Baruany: Kiboko cha Abdulaziz


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

SALUM Khafan Nassor Baruany (51), mbunge mteule wa Jimbo la Lindi Mjini, ameweka historia ya kuwa mtu wa kwanza nchini mwenye ulemavu wa ngozi (albino) kushika wadhifa huo kupitia njia ya kuchaguliwa na wananchi.

Baruany amevunja rekodi iliyowekwa mwaka jana na Al-Shymar Kwegyir, ambaye alikuwa mtu wa kwanza mwenye ulemavu huo kuwa mbunge wa Bunge la Tanzania. Hata hivyo, Al-Shymar alipata nafasi hiyo baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kama miongoni mwa wabunge 10 anaoruhusiwa kuwateua kwa mujibu wa Katiba.

Baruany aliingia katika mchujo na baadaye akashiriki kampeni zilizojaa ushindani na kashfa hadi akamshinda aliyekuwa anashikilia kiti hicho kwa miaka 15, Mohamed Abdulaziz kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mbali ya kuwa mbunge, Abdulaziz pia alikuwa mkuu wa mkoa wa Iringa.

Baruany aliyegombea kupitia Chama cha Wananchi (CUF), katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu, aliwania pia nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2005 lakini alishindwa na Abdulaziz kwa tofauti ya kura 3,000.

Katika uchaguzi uliopita, Baruany alipata kura 13372 huku Abdulaziz akipata kura 11450, tofauti ikiwa ni kura 1922 baina ya wagombea hao wawili waliochuana vikali.

Anasema, “Huu si ushindi wangu binafsi. Ni ushindi wa wananchi wa Lindi Mjini ambao wameamua kuchagua mabadiliko na haki sawa kwa wote.

“Huu pia ni ushindi kwa watu wote wenye ulemavu hapa nchini. Ushindi wangu haukuwa kwa sababu ya huruma bali kwa vile nilistahili,” alisema Baruany katika mahojiano jijini Dar es Salaam juzi.

“Nina imani kubwa kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2005, mimi nilishinda lakini tume ikaamua kumpa ushindi Abdulaziz. Mwaka huu nimemshinda kwa mbali sana ndiyo maana ikashindikana hata kuchakachua,” alisema.

Historia
Baruany ni mzaliwa wa kijiji cha Mingoyo kilichopo umbali wa kilomita 24 kutoka Lindi Mjini na ni mtoto wa tano katika familia ya watoto watano wa Mzee Khalfan Nassor.

Mbunge huyo alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mingoyo na alisoma sekondari katika shule ya Mkonge hadi kidato cha nne.

“Mimi nimeishia kidato cha nne kwa sababu ya ukosefu wa fursa zilizokuwapo zamani. Nakumbuka kulikuwapo wanafunzi maalbino wachache sana wakati mimi nikisoma sekondari miaka ya 1970.

“Zile naweza kusema zilikuwa nyakati za giza kwa walemavu. Fursa hizi unazoziona leo kwa walemavu hazikuwapo zamani na hilo lilikuwa kikwazo kikubwa kwangu.

“Na ubaguzi haukuishia kwenye elimu tu. Wenzangu niliomaliza nao kidato cha nne na darasa la saba walikuwa wakipata ajira lakini mimi nilinyimwa kwa sababu ya huu ulemavu wangu.

“Baada ya kuona kwenye elimu sipewi fursa sawa na kwenye ajira pia sitendewi haki, ndipo nikaamua kuwa mjasiriamali na kufanya biashara zangu. Nimefanya biashara hadi nimepata huu ubunge,” anasema.

Baruany si mgeni katika masuala ya siasa. Kwa mara ya kwanza alijiunga na chama cha NCCR-Mageuzi mwaka 1993 na alikuwa mwanachama hadi mwaka 1999 alipohamia chama cha Tanzania Labour (TLP).

Mwanasiasa huyu anasema alihama NCCR kutokana na mgogoro uliokikumba chama hicho na kusababisha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema kukihama na kuhamia TLP.

“Mimi nilikuwa shabiki mkubwa wa Mrema. Alipohama NCCR-Mageuzi, sisi wa mikoani tulibadili tu bendera kwenye matawi yetu kutoka chama hicho na kwenda TLP,” anasema. 

Hata hivyo, mwaka 2000 aliitosa TLP akahamia CUF kwa vile alifurahishwa na kauli mbiu ya chama hicho ya “Haki Sawa kwa Wote.”

Kwa mtu aliyepitia katika manyanyaso na kunyimwa haki kama yeye, kujiunga na chama kinachotetea haki sawa kwa wote lilikuwa ni jambo lisilohitaji akili nyingi.

“Na leo hii nimevuna matunda ya kujiunga na CUF. Kwanza walinichagua kuwa mwenyekiti wa wilaya ya Lindi Mjini na mjumbe wa chombo cha juu kabisa cha maamuzi cha chama yaani Baraza Kuu.

“Halafu wakanipa fursa ya kuwa mgombea ubunge mwaka 2005 na hata baada ya kushindwa wakanipa nafasi nyingine mwaka huu. Wananipa nafasi kwa vile wanaona naweza,” anasema.

Kampeni
Ilidaiwa kwamba katika kipindi cha kampeni, Abdulaziz alishutumiwa kwa kupiga kampeni za kibaguzi dhidi ya Baruany, akiwataka wananchi kutomchagua mgombea huyo wa CUF kwa sababu ya ulemavu wake.

Baruany anazungumziaje kampeni hizi za Abdulaziz?

“Kwanza mimi sikushangazwa na kampeni hizo za Abdulaziz. Mwaka 2005 alitumia mbinu za ubaguzi kwenye kampeni zake na hivyo nilitarajia ataziendeleza tena safari hii,” anasema.

“Nilichofanya ni kujiandaa na mashambulizi yake. Usisahau kwamba mimi ni mtoto wa Lindi. Wapiga kura ni wazazi wangu, dada zangu, kaka zangu, wajomba zangu na marafiki. Kampeni chafu hazisaidii kitu katika mazingira hayo.

“Watu wa Lindi wamekataa ubaguzi dhidi ya walemavu. Huu ndiyo ujumbe ambao nataka Watanzania kwa ujumla wao waupate kwenye ushindi wangu huu,” anasema.

Katika miaka yake mitano ya kwanza kama mbunge, wananchi wa Lindi Mjini wanapaswa kutarajia mabadiliko makubwa katika maisha yao.

“Binafsi siwezi kuwaahidi wananchi maisha ya peponi. Nitafanya kile ambacho wananchi watataka tukifanye. Tutafanya mambo pamoja. Mimi nitakuwa msemaji wao na wao watafanya mambo pamoja na mimi.

“Lindi iko nyuma kielimu na katika huduma mbalimbali za kijamii. Watu wapo na rasilimali nyingine pia zipo. Kinachohitajika ni ushirikishwaji wa wananchi na kusikia wanachokitaka,” anasema.

Kitaifa, Baruany anasema atapigania kuhakikisha kuna ushindani sawia baina ya vyama wakati wa uchaguzi, kuwepo kwa Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: