Ban Ki-Moon lawamani


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 31 March 2009

Printer-friendly versionSend to friend

HIVI inawezekana Afrika haikujua thamani ya mtoto, mtumishi na mwakilishi wao kiasi kwamba lolote litakalompata inakuwa, “potelea mbali?”

Kuondolewa kwa Profesa Anna Tibaijuka, kutoka kwenye nafasi yake ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON), na kimya cha Afrika kilichofuatia, ni aibu kubwa kwa uongozi wa nchi za bara hili.

Tibaijuka aliteuliwa na Katibu Mkuu wa zamani wa UN, Kofi A. Annan kupita barua yake ya 13th Septemba 2006, kushika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu, UNON.

Nafasi hiyo ilikuwa inakwenda sambamba na ile ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UN-HABITAT), na zote zinaisha tarehe 31st Agosti 2010.

Lakini Ban Ki-Moon, katibu mkuu mpya wa UN amesitisha uteuzi wa Tibaijuka kuanzia 1 Machi 2009 bila sababu yoyote ya msingi, kufuatana na taratibu na miongozo ya UN.

Kinachosikitisha ni kwamba mataifa yameshindwa kumlaani; na Afrika imeonyesha udhaifu na mapungufu makubwa.

Kwa mujibu wa kanuni, ofisi za UN, ikiwemo hii ya Nairobi (nje ya makao makuu ya New York), huongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa kiwango cha Katibu Mkuu Mwandamizi.

Kwa upande wa kituo na Ofisi ya Nairobi (UNON) ambako kuna wakuu wawili, mmoja wa UN-HABITAT na mwingine wa UNEP, ni yule mwandamizi, kwa mujibu wa utumishi katika umoja huo, ambaye anashika nafasi ya UNON.

Mwandamizi amekuwa Tibaijuka ambaye yumo katika mfumo wa UN kwa miaka tisa (9) sasa na ndiye amekuwa akiendesha UNON tangu 2006.

Sasa, kwa kikiuka misingi ya ukuu na utendaji, Ban Ki-Moon amemwondoa mwandamizi na nafasi yake kupewa wa chini yake. Aliyepewa nafasi ya Tibaijuka ni Achim Steiner anayeongoza UNEP, uteuzi uliopingwa kwa maandamano ya wafanyakazi wa UNON.

Katika barua yake kwa Katibu Mkuu, rais wa chama cha wafanyakazi UNON, Rhoda Atana anasema, “…Tibaijuka ni mwanamke pekee hadi sasa kuteuliwa kushika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha UN…Tunaamini kuondolewa kwake ni kinyume cha misingi ya usawa kijinsia…Kama unavyojua, ofisi za Geneva na Vienna zinaendeshwa na wanaume.”

Hata hivyo, Ki-Moon ambaye makao makuu UN sasa anaitwa “kiziwi wa diplomasia” au mtu anayeshauriwa vibaya, hakujibu barua hiyo ya 26 Februari 2006, kama ambavyo hakufanya kwa mapendekezo kutoka watu mbalimbali. Naye msemaji wake anasema “Katibu Mkuu anataka kuanzisha utaratibu mpya wa kupokezana ukuu wa UNON.”

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Katibu Mkuu mwandamizi (Utumishi), Angela Kane, amejikuta akihusishwa kwenye mpango wa kumwondoa Tibaijuka. Huyu ni Mjerumani na aliyechukua nafasi ya Tibaijuka ni Mjerumani, Achim Steiner.

Ukimya wa Ki-Moon, sasa unahusishwa na mahusiano ya kiofisi unaozaa maswali mengi. Kwanza, kama shabaha ni kupokezana nafasi UNON, kwa nini isisubiriwe hadi uteuzi wa Tibaijuka uishe – ambao ni mwaka kesho?

Pili, kuna taarifa kwamba serikali ya Kenya, ambako kuna makao makuu ya UNON, ilitaka awepo Mkurugenzi Mtendaji asiyehusika na UN-HABITAT wala UNEP na kwamba Ki-Moon aliishakubaliana na wazo hilo.

Hii inatokana na watawala Kenya kuchukia jinsi Tibaigana alivyobaki na msimamo, bila kuunga mkono upande mojawapo katika mgogoro wa uchaguzi wa nchi hiyo.

Ni msimamo wa Tibaijuka ulioipa heshima UN. Hata kushiriki kwa Kofi Annan katika usuluhishi ulioambatana na ugawanyaji madaraka, ulifanikiwa kwa kuwa Tibaijuka alikuwa amechukua msimamo wa kutoingiza UN katika ugomvi wa vyama viwili vikuu vya siasa.

