Bila uhuru hakuna maendeleo


Fred Mpendazoe's picture

Na Fred Mpendazoe - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version

SHEREHE na shamrashamra nyingi mwaka jana zilikuwa juu ya Tanzania Bara au Tanganyika kutimiza miaka 50 ya uhuru. Tanganyika ilipata uhurutarehe 9 Desemba 1961 na mwaka mmoja baadaye ikawa Jamhuri baada ya kujikomboa toka mikononi mwa ukoloni wa nchi ya Uingereza.

Hivyo basi tarehe 9 Desemba 2011, Tanzania Bara ilifikisha miaka 50 ya kujitawala. Maandalizi ya kusherekea miaka 50 ya uhuru yalifanyika nchi nzima.

Swali walilojiuliza mwaka jana, wakati wa kuadhimisha na baada ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru, je umri wa miaka 50 wa kujitawala na maendeleo tuliyonayo vinalingana?

Katika kitabu cha Binadamu na Maendeleo cha Mwalimu Nyerere (1974),  uhusiano kati ya uhuru na maendeleo umefafanuliwa hivi, “Uhuru na maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana; uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai! Bila ya kuku hupati mayai, na bila mayai kuku watakwisha. Vile vile, bila uhuru hupati maendeleo, na bila maendeleo uhuru utapotea”.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alilielewa hili, na katika uongozi wake wa miaka 23 alilisimamia kwa nguvu. Kwanza tunapozungumzia uhuru maana yake ni kwamba, upo uhuru wa nchi, yaani uwezo wa wananchi kujipangia maisha yao, kujitawala wenyewe bila kuingiliwa na mtu au nchi yoyote.

Pili kuna uhuru wa kutosumbuliwa na njaa, kuna uhuru wa kutosu na maradhi, na kutosumbuliwa na umaskini.  Tatu, kuna uhuru wa mtu binafsi yaani haki ya mtu kuishi, akiheshimika sawa na wengine na uhuru wake wa kusema au kutoa maoni yake kuhusu mambo yanayogusa maisha yake, na uhuru wa kutokamatwa ovyo na kutiwa ndani kwa kuwa tu kamuudhi mkubwa fulani.

Uongozi wa Mwalimu Nyerere ulitambua na kusimamia kupatikana kwa uhuru huo kwa kila raia kwani bila uhuru huo maendeleo hayawezi kupatikana. Chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilisimamia misingi ya haki, usawa na kujitegemea. CCM ni chama kilichopigania maskini na wanyonge. Kilitambulika kama chama cha wakulima na wafanyakazi.

Ni dhahiri awamu ya kwanza ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, Tanzania ilipiga hatua kimaendeleo. Awali nimeeleza uhusiano uliopo kati ya uhuru na maendeleo. Kumbuka bila maendeleo uhuru uliopatikana utapotea kama ilivyo uhusiano kati ya kuku na yai. Bila mayai kuku watakwisha.

Popote duniani, katika nchi yoyote, maendeleo hupatikana kutokana na uongozi imara wa chama tawala na ustawi wa demokrasia. Uongozi imara na demokrasia ni vitu muhimu katika kupatikana kwa maendeleo popote pale.

Tatizo la uongozi mbovu ndani ya CCM ambalo ni la muda mrefu limedhorotesha kasi ya maendeleo nchini.

Tanzania imefikisha miaka 50 chini ya uongozi wa CCM. Ni ukweli ulio wazi kwamba nchi yetu iko katika misukosuko kijamii, kisiasa na kiuchumi. Taifa haliko salama tena. Watanzania hawako huru tena na hali inasikitisha sana.

Mwaka 1995 Mwalimu alipokuwa akimnadi mgombea urais, Benjamin Mkapa alisema “Kutokana na umri wake kuwa mkubwa, watu wengi wasiofaa wamejiingiza na kuichafua CCM.

Ndani ya CCM kuna watu wengi wa ajabu sana. Wapo wala rushwa, wezi, watu wasio na maadili, walevi wa madaraka. CCM limekuwa kama kokoro linalosomba viumbe vinavyofaa na visivyofaa”.

Kutokana na hali hiyo ya CCM kupokea watu wa aina zote na hasa wakati wa uchaguzi imekuwa chama cha kushinda uchaguzi tu badala ya kuwa chama chenye kutoa uongozi bora.

CCM imepoteza dira na mwelekeo wake, kimeacha misingi yake. Kwa sasa ni kivuko kuelekea kupata utajiri. CCM ya Nyerere si CCM ya leo.  Maendeleo yaliyopatikana wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere hayapo tena. Na matokeo yake uhuru uliopatikana unatoweka kwani bila maendeleo uhuru utapotea.

Wafanyakazi wana uhuru gani leo, wakati hawawezi kujadiliana na serikali yao waliyoichagua juu ya mishahara yao?

Wakulima wa pamba, kahawa na korosho na wafugaji wana uhuru gani wakati hawana uhakikika na mahali pa kuuzia mazao yao?

Raia ambaye hana uhakika wa mlo mmoja ana uhuru gani leo na wanafunzi wa vyuo wana uhuru gani wakati fedha zao wakubwa wanafanyia biashara? Mtanzania anayepigwa mabomu akidai haki zake ana uhuru gani?

Bila uongozi imara hakuna maendeleo, bila maendeleo uhuru utapotea. Uhuru wa Watanzania sasa unapotea kwani hakuna maendeleo tena.  Chini ya uongozi wa miaka 10 wakati wa Mkapa, serikali ya CCM iliuza mashirika ya umma na kuingia mikataba mibovu kwenye sekta ya madini, na iliuza  nyumba za watumishi wa umma.

Na Chini ya uongozi wa miaka 6 wa Kikwete (2005 – 2011) CCM na serikali ya CCM imekumbwa na kashfa nzito za Richmond/ Dowans, ukodishaji holela wa reli ya kati, uuzaji wa shirika la UDA na kushindwa kutoa suluhu ya kashfa za EPA, Meremeta na Deep Green Finance.

Ni dhahiri, CCM imeshindwa kutoa uongozi imara na kusababisha kasi ya maendeleo kufifia. Miaka 50 ya Uhuru na maendeleo yaliyopatikana hayalingani kabisa, na ni dhahiri kabisa uhuru wa Watanzania unaanza kupotea. Ni kweli, bila maendeleo uhuru utapotea.

Maendeleo yaliyojengwa kwa miaka 23 chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere yanatoweka kwa kasi kubwa.  Inasikitisha.

Rai yangu kwa Watanzania ni kwamba, baada ya kuadhimisha miaka 50 ya kujitawala tujitahimini na tujiulize ni wapi tulipojikwaa.

Kwa maoni yangu, tunahitaji mabadiliko ya mfumo wa utawala na mfumo wa namna ya kupata viongozi ngazi zote. Katiba Mpya ituelekeze namna ya kupata viongozi adilifu.

0
No votes yet