Berlusconi amwaibisha Waziri Mkuu wa Hispania


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly versionSend to friend
WAZIRI Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi

WAZIRI Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, alitoa kali ya mwaka wiki iliyopita baada ya kumwacha kwenye mataa Waziri Mkuu wa Hispania, Jose Luis Zapatero, kwenye mkutano wa waandishi wa habari.

Kwa kawaida, Berlusconi hufanya mazungumzo na waandishi wa habari akiwa na kiongozi anayeitembelea nchi yake lakini Alhamisi iliyopita aliaga na kuondoka wakati mkutano hata haujaanza.

Zapatero alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Italia, lakini siku hiyo alikuwa ametokea kwenye makazi ya Papa, Vatican, kabla ya mkutano wake huo na waandishi wa habari.

“Kabla hamjaanza mkutano, naomba niwaache na mheshimiwa waziri mkuu ili mumuulize maswali mtakayo. Kama mjuavyo, mwenzetu ndiyo kwanza ametoka Vatican na hivyo nina hakika ana baraka nyingi sana hivi sasa,” alisema Berlusconi kabla ya kuondoka huku akitabasamu.

Vyombo vya habari vya Italia pamoja na wachunguzi wa masuala ya kisiasa nchini humo walilaumu sana kitendo hicho cha waziri mkuu huyo na kusema kilimvunjia mno heshima mwenzake.

Magazeti ya kawaida na magazeti ya kwenye mitandao maarufu kwa jina la blogu yalijaa maneno makali dhidi ya kiongozi huyo ambaye hata hivyo amekuwa mwingi wa habari katika utawala wake.

Zapatero mwenyewe alionekana kushangazwa na hatua hiyo ya Berlusconi ambayo hakuna aliyeitegemea ingawa alijitahidi kutabasamu kwa dakika chache kabla hajaanza mkutano wake huo na waandishi wa habari.

Hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Italia, imepinga madai hayo ya Berlusconi kumdhalilisha Zapatero, ikisema hakukuwapo na chochote cha ajabu.

“Berlusconi hakukimbia kutoka mkononi. Alitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kuondoka kwake. Alimshika mkono mwenzake (Zapatero) na kumuaga vizuri. Alikuwa na udhuru na ndiyo maana aliondoka mapema,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo.

Hakuna lolote la ajabu. Lipi hasa lilikuwa la ajabu jamani?" Tatizo la waandishi wa habari ni kukuza mambo ambayo katika hali ya kawaida hayana umuhimu wowote, alisema msemaji wa Berlusconi, Giuseppe Bonauiti.

0
No votes yet