Benson: CCM incheza ngoma ya CHADEMA


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Singo Kigaila Benson Masamakali

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakikushinda uchaguzi mkuu mwaka 2010 kiliangushwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pamoja na kutoshinda, CHADEMA kinaweza kujisifu kwa sasa kwamba mambo yaliyoainishwa kwenye ilani yake ya uchaguzi na ambayo CCM ilikuwa inapinga, ndiyo yanafanyiwa kazi na serikali hiyo ya CCM.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2010, CHADEMA walisema wakiingia madarakani watawapa Watanzania Katiba mpya katika muda wa siku 90 yaani wangeweka wazi utaratibu wa kidemokrasia wa kupata katiba mpya—CCM walisema katiba ya sasa inatosha.

CHADEMA walisema wakiingia madarakani watapambana na kuwashtaki mafisadi walioangamiza uchumi wa nchi—CCM haikuwa agenda yao kwani wanaosemwa ndio wafadhili wakuu wa chama.

Serikali ya CCM imejikuta ikilazimika kutekeleza ilani ya CHADEMA baada ya jamii nzima ya Watanzania kuhitaji mabadiliko na hatua dhidi ya wahujumu uchumi. CCM hakukaliki na serikalini moto.

CHADEMA waligundua kwamba vijana ni taifa la leo wakawaaminia wakawapa madaraka, CCM wanahangika kufuata nyayo hizo kwa kupunguza wazee kwenye sekretarieti yake.

Singo Kigaila Benson, Murugenzi ya Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA anasema, “CCM inacheza ngoma ya CHADEMA.”

Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya yaliyofanyika wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam, Benson, anasema sera za chama chake ni nzuri ndiyo maana CCM wamelazimika kutekeleza katika kipindi hiki kinapokabiliwa na ukosefu wa ushawishi ndani ya wanachama wake na nchi kwa ujumla.

Benson anasema, ushawishi huu unaoifanya CHADEMA ikubalike sana sasa una historia yake, kwamba baada ya kuanguka kwenye Uchaguzi Mkuu 2005, CHADEMA waliamua kujipanga upya kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba, mwaka jana.

Mwaka 2005 ndiyo ilikuwa mara ya kwanza CHADEMA kumteua mgombea urais—kilimteua mwenyekiti wa chama Freeman Mbowe ambaye hakupata kura za kutosha. Jakaya Kikwete wa CCM alishinda kwa kura za kishindo.

Mwaka 1995 CHADEMA hakikuwa na mgombea. Awali kiliamua kumuunga mkono aliyekuwa mgombea wa NCCR-Mageuzi, Augutine Mrema, lakini katika dakika za mwisho, akasema hataki ushirika.

Mwaka 2000 CHADEMA waliamua kumuunga mkono Prof. Ibrahimu Lipumba na Chama cha Wananchi (CUF), lakini 2005 kikamteua Mbowe.

Matokeo yalipotangazwa CHADEMA walikaa wakajiuliza sababu za kushindwa. Wakagundua kwamba tatizo lao lilikuwa mfumo wa chama hicho kwamba kilikuwa na uzito juu hasa makao makuu na si mikoani ambako kuna wanachama.

Wakajisahihisha. Kupitia mfumo mpya wa kupeleka madaraka kwa wanachama kuwa na wajumbe wengi wa baraza la chama kuanzia ngazi ya taifa hadi matawi (kijiji/mtaa) na mabalozi.

“Mfumo huu mpya ndio uliozaa katiba ya sasa na kutokana na sera zake bila shaka ndizo zitaingiza CHADEMA kuchukua dola kwani tayari umeonyesha njia,” anasema Benson.

“Katika uchaguzi wa mwaka 2005, tulipata wabunge watano ukijumlisha na viti maalumu tukawa na wabunge 11, lakini sasa tumepata wabunge wa majimbo 23 na ukijumulisha wale wa viti maalumu jumla yake ni 48. Mwaka 2005, tulikuwa na madiwani 102 lakini sasa wako zaidi ya 500. Na tumeunda kambi rasmi ya upinzani bungeni,” anasema.

Mabadiliko hayo ndiyo yaliyoza bendera mpya ya CHADEMA hivyo kutetemesha CCM kiasi cha kuamua kufanya mabadiliko ya ghafla katika sekretarieti kwa falsafa ya ‘kujivua gamba’.

“CCM imekifanya kile kitu kinaitwa kiini macho. Siku hizi watu wanaita huo ni usanii. Kiumbe hodari wa kujivua gamba ni nyoka. Hufanya hivyo akizeeka, lakini tabia yake ya uadui kwa binadamu iko palepale na zaidi ya hapo sumu yake inakuwa kali,” anasema.

“Ni kweli tumeona chama kimetoa wazee na kuingiza vijana ambao hatudhani kama watakuwa na tabia tofauti. Chiligati (John) ambaye alikuwa itikadi na uenezi, leo anapandishwa cheo, ana jipya gani?” anahoji.

“CCM inadhani kwamba gamba lao ni uzee. Gamba la CCM si uzee bali ni ufisadi. Kama wanaibiana ndani hatujui na hatutaki kufuatilia, lakini CHADEMA inalia na watawala wanaotoka CCM kuwa na gamba la wizi wa rasilimali za nchi,” anafafanua.

Benson anasema kwamba CCM inacheza ngoma ya CHADEMA inayopinga ufisadi unaofanywa na baadhi ya watawala—kuiba rasilimali za nchi, kuingia mikataba mibovu ya uwezekaji na kulindana.

“Sisi CHADEMA tumewapa orodha mbili kwa majina na namna watu hao walivyotafuna nchini, akiwamo Rais Jakaya Kikwete. Tulifanya hivyo mwaka 2007 na mwaka huu huko Tabora. Badala yake serikali inasema inakwenda serikali za mitaa, kufanya nini? Anza na hawa tuliowatajia,” anasema.

Orodha mpya, ambayo imetangazwa kwa kuangalia ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali, inaonyesha kwamba kuna ufisadi wa Sh 70 bilioni zilizolipwa na serikali kwa ‘mafisadi’ waliofichwa na Rais Kikwete.

“Jambo moja zuri sana kwa sasa ni kwamba CCM nao wanakiri kuna ufisadi. Walikataa sasa wanakubali. Lakini si CHADEMA waliomtuma Rais Kikwete aseme kwamba Sh 70 bilioni ziende TIB, huko haziko kwa mujibu wa CAG! Zimekwenda wapi? Amepewa nani? Kikwete atuambie ndiyo maana tumempa siku 90,” anaeleza.

Vilevile, anasema kwamba kuna Sh 48 bilioni ambazo zilikuwa kwa ajili ya kunusuru mdodoro wa uchumi wa nchi ambazo pia CAG anahoji zilizoko kwani haifahamiki aliyepewa. “Hata CAG anasema kwenye ripoti yake kwamba hajawahi kuziona,” anaongeza.

Benson anashangazwa na Rais Kikwete kushindwa kutumia mamlaka yake kushitaki ilihali ana vyombo vya usalama ili kama anasamehe basi asamehe wafungwa na si mafisadi ambao ameendelea kuwa nao ndani CC na NEC yake.

Aidha, Benson ana maoni tofauti kuhusu mkuu mpya wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Mnauye kuwa anakurupuka katika majukumu yake.

“Nape anakurupuka. Sina uhakika kama anajua anachozungumza. Nadhani ameanza na mguu mbaya, lakini tunamshukuru kwa kazi anayofanya kumtetea mwenyekiti wake, Rais Kikwete.”

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: