Batilda, Mrema waigawa CCM Arusha

HARAKATI za kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu mwakani zimeanza katika maeneo mengi hapa nchini, ikiwa ni pamoja na mkoani Arusha.
Katika uchaguzi huo, kuna majimbo ambayo yanatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwenye majimbo mengine upinzani utakuwa ndani ya CCM yenyewe, likiwamo jimbo la Arusha.
Jimbo hilo ni mmoja ya majimbo ambayo upinza mkubwa unatarajiwa kuwa kwa wagombea wawili ndani ya CCM, ambao tayari mitandao yao imeimarika, tayari kwa uchaguzi ujao.
Wagombea hao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia mazingira, Dk. Batilda Buriani na mbunge wa sasa wa Arusha, Felix Mrema.
Tangu Waziri Buriani, ambaye ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Arusha, alipoonyesha nia ya kuwania ubunge wa kuchaguliwa katika jimbo hilo, mgawanyiko mkubwa imekikumba chama hicho.
Mgawanyiko huo unatokana na jinsi makundi ndani ya chama hicho, yalivyojitokeza kuwaunga mkono wagombea hao.
Wakati Dk. Burian anaungwa mkono na kundi kubwa la Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) wilaya ya Arusha, Mrema amekuwa akiungwa mkono na Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT) wilaya ya Arusha.
Ndani ya viongozi wa CCM wilaya ya Arusha, Mrema amekuwa akiungwa mkono, kwa kiasi kikubwa, hasa kutokana na nguvu za swahiba wake mkubwa, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Jubilate Kileo.
Kileo ambaye pia ni diwani wa kata ya Kaloleni manispaa ya Arusha, amekuwa ni nguzo kubwa ya Mrema, hasa kutokana na ushawishi kwa wafanyabiashara wa Arusha kutoka mkoani Kilimanjaro.
Hata hivyo, mtikisiko wa Kileo hivi karibuni, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kinidhamu, la kupokea na kuzigawa pikipiki zilizotolewa na wafanyabiashara kadhaa, akiwamo mtuhumiwa mmoja wa kesi ya Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu (EPA) kumeyumbisha umaarufu wake katika CCM.
Katika sakata hilo, Katibu wa CCM mkoa wa Arusha, Mohamed Mbonde na katibu wa CCM wilaya ya Arusha, Mohamedi Nyawenga wamehamishwa huku Kileo akipewa onyo na vikao vya juu vya CCM.
Sakata hilo lilifikia hatua ngumu. Rais Jakaya Kikwete aligoma kuzigawa pikipiki hizo za makatibu kata wa CCM, baada ya kubaini ilikuwa ni “janja” ya viongozi wa CCM wilaya ya Arusha kutaka kumsafisha mtuhumiwa huyo wa EPA.
Lakini bado Kileo amekuwa na ushawishi mkubwa kwa wafanyabiashara kutoka mkoani Kilimajaro na ndani ya viongozi wa CCM wa kata za Revolosi, Kaloleni, Ngarenaro na Sekei.
Kitendo cha Mwenyekiti wa UV-CCM, wilayani Arusha, Godfrey Mwalusamba, kuonyesha kumuunga mkono Dk Burian, kimefufua matumaini yake ya kuungwa mkono kuwania ubunge.
Mwalusamba awali alikuwa katika kambi ya Mrema. Ameonekana kubadilika na amekuwa mmoja wa wapiga kampeni wakubwa wa Dk. Burian.
Hatua ya kutaka kumng’oa Mwalusamba kwenye nafasi yake hivi karibuni, kilitokana kupokea misaada ya kumuimarisha Dk. Burian. Pia anadaiwa kushinikiza Mrema kuenguliwa ukamanda wa UV-CCM wilaya ya Arusha, mbako kumeonyesha mpasuko katika CCM.
Kwa upande wa UWT, mwenyekiti wilayani Arusha, Judith Ringo, alikuwa kambi ya Dk. Burian. Sasa amejiunga na kambi ya Mrema.
Ringo aliwahi kuwa swahiba mkubwa wa waziri Burian. Amegeuka na nguvu fedha ya kambi ya Mrema, iliyomsaidia kuwa mwenyekiti wa UWT wilayani.
Licha ya Burian kuanza kampeni za chini kwa chini, amekuwa akisita kutangaza kugombea ubunge. Anahofia kukiuka taratibu za kampeni za CCM.
Ushiriki wake katika shughuli za kisiasa na kijamii katika manispaa ya Arusha umetajwa kuwa ni kutaka kuungwa mkono na watu wengi, jambo ambalo amefanikiwa.
Karibu kila mwezi Burian amekuwa akialikwa katika sherehe katika manispaa ya Arusha na nyingi amekuwa akihudhuria. Sherehe hizo zimekuwa zikionekana kumpigia “chapuo” kuwa mbunge.
Kuungwa mkono kunatokana na kuwa karibu na watu. Ni tofauti na Mrema. Amekuwa mbali na wapiga kura. Ameshindwa kuhudhuria kwenye matukio mengi ya kijamii.
Tayari Mrema ametangaza nia ya kutetea ubunge wake. Imekuwa ni kawaida kuupata kwa taabu kila wakati wa uchaguzi.
Katika uchaguzi wa mwaka 1995, 2000 na 2005, Mrema alishinda kwa mbinde. Ni kutokana na upinzani mkubwa kutoka kwa wagombea wa vyama vya upinzani.
Rufani yake ndiyo ilimpa ubunge mwaka 1998. Ni baada ya kubwagwa na aliyekuwa mgombea wa NCCR-Mageuzi wakati huo, Makongoro Nyerere.
Mambo yalikuwa magumu hata katika chaguzi zilizofuata kutoka kwa wagombea wa chama cha Tanzania Labour (TLP).
Ugumu wa ushindi wa Mrema katika chaguzi hizo ndio unaosababisha viongozi wa juu wa CCM kutaka agombee mwana-CCM mwingine katika jimbo la Arusha. Kwamba chaguzi zote zilizopita Mrema alishinda baada ya kutumika nguvu kubwa kupita kiasi.
Kwa vyovyote vile, hali ya sasa ya kisiasa huenda ikasababisha upinzani mkubwa zaidi kwa Mrema. Amekuwa hawezi kujenga hoja vizuri majukwaani na hata bungeni.
Kuendelea kuungwa mkono kwake na viongozi wengine wa CCM kunatokana na hofu ya kulipoteza jimbo la Arusha, kama wafanyabiashara wa mkoa wa Kilimanjaro wataacha kumuunga mkono mgombea wa CCM.
“Nguvu ya Wachaga hapa Arusha hatuwezi kuipuuza. Ndiyo sababu licha ya ugumu wa kumpitisha Mrema, pia tunadhani kutakuwa na ugumu zaidi tukiwa na mgombea ambaye hataungwa mkono na wafanyabiashara hawa,”anasema kada mmoja wa CCM wilaya ya Arusha.
Kwa vyovyote vile, uchaguzi mkuu ujao ndani ya CCM katika jimbo la Arusha utakuwa mgumu na huenda ukasababisha kung’oka kwa Mrema au kuumbuka kwa Waziri, Dk Batilda Burian.