Banda amfuta kazi IGP wa Malawi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

TAKRIBAN saa 24 tangu aliyekuwa Makamu wa Rais, Joyce Banda aapishwe kuwa Rais wa Malawi kuchukua nafasi ya hayati Bingu wa Mutharika, amemtupia virago Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

IGP aliyeondolewa, Peter Mukhitho aliyekuwa wakati fulani mpambe wa Mutharika, amekuwa kiongozi wa kwanza kutupwa nje na nafasi yake imechukuliwa na Loti Dzonzi.

“Rais amemteua Kamishna Loti Dzonzi kuwa IGP mpya wa polisi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Dzonzi amekuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi tangu mwaka 1987 na uteuzi wake unatarajiwa kuthibitishwa na Kamati ya Bunge ya Uteuzi wa Umma.

Taswira ya Mukhitho ilichafuka baada ya jeshi la polisi kuua takriban watu 20 walioandamana nchi nzima 20 Julai 2011 kupinga serikali ya Mutharika. Mbali ya polisi kuua, viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani na asasi za kiraia walitiwa ndani.

Katika hali nyingine, wanasiasa na wafanyabiashara ambao walikuwa wafuasi wa Mutharika wameahidi wazi kumuunga mkono Rais Banda.

Chama tawala cha Democratic Progressive Party (DPP), kilichoasisiwa na Mutharika kimepata pigo kwani wanachama wake wengi wamehama tangu siku Banda alipokabidhiwa madaraka na wabunge wamekuwa wakijiunga na chama cha People’s Party kilichoanzishwa mwaka jana na Banda.

Hata hivyo hatua hiyo imeshangaza watu kwa sababu, katika hotuba yake baada ya kuapishwa alisema kuwa hakutakuwa na nafasi ya kulipiza kisasi.

Wachunguzi wa masuala ya siasa wamesema hatua hiyo ya Banda, mwanamke wa pili kuwa rais barani Afrika ina lengo la “kusafisha” safu ya uongozi. Rais wa kwanza mwanamke ni Hellen Johnson wa Liberia.

Asasi zinazoshughulikia haki za binadamu zimepokea hatua hiyo kwa furaha.

IGP Mukhito, ambaye aliteuliwa na Mutharika miaka miwili iliyopita, alikuwa anashutumiwa kwa kusimamia jeshi lililokuwa likisababisha hofu, kukamata watu, kutia ndani na kuua watu 19 waliokuwa wanaandamana kupinga sera za serikali mwaka jana.

Wapona Kita, mwanasheria wa haki za binadamu ambaye amewahi kumwakilisha Banda miaka ya nyuma alisema: "Hiki ndicho tumekuwa tukikisubiri muda wote. Tulikuwa tunahitaji polisi wenye mipango, thabiti na wanaofuata katiba na kuheshimu haki za binadamu.”

Lakini chini ya Mutharika na Mukhito, Kita alisema “taifa lilikuwa na hofu kuu. Hatukuwa na uhakika wa kitakachotokea siku inayofuata tulipoamka. Kulikuwa na kukamatwa na kuwekwa ndani kinyume cha taratibu na ukandamizaji wa haki za binadamu.”

Kita alisema alikula chakula cha mchana na Banda baada ya mwanamke huyo kuwa rais na ana imani na mustakbali wa nchi.

"Hali ya hewa ya haki za binadamu itaboreka. Kuna uwezekano mkubwa wa kuwa huru katika nchi yetu. Watu watakuwa huru kujieleza na hicho ndicho hasa tulikuwa tunahitaji," alisema.

Mtazamo wake uliungwa mkono na Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu na Urekebishaji Tabia, Undule Mwakasungula.

"Tumekuwa na hofu muda wote namna Peter Mukhito alivyojiheshimu," alisema. "Aliathiriwa na wanasiasa na akaishia kudhalilisha taaluma yake. Tunaamini Lot Dzonzi atarejesha sura ya zamani ya jeshi la polisi. Tunataka polisi wa watu siyo polisi wa wanasiasa."

Taarifa kutoka Ikulu na Baraza la Mawaziri ilisema Rais Banda ametumia mamlaka yake kama Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama wa Malawi kumteua IGP mpya.

0
No votes yet