Baraza la mawaziri ‘kuvunjwa’


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 17 August 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete anaweza kuvunja baraza la mawaziri wakati wowote, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema baraza linaweza kuvunjwa baada ya kumalizika mkutano wa bunge la bajeti, 26 Agosti 2011.

Zikinukuu walioko ndani ya serikali na waliokaribu na Rais Kikwete, taarifa zinasema, hatua ya kuvunja baraza la mawaziri na kuliunda upya inalenga kurejesha hadhi, ufanisi na uwajibikaji serikalini.

Mtoa taarifa anasema hatua ya rais ya kutaka kuvunja baraza la mawaziri au kufanya mabadiliko makubwa, inatokana na mdororo katika utendaji serikalini.

Iwapo hilo litafanyika, basi lililompata Edward Lowassa laweza kumkumba waziri mkuu Mizengo Pinda kwani rais aweza kutomrudisha kwenye nafasi yake.

Miongoni mwa sababu ni serikali kushutumiwa na wananchi na vyama vya upinzani kwa kutotenda; hasa kutochukua maamuzi mazito dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi.

Sababu nyingine ni kutofikiwa kwa malengo ya serikali ya Kikwete ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania; jambo ambalo yeye na viongozi wake wengine wanakiri “kuna mahali tumepotoka.”

Kile kinachoitwa ulegelege na kutotenda kimeelekezwa kwa rais Kikwete ambaye taarifa zinasema kwa vile siyo pekee katika utendaji ndani ya serikali yake, afadhali aunde timu mpya itakayokuwa na upya wa mawazo na msukumo katika kuleta mabadiliko haraka.

Rais Kikwete amebakiwa na miaka minne ya ngwe yake ya pili ya utawala kikatiba. “Kama atafanya mabadiliko sasa, aweza kurekebisha sura na hadhi ya chama chake na serikali,” ameeleza mmoja wa mawaziri waandamizi.

Kumong’onyoka kwa hadhi ya serikali ya Rais Kikwete kumetokana pia na tabia ya baadhi ya mawaziri wake kutotenda kama walivyotarajiwa.

Baadhi ya mawaziri wanatuhumiwa kutumia madaraka yao vibaya; kujiingiza katika mambo ambayo hayahusiani na nyadhifa zao na kushindwa kuitetea serikali, kama ilivyodhirika bungeni ambako bajeti za wizara zimekuwa zikipita kwa mbinde.

Aidha, udhaifu wa serikali ambao wachunguzi wanataja Rais Kikwete anataka kukabili, ni kutokana na tishio la wafanyabiashara ya mafuta ambao wiki mbili zilizopita walionyesha “kuiweka serikali kitanzini.”

“Hili ni moja ya mambo makubwa. Sharti sasa uhusiano kati ya wafanyabishara na serikali uangaliwe upya, vinginevyo wataichezea serikali na hata kutishia uhalali wake,” ameeleza waziri huyo.

Kwa karibu wiki nzima, makampuni ya wauza mafuta yaliigomea serikali kuteremsha bei ya mafuta ya taa, dizeli na petroli na kufikia hatua ya kuipa masharti kuondoa amri yake.

Hata kampuni ambamo serikali ina hisa asilimia 50 (BP) imeikomalia serikali hadi ikafungiwa kuuza mafuta kwa rejareja. Imeruhusiwa kuuza mafuta yake kwa makampuni mengine ya mafuta yaliyokubaliana na serikali.

Ukaidi wa makampuni ya mafuta umeiweka serikali pabaya na hasa kuidhalilisha mbele ya wananchi na jumuia ya kimataifa. “Sasa kama serikali yetu inatunishiwa msuli na vikampuni, sisi nani atatutetea; nani atatulinda,” ameuliza Salum Juma mwendesha taxi wa Mtaa wa Kasaba, Kindondoni jijini Dar es Salaam.

Kitu kingine kilichoiweka serikali pabaya ni tuhuma kuwa mawaziri wawili wa Rais Kikwete wamejihusisha katika miradi binafsi kwa mgongo wa serikali.

Wanaotajwa ni waziri wa utawala bora, Mathias Chikawe na naibu waziri wa nishati na madini, Adam Malima; kwamba wako mbioni kuingiza nchi katika mikataba mitatu mikubwa ya kinyonyaji.

Tangu taarifa hizi zichapishwe katika toleo la gazeti hili wiki iliyopita, si Malima, Chikawe wala serikali imetoa taarifa kuhusu suala hilo.

Malima anatajwa katika kufanikisha kufungwa kwa mkataba wa uchimbaji madini ya shaba (Copper) wilayani Mpanda mkoani Rukwa kinyume cha taratibu.

Naye Chikawe anadaiwa kuwa mbioni kufanikisha biashara kubwa ya dawa za virutubisho vya binadamu kwa wagonjwa wa HIV – Secoment V.

Katika miradi hiyo, Malima na Chikawe wanatuhumiwa kutaka kutumia mamlaka ya serikali kujinufaisha binafsi.

Malima alipoulizwa kuhusu suala hilo, Jumapili iliyopita alisema, “Niko kazini na watendaji wa wizara yangu. Nashughulikia masuala ya bunge kesho (juzi Jumatatu).” Aliomba apelekewe maswali.