Je, kwa nini sasa asiletwe mkurugenzi anayejitegemea, nje ya mfumo wa sasa, bila kumteua “bwana-mdogo” kumkulia mwandamizi? Kwa nini hili lisisubiri mwenye nafasi hiyo kumaliza muda wake?

Tatu, uteuzi wa Ki-Moon unamwondoa Mwafrika na kumweka Mjerumani, tena wa ngazi ya chini kiutendaji katika mfumo wa UN.

Nne, uteuzi wa Ki-Moon unamwondoa mwanamke na kumweka mwanaume. Hii, katika hali ya kawaida, isingekuwa hoja. Inakuwa hoja kwa kuwa aliyeteuliwa ni “bwana-mdogo” kimfumo wa utendaji UN akilinganishwa na Tibaijuka.

Tano, ni Tibaijuka aliyejenga hadhi ya UN-HABITAT tangu mwaka 2000 alipoteuliwa na kuthibitishwa na Baraza la UN; kufaulu kuondoa shirika hilo katika tope la matumizi mabaya, na hadi kilele cha kuthaminiwa na wafadhili wote wa shirika hilo.

Kwa kazi hiyo na nyingine, Kofi Annan alitambua uwezo wake na kumpa wadhifa mwingine wa kukalia ofisi ya UN Afrika, mjini Nairobi. Leo hii Tibaijuka anachukuliwa kuwa miongoni mwa mifano bora ya utendaji unaokubalika kwa wengi wanaojali maendeleo ya UN.

Mwanamke huyu alikubalika hata mitaani Nairobi, hasa pale alipojitambulisha na walalahoi karibu milioni moja wa kitongoji cha Kibera ambako aliapa kuweka mipango ya kugeuza dhiki zao kuwa faraja.

Francis Atwoli, Katibu Mkuu wa Chama Kikuu cha Wafanyakazi Kenya (COTU) anasema chama chao kinapinga kuondolewa kwa Tibaijuka.

“Kazi ya Tibaijuka pale UNON imekuwa ya mfano…Kinachoonekana dhahiri kuwa sababu ya kumwondoa, ni ubaguzi kwa Mwafrika na mwanamke.

“Tunapinga vikali mfumo uliopitwa na wakati wa ubaguzi wa rangi katika ofisi za Umoja wa Mataifa, ambako watu hawaajiriwi kutokana na sifa za utendaji na uwezo wao, bali kwa rangi na jinsia zao,” amesema Atwoli katika taarifa maalum ya 12 Machi 2009.

Alikuwa Marcos G. Namashulua, Balozi wa Msumbiji, mwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo katika UN-HABITAT na UNEP mjini Nairobi aliyeona bundi mapema.

Katika barua yake ya 4 November 2008 kwa balozi wa Mauritius kwenye UN, iliyosambazwa kwa mabalozi wengine na nakala kwenda kwa Katibu Mkuu, alisema hatua ambayo Ki-Moon anataka kuchukua italeta mgongano, kutoaminiana na kupunguza tija.

Katika waraka mwingine wa 26 Februari 2008, kwa Ki-Moon, Namashulua anasema, “Kama hujaunda ofisi ya Mkurugenzi Mkuu inayojitegemea, tunakushauri kwa dhati ubakize mambo kama yalivyo mpaka Mkurugenzi Mtendaji wa sasa atakapomaliza muda wake 2010.”

Wakati wote huu, hakuna popote pale ambako sauti ya Tanzania ilisikika ikitetea haki ya mwananchi wake dhidi ya uamuzi batili unaovunja misingi ya utendaji UN.

Hatua ya Ki-Moon, siyo tu inadhalilisha watendaji wazuri waliopata nafasi zao kwa kustahili, bali inamomonyoa pia hadhi ya ofisi ya Katibu Mkuu na umoja huo kwa ujumla.

Kama hilo linaweza kutokea kwa mwanamke wa uwezo wa Tibaijuka, Katibu Mkuu Mwandamizi, wangapi ngazi za chini watatendewa mazonge na kutupwa nje ya ajira?

Wakati Tibaijuka anaendelea na nafasi yake ya Katibu Mkuu Mwandamizi wa UN-HABITAT inayofikia ukomo mwaka kesho, Ban Ki-Moon anadaiwa. Anadaiwa maelezo rasmi: Kwa nini amevunja misingi ya utumishi UN?

0
No votes yet