Barua ya JK, IMF yavuja


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 January 2012

Printer-friendly version
Mkullo akana kusaini mkataba

SERIKALI imekana kuidhinisha mpango wa shirika la fedha duniani (IMF) unaotaka kuweka masharti ya ukopaji na urejeshaji fedha katika shirika hilo, imefahamika.

Kwa mujibu wa taarifa mikononi mwa MwanaHALISI mpango huo uwe umeidhinishwa kwa saini tarehe 9 Desemba mwaka jana, au kama saini zingekuwa hazijakamilika, basi tarehe 12 ya mwezi huohuo.

Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo alimwambia mwandishi wa gazeti hili juzi Jumatatu kwa njia ya simu kuwa serikali ya Tazania haijasaini mpango wala mkataba unaolenga, pamoja na mambo mengine, kuweka utaratibu mpya uliobuniwa na wakurugenzi wa IMF.

Mkulo alikiri kwamba alikuwa New York Marekani mwezi Desemba mwaka jana, lakini akakana kushiriki majadiliano yeyote yaliyohusu utaratibu mpya wa nchi kukopa kutoka IMF.

“Mimi sikuhudhuria mkutano wa kujadili au kupigakura juu ya utaratibu mpya wa kukopa. Na kwa kuwa sikuhudhuria, hivyo sikusaini na wala siufahamu mpango au masharti hayo mapya,” alisema Mkulo.

Taarifa kutoka mwakilishi mkazi wa IMF nchini, Wakeman-Linn, John K, zinaonyesha kuwa mwakilishi huyo amekuwa akiwasiliana na Dk. Servacius Likwalile, naibu katibu mkuu hazina.

Katika moja ya mawasiliano yake, mwakilishi anamwambia Dk. Likwalile kuwa zinahitajika nchi 94 kuweka saini za kuwezesha kupitisha alichoita, “utaratibu mpya wa kukopa” na kwamba Tanzania ingesaini makubaliano hayo.

Mapendekezo hayo mapya yamefuatia hatua ya wakurugenzi wa IMF kubuni kile kilichoitwa “taratibu mpya za kukopa.” Katika utaratibu huo wadeni watapewa muda zaidi wa kujaddili jinsdi ya kukopa na kulipa.

Wakeman-Linn katika mawasiliano yake na Dk. Likwalile anathibitisha kuchumbia saini ya Tanzania na kuonyesha kuwa “wala…haihitaji idhini ya Bunge au mlolongo wa taratibu za kiserikali kwa kuwa hayana madhara kwa Tanzania.”

Anasema, “…muhimu ni kwamba haya ni maamuzi ambayo waziri anaweza kuyafanya yeye mwenyewe bila kuhitaji Bunge au taratibu za kiserikali.”

Wakeman-Linn anaekeza itakuwa vizuri zaidi kama waziri (Mustapha Mkulo) atakapokutana na mkurugenzi mtendaji wa IMF, Ms Christine Lagarde, Washgton DC, amjulishe kuwa amekubaliana na uamuzi uliopendekezwa.”

Lakini mjini Dar es Salaam, Mkulo ameendelea kusema, “Sikumbuki kama lilitokea jambo kama hilo kwa kuwa tumezungumza kwenye simu, naomba vilevile ikiwezekana uniandikie ili tuchambue na kuona ni kitu gani hasa ambacho Watanzania wangependa kukifahamu,” alisisitiza.

Mkulo aliondoka Dar es Salaam akiwa na barua ya Rais Jakaya Kikwete kwenda kwa mkurugenzi mkuu mpya wa IMF ambamo anampongeza kwa mara ya pili kwa kushika nafasi hiyo.

Katika barua hiyo pia anasema ana muunga mkono na kuahidi ushirikiano katika kuleta mabadiliko nchini mwake.

Haikufahamika kwa nini rais alikuwa anampongeza mkurugenzi wa IMF kwa mara ya pili, mara hii kwa barua rasmi.

Kabla ya kauli ya Mkulo, gazeti lilimfuata naibu waziri wa fedha, Gregory Teu, kutaka kujua iwapo Tanzania imesaini mpango mpya wa mikopo.

Kwanza alistuka, “Aah!”

Baadaye na taaratibu akaeleza, “Sifahamu hatua ambayo waziri amefikia. Hilo kwa kweli silifahamu. Anayeweza kuelezea kwa kina ni mheshimiwa waziri; kwani alikuwa huko.”

“Alikuwa Marekani na kilichojiri huko anakijua yeye. Na haya mambo yako kwenye pipeline (mkondo) wa mheshimiwa waziri. Mimi na hata mwenzangu Silima (Pereira) hatujui. Halafu kwa utaratibu wa wizara wa sasa na kwa jambo hilo, msemaji ni waziri mwenyewe,” alieleza Teu.

Akiandika kwa kiongozi huyo wa IMF, Rais Kikwete alisema “…nachukua fursa hii kukuandikia barua hii ya kukuomba kukutana na waziri wangu wa fedha na uchumi, mheshimiwa Mustapha Mkulo.”

MwanaHALISI limeelezwa na wachunguzi kuwa hatua ya Rais Kikwete kuandika kwa mtendaji mkuu wa IMF, siku tatu kabla ya muda wa mwisho kuridhia masharti mapya ya ukopaji, yaweza kuwa uthibitisho kwamba alibariki yote yaliofanyika.

Akiandika kwa lugha ya kina, Rais Kikwete alisema, “Nakuahidi ushirikiano wangu binafsi na msaada wangu pamoja na ule wa serikali yangu katika kutekeleza majukumu yako…”

Alisema Tanzania inaamini katika uongozi wake uliyosheheni ujuzi na kwamba anaamini pia kuwa ataiongoza IMF hadi hatua ya juu ya mafanikio.

Katika barua yake, Rais Kikwete anasema serikali yake inatambua mchango wa shirika hilo na kwamba Tanzania inahistoria ndefu ya ushirikiano na IMF.

Anasema, “Natambua kuwa umechukua ofisi katika kipindi hiki kigumu cha uchumi wa dunia na hivyo unahitajika uongozi madhubuti wa IMF.”

Anarejea mahusiano ya Tanzania na shirika hilo ambayo anasema yalikuwa ya mashaka na “kulikuwa na changamoto mbalimbali katika uhusiano huo;” lakini yote hayo anayachukulia kama mambo ya kawaida.

Anasema serikali inashukuru kuona kuwa pamoja na changamoto zilizopo, uchumi duniani umeimarika kutokana na ushauri na msaada wa shirika hilo.

Rais anamaliza barua yake kwa kumkaribisha mkuu mpya wa IMF kutembelea Tanzania wakati wowote atakapopata nafasi.

Utaratibu mpya wa mikopo kutoka IMF unalenga pia kuiondolea Marekani wajibu wa kuchangia mfuko wa mikopo.

Taarifa za IMF zinasema mfuko wa mikopo sasa umeongezeka mara kumi ya ilivyokuwa mwaka 2010, kutoka dola za Marekani 34 bilioni kwa mwaka hadi dola za Marekani 370 bilioni, hivyo kuongeza uwezo wa mfuko wa kukopesha.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: