Bendera ataja sababu za kukosa vipaji vipya


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 21 December 2011

Printer-friendly version

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Joel Nkaya Bendera amesema kwamba baadhi ya watendaji serikalini ni kikwazo kikubwa katika juhudi za kuvumbua na kuviendeleza vipaji vipya vya michezo nchini.

Bendera amesema hayo kutokana na uzoefu aliopata kama kocha wa timu ya soka ya taifa, kama mbunge wa Jimbo la Korogwe  Mashariki na kama naibu waziri wa habari, vijana, utamaduni na michezo.

Akifungua mkutano mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Morogoro, Bendera alisema wakati akiwa wizarani, aliona baadhi ya watu kama wanafanya makusudi kutowajibika katika utekelezaji wa majukumu yao kuhakikisha Tanzania inapiga hatua katika michezo ikiwemo kuvumbua vipaji vipya vya michezo kila mwaka.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya soka ya taifa amewataja baadhi ya watendaji hao ambao ameahidi kuwafuatilia kila hatua kuwa maafisa utamaduni na michezo. Kwa uzoefu wake, anaona wengi hawawajibiki ipasavyo katika kuinua michezo.

Sababu kubwa ni kwamba wapo maafisa utamaduni wengi kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa, ambao ama hawana elimu ya michezo au wanakosa ari ya kuhakikisha wanawajibika ipasavyo katika kuinua michezo katika maeneo yao.

Vilevile, wengi wa watendaji hao nchini wapo kinadharia zaidi kuliko utendaji, yaani sawa na mtu anayepewa madaraka halafu hakuna analotekeleza huku akiendelea kupokea mshahara kutoka serikalini. “Hao ndio wanaoua michezo nchini,” anasisitiza.

Bendera amefikia hatua hiyo baada ya kuona wazi, baadhi ya watendaji wa serikali wanaona michezo ni mchezo! Hao hawaamini kama michezo ni ajira kama ilivyo kwa serikali mbalimbali duniani zilizopiga hatua.

“Je, tunaridhika kwamba vijijini, kata, tarafa, wilayani na hata mikoani michezo ipo na inaendeshwa ipasavyo? Nakataa hakuna michezo katika ngazi hizo! Nani anayewajibika kuhakikisha vipaji vinavumbuliwa na kutunzwa ipasavyo?” anahoji Bendera.

Kauli ya Bendera inaungwa mkono na ukweli kwamba, wakati Tanganyika ikitimiza miaka 50 ya Uhuru wake, kwa eneo la Afrika Mashariki, hatuna kikubwa cha kujivunia katika nyanja mbalimbali za michezo.

Katika Michezo ya Olimpiki, Tanzania iliyozaliwa 26 Aprili 1964 baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana, inajivunia medali mbili tu katika medani ya riadha licha ya kujitahidi kushiriki kila inapofanyika.

Baadhi ya wadau wamekuwa wakiwatupia lawama viongozi wa vyama vya michezo vya kitaifa kwamba wanakosa mbinu za kwenda kuibua vipaji ngazi za chini, wengine huwalaumu makocha na baadhi huwatupia lawama wakurugenzi wa ufundi, hasa katika soka.

Bendera anasema, pamoja na kasoro za viongozi wa vyama vya michezo, sera mbovu ya uibuaji na uendelezaji vipaji katika harakati za kukuza na kuendeleza michezo nchini ni sababu kuu.

Maswali ya kujiuliza ni haya, Bendera ameona tatizo, ni wakuu wangapi wa mikoa walioona na hivyo kujitoa kuhakikisha wanasimamia ipasavyo michezo katika mikoa yao? Je, wakuu wangapi wanafuatilia utendaji wa maafisa utamaduni na michezo? Je, si kweli kwamba wengi husubiri kuwa wageni rasmi katika hafla za ufunguzi au ufungaji michezo na ikiwa hawakuitwa hubaki ofisini tu?

Hata wakuu wa mikoa, wengi wapo makini kufuatilia kuona bajeti za miradi mbalimbali zinapitishwa na maendeleo ya sekta nyingine za kiuchumi, lakini si michezo. Baadhi ya wakuu wa mikoa huchangamka wakisikia timu za mikoa yao zimefikia hatua fulani ya michuano ya Kombe la Nyerere.

Tena husikika katika michezo ya soka na netiboli tu lakini si michezo mingine kama mpira wa kikapu, mpira wa wavu na hata ngumi na riadha ambayo walau hutoa wachezaji wa kushiriki michezo kama ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola, Mataifa huru ya Afrika.

Viongozi wa mikoa, wanaoipa kisogo michezo hawana tofauti na wale waliohimiza kufutwa michezo shuleni.

Popote pale duniani, mchezaji mzuri hupatikana kuanzia akiwa chipukizi, huyo atapewa misingi ya mchezo husika na hukua akiwa na akili moja kuhusu mchezo husika, tofauti na sasa ambapo Tanzania inakosa wachezaji walio na misingi katika michezo husika.

Wachezaji waliokosa misingi ya michezo husika, ndio hao wasio na nidhamu uwanjani hata na wakiteuliwa kuwakilisha timu ya taifa, hugoma kwa vile hawana uzalendo. Kwao michezo ni kama mchezo na si kazi.

Je, wakuu wa mikoa wangapi walio na moyo wa kuendeleza au hata kuisemea michezo kama Bendera? Tanzania ina mikoa zaidi ya 26, haingii akilini kama Bendera peke yake ataweza kuinua michezo hata katika mkoa wake, kwani atakumbana na kikwazo cha wanafiki wanaoyumbisha maendeleo ya michezo.

Ni wakati wa serikali kuzalisha na kuwaendeleza maafisa utamaduni waliopo huku ikiwasimamia kwa karibu katika utendaji wao kama afanyavyo Bendera ili kukuza michezo nchini.

Nje ya hapo, tutabaki na watu wanaongoja mishahara huku eneo lao la kazi likidorora. Hao, wala hawaibii serikali, anayeibiwa ni Mtanzania mkarimu anayekubali kulipa kodi ambayo baadaye inageuka mshahara wa mtu huyo.

0713801699
0
No votes yet