Hata hivyo, pamoja na gazeti kumpelekea maswali, Malima hakuyatolea majibu hadi gazeti lilipokwenda mtamboni.

Malima anadaiwa kutumia majina tofauti kuficha utambulisho wake katika mikataba yake nchini Afrika Kusini. Badala ya kuitwa Adam Kigoma Malima, mshirika wake anamtambulisha hotelini na kwenye uwanja wa ndege kuwa ni Johan Ernest Malima.

MwanaHALISI lilitaka kujua kwa nini alibadilisha majina yake, kwa mujibu wa mawasiliano kati yake na mkurugenzi wa kampuni ya Lions of Africa ya Afrika Kusini, Bw. Abdurrazak Ebrahim.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, Malima alisafiri hadi nchini Afrika Kusini kwa gharama za Abdurrazak Ebrahim anayetajwa kuwa bingwa wa ushawishi. Katika safari hiyo kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (hadi Cape Town), Malima alilipiwa gharama zote na Ebrahim.

Akiwa nchini humo alifikia katika hoteli ya kimataifa ya Michelangelo. Ziara ya Malima nchini humo ililenga kufanikisha mradi wa kuipa kazi ya kuchimba shaba kampuni ya Lions of Africa Holdings (LAH).

Kampuni ya LAH inajitambulisha katika mawasiliano yake ya intaneti kuwa ni moja ya makampuni makubwa nchini humo; inajishughulisha na uwekezaji katika masuala ya madini na bima. Makao yake makuu yako Cape Town. Ofisi zake nyingine ziko Johannesburg.

Naye Chikawe alipohojiwa kuhusu biashara hiyo ya dawa alisema, “Ningependa kuzungumza na mwandishi ana kwa ana.” Alisema hawezi kuzungumza pia kwa kuwa hajasoma gazeti kwa vile alikuwa nje ya nchi kikazi.

Mradi wa virutubisho unashirikisha makampuni ya Andrew Gaskell, Sean Gaskell na Lion of Africa. Wabia wamekubaliana katika mkataba wao uliosainiwa 14 Machi 2011, kwamba kila upande utapata gawio la asilimia 50 ya mradi.

Wachunguzi wa mamabo ya kisiasa wanahoji, “Kama kweli mawaziri hawa wanafanya shughuli zao kwa kutumia mgongo wa serikali; ni wangapi wengine wanafanya hivyo katika serikali ya Rais Kikwete?”

Hili nalo linalegeza misuli ya serikali ya Kikwete, kimnyima usingizi na kusababisha afikirie kuvunja baraza la mawaziri na kuunda jipya la kumvusha hadi mwishoni mwa ngwe yake, Oktoba 2015.

Hata hivyo kuna madai kuwa baadhi ya mawaziri wamechoka ingawa hakuna uthibitisho wowote kuonyesha wamechoka vipi. Bali baadhi wanahusishwa na kutotenda kazi zao ipasavyo; badala yake  wanahaha kusaka urais wa 2015, au kwa kupigia debe maswahiba wao.

Lengo ni kutaka kurejesha hadhi ya serikali mbele ya wananchi na jumuiya ya kimataifa na kurejesha uwajibikaji serikali.”

Udhaifu wa mawaziri unahusishwa na kinachoendelea bungeni, mjini Dodoma ambako katika suala la bajeti za wizara, mawaziri wanalaumiwa ama kwa kutoshirikisha viongozi wao ngazi ya juu au kwa kushindwa kujenga hoja kama ilivyokubaliwa katika vikao vya ndani.

Mapungufu hayo yanaelemea kwa rais ambaye alipaswa kujua ni nini kinahitajika na kutarajiwa. Kushindwa kwa mawaziri kutenda ilivyoamuliwa, kunaleta aibu kwa serikali, kuidhoofisha na kuidhalilisha mbele ya wananchi.

Kwa mfano, hatua ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), kuinglia kati mambo ambayo tayari yameamuliwa na bunge katika bajeti kuu, kunaonyesha kuna ukosefu wa mawasilano ya kiutendaji na kunamwingiza rais moja kwa moja katika kile kinachoitwa uzembe wa serikali wa kutoona mbali.

Ni CC iliyoagiza serikali kutafuta njia ya kupunguza bei ya mafuta ya taa, dizeli na petroli ili kuleta afueni kwa wananchi. Hatua hii ndiyo iliingiza serikali katika mnyukano na wauza mafuta wakubwa nchini.

Aidha, hatua ya wafanyabiashara kukaidi pendekezo na hata amri ya serikali, imechukuliwa na baadhi ya wachambuzi kuwa inaonyesha kuwa huenda ndani ya makampuni hayo kuna viongozi wa ngazi mbalimbali za serikali wanaoongoza ukaidi.

Iwapo Rais Kikwete atavunja baraza la mawaziri, atakuwa rais wa kwanza tangu awamu ya kwanza, kuvunja baraza mara mbili katika kipindi chake cha utawala wa miaka 10.

“Si hivyo. bado ana muda mwingi; miaka minne. Anaweza kuvunja tena na tena kutegemea na anavyotaka kuacha sura ya utawala wake katika historia ya nchi hii,” ameeleza mchambuzi mmoja wa historia ya siasa Tanzania.

0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: