii.
Wapo wazee kutoka kisiwa cha Pemba walioanzisha mawasiliano na ofisi ya UN jijini Dar es Salaam kiasi cha mwaka sasa. Kiongozi wao, Hamad Ali Mussa ana barua ya majibu ya Ki-moon baada ya kupokea malalamiko yao.
Kwa kuona hakuna hatua zaidi, Mzee Hamad alitaka kuonana na Ki-moon ili kukazia hatua za utatuzi. Nia ya wazee ni kurekebisha siasa nchini ili hatimaye kuhakikisha “Amani, Usalama na Haki” – mambo muhimu aliyoyaeleza Ki-moon katika mhadhara – yanastawi. Na hiyo ndiyo kazi ya msingi ya UN.
Kwa bahati mbaya sana, Ki-moon hakugusia suala hili alipotoa mhadhara wala alipokutana na waandishi wa habari hotelini Kempinski. Bahati mbaya zaidi, nilipojiandaa kuuliza swala hili, na jingine linalohusu ofisi kuu ya UN mjini Nairobi, baada ya kuona mbinu za serikali kuzuia wazee kumuona Ki-moon, sikupata nafasi.
Kinachouma zaidi ni waandishi waliopata nafasi kushindwa kuuliza haya. Sikushangaa kwa sababu najua kati ya waandishi wa Tanzania, ni wachache mno wanaotambua tatizo la Zanzibar na kukerwa nalo.
Wengi wanajua kinachofanyika wakati wa uchaguzi Zanzibar, lakini wanajisikia tu hawana wajibu wa kupigia kelele ushenzi dhidi ya demokrasia. Ila wanakuwa mbele kuulizia masuala ya Darfur, Somalia na DRC.
Mwandishi angeuliza angalau msimamo wa Ki-moon katika mgogoro na njama za baadhi ya watendaji katika Ofisi Kuu za UN mjini Nairobi (UNON) za kutaka Mkurugenzi Mtendaji wa UN-HABITAT, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa UNON, aondolewe kwenye nafasi yake hata kabla ya kumaliza muda wake wa mkataba hadi mwaka 2010.
Mambo haya ndio muhimu kwa Tanzania. Najua umuhimu wa masuala ya DRC, Rwanda, Burundi na Sudan, lakini wa kuyaulizia hayo si Watanzania tu peke yao. Wenyewe wana matatizo mengi ya kutakia utatuzi na misimamo ya UN.
Hivi wenzangu hawaamini uchaguzi wetu unatatizwa sana na rushwa? Hawaamini upo mgogoro Zanzibar? Hawajiulizi kilichomsukuma Rais Kikwete kuahidi, alipozindua Bunge Desemba 2005, kuwa atahangaikia ufumbuzi wa “mpasuko wa Zanzibar?”
Kilichokwishafanyika hata kukwamisha ufumbuzi huo na kilichotengenezwa kukaribia ziara ya Ki-moon ni muendelezo wa mbinu za serikali ya CCM kukwepa majukumu yake muhimu. Kusaidia matakwa hayo, si jukumu la mwandishi wa habari.
Siku mbili kabla ya kuwasili kwa Ki-moon nchini, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe alitangaza hadharani kuwa kuna kikundi kimepanga kuhujumu ziara ya Ki-moon.
Hakutafuna maneno. Alisema wazee wa Pemba wanataka kuharibu ziara. Kauli yake ilikuwa na maana nyingi. Moja ni kutuma vyombo vya ulinzi na usalama viwashughulikie.
Maana yake alikuwa anataka Watanzania waamini wazee hawa ni watu waovu wanaotaka kuhujumu serikali. Hivi si ni wazee hawahawa wamekuwa na mawasiliano na UN walipoanza kutuma malalamiko yao kwa Mwakilishi Mkazi wa UN nchini, Taranco?
Serikali ya CCM isiyopenda kutatua matatizo yake makubwa ya kisiasa bali kujipendekeza kwa matatizo ya wengine, iliwasakama kwa kutuma Jeshi la Polisi kuwatisha.
Viongozi wa CCM wakapiga chapuo kwa kuwaita wahaini. Polisi ikawakamata usiku wa manane majumbani kwao kama ni magaidi. Ikawapeleka Unguja kwa kuwahoji hadi usiku wa manane. Baadaye ikawapeleka gerezani Kiinuamiguu.
Hadi leo hawajashitakiwa mahakamani, kudhihirisha hawajatenda kosa lolote. Hakuna mashitaka; huo ndio mfumo wa serikali: “kutisha raia zake.”
Inashangaza kwamba CCM haijali madhila yanayowafika Watanzania. Mbaya zaidi inajenga mikakati ya kubaki madarakani hata ikibidi kuua.
Wazanzibari wamechoka kudhalilishwa na hawawezi kuendelea kufanywa njia ya watu kupata misaada na kujikweza kwenye jumuiya ya kimataifa. Wanachotaka ni kutambuliwa ubinadamu wao na haki zao za msingi.
Kuchagua viongozi wawatakao ni moja ya haki hizi. Waachiwe tu wachague na maamuzi yao yaheshimiwe. Hiyo ndiyo demokrasia na ndivyo watawala watatunza “Amani, Usalama na Haki” – misingi ya kuharakisha maendeleo.
Vinginevyo, watawala wanaringa kwa kustawisha demokrasia isiyokuwepo